November 21, 2024

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Gachagua kunyoa au kusuka Bunge la Seneti wiki ijayo

 

BUNGE la Seneti nchini Kenya, litaanza kujadili hoja ya kumuondoa ofisini, Naibu wa Rais, Rigathi Gachagua, Jumatano na Alhamisi, wiki ijayo. Inaripoti Mitandao ya Kimataifa … (endelea).

Seneti limepokea hoja kutoka kwa kiongozi wa walio wengi Aaron Cheruyot, baada ya bunge la kitaifa, kupiga kura ya kumtimua Gachagua jana Jumanne.

Bunge zima la Seneti litachunguza mashtaka dhidi ya Gachagua na kusikiliza ushahidi kutoka pande zote.
Gachagua alitimuliwa jana Jumanne tarehe 08 Oktoba 2024, baada ya wabunge 281, kupiga kura ya kuunga mkono kuondolewa kwake ofisini.

Kiwango kilichowekwa na katiba ni angalau wabunge 233.

Katika kura za jana, wabunge 281 waliunga mkono hoja hiyo, na 44 waliipinga; na kufikia theluthi mbili ya kura zilizohitajika ili kupitisha uamuzi wa kumuondoa ofisini.

Hoja hiyo imepelekwa bunge la Seneti, ambalo litafanya kazi kama mahakama ya kesi na litatoa uamuzi wa mwisho ndani ya siku 10. Ili atimuliwe, theluthi mbili ya kura za wabunge wa seneti inahitajika.

Kabla ya kupigiwa kura jana, Gachagua alijitetea mbele ya bunge na kuwasilisha ushahidi wa kupinga mashtaka 11 yanayomkabili.

Kiongozi huyo, anakabiliwa na tuhuma za ufisadi, kumhujumu rais na kuendeleza mgawanyiko wa kikabila, madai ambayo ameyakana akisema anafanya kazi kwa maslahi ya Wakenya.

Juzi Jumatatu, Gachagua alisema: “Sina nia ya kujiuzulu wadhifa wangu na nitapambana hadi mwisho.”
Wachambuzi wa siasa za Kenya wameeleza kuwa hadi hoja ya kumwengua Gachagua inafika bungeni, ina baraka zote za Rais William Ruto.

Licha ya kumwomba msamaha rais Ruto akiwa ibadani Jumapili iliyopita, Gachagua alisema uamuzi huo haumaanishi kwamba ana makosa mbele ya Wakenya.

About The Author