December 22, 2024

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Dk. Biteko azitaka wizara, taasisi, wakala wa serikalini kutenda bajeti ya kutosha Shimiwi

 

WIZARA, Taasisi, Mashirika, wakala  za Serikali zimetakiwa kutenga Bajeti ya kutosha kwa ajili ya kushiriki Michezo ya SHIMIWI ili kukidhi malengo na misingi ya kuanzishwa kwa kwa michezo hiyo na kuleta tija. Anaripoti Mwandishi Wetu, Morogoro … (endelea).

Agizo hilo limetolewa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko wakati akimwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan kufungua mshindano ya  38 ya SHIMIWI yanayoendelewa mkoani Morogoro ambapo amesema hatopenda kusikia visingizio vya aina yoyote kutoka kwa wale wasiotuma washiriki.

“Kama tumekubaliana kufanya jambo lazima tulifanye jambo linakuwa ni lazima siyo hiari, Kama kuna sababu ya kuliboresha tuboreshe kwa kufanya mabadiliko na siyo kukubaliana bila kufanya utekelezaji” amesema Dk. Biteko na kuongeza kuwa michezo hiyo inafanyika kwa mujibu wa sheria na kama kuna changamoto zibainishwe na kufanyiwa marekebisho.

Agizo la Dk. Biteko linafuatia kushuka kwa idadi ya vilabu vinavyoshiriki mashindano hayo kutoka 74 mwaka 2023 hadi 66 mwaka 2024 jambo ambalo amesema linaashiria uwepo wa changamoto katika uendeshaji wa michezo ya SHIMIWI na hivyo kuwaagiza waajiri na Wakuu wa Taasisi ambao hawakutuma washiriki kutoa maelezo juu ya uamuzi wao kwa ajili ya hatua siku zijazo.

Dk. Biteko pia amewataka watumishi wa umma kutoa huduma bora kwa watanzania bila kuzingatia tofauti zao, kuzingatia matumizi ya TEHAMA, Ushirikishaji wa Serikali na sekta binafsi katika kuelekea maendeleo ya pamoja na kuzingatia Utawala wa Sheria, taratibu pamoja na kushirikisha makundi ya watu wenye mahitaji maalum.

Amesema Mashindano ya aina hiyo mbali na kuwauganisha watumishi, lakini yanawezesha mshikamano miongoni mwao na kujenga afya ambayo ndio msingi watendaji bora wa kazi na wenye tija.

Akizungumzia uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Dk. Biteko ametaka wasimamizi wa Michezo ya SHIMIWI kutao siku maaluma kwa ajili washiriki kupata fursa ya kwenda kujiandikisha katika makazi yao ili kuwawezesha kupata sifa ya kuwachagua viongzi wanaowataka.

“ Najua mnaendelea na SHIMIWI kwa siku kadhaa, viongozi waangalie namna ya kuwapa fursa ili mkajiandikishe kwa ajili ya kuwachagua viongozi wenu,” amesema Dk. Biteko.

Kwa upande wake Katibu Mkuu  Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora Juma Mkomi amewataka watumishi kujenga mtandao wa kufahamiana na kuelimishana katika masuala ya kazi huku wakishiriki michezo ili kuboresha afya ambayo ni mtaji katika utumishi wao.

Naye Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma ameishukuru serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendeleza sekta ya michezo na kusema kwa sasa kuna mafanikio makubwa kitaifa na kimataifa yaliyofikiwa katika sekta ya michezo nchini.

Amesema wizara itaendelea kufanya kazi kwa bidii kuhakikishaTanzania wanaendelea katika michezo mbalimbali sambamba na kuibua na kuonesha vipaji fiche miongoni mwa wanamichezo.

Awali Mwenyekiti wa SHIMIWI, Daniel Mwalusamba amesema lengo la michezo kuwajenga watumishi wanaozingatia misingi ya uzalendo, kujitolea kulipa kodi, wasikivu kwa serikali iliyoko madarakani.

Hata hivyo amesema michezo hiyo inakabiliwa na changamoto ikiwemo kushuka kwa mahudhurio kwa idadi ya vilabu vya washiriki.

Mashindano ya SHIMIWI mwaka 2024 yamebebwa na Kauli mbiu “Michezo uongeza utendaji kazi, Shiriki uchaguzi Serikali za Mitaa kwa ujenzi wa Taifa Endelevu.

About The Author

error: Content is protected !!