RAIS wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni amekutana na kufanya mazungumzo na Rais mstaafu wa Tanzania na Mwakilishi Maalum wa Umoja wa Afrika (AU) kwa Ukanda wa Pembe ya Afrika na Bahari ya Shamu, Jakaya Mrisho Kikwete. Anaripoti mwandishi wetu, Dar es Salaam …(endelea).
Mazungumzo hayo yamefanyika katika Ikulu ndogo ya Nakasero jijini Kampala, Jumanne 7 Aprili 2027.
Katika kikao hicho, viongozi hao walijadili kwa kina hali ya kisiasa na kiusalama nchini Sudan Kusini, wakisisitiza umuhimu wa kuendeleza mazungumzo ya amani na maridhiano kati ya pande zote zinazohusika ili kurejesha utulivu wa kudumu.
Rais Museveni alieleza kuwa Uganda itaendelea kuunga mkono juhudi za kuleta amani nchini humo, akibainisha kuwa utulivu wa Sudan Kusini, hususan katika eneo la Equatoria lenye idadi kubwa ya raia wa Uganda, una mchango mkubwa kwa usalama wa kikanda na maendeleo ya kiuchumi.
Kwa upande wake Kikwete alisisitiza dhamira ya Umoja wa Afrika katika kusimamia na kuimarisha juhudi za upatanishi katika ukanda huo.
Uteuzi wake kama Mwakilishi Maalum unalenga kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kuchochea suluhu ya kudumu ya migogoro katika Pembe ya Afrika na Bahari ya Shamu, maeneo yanayokabiliwa na changamoto za kiusalama na kisiasa.
ZINAZOFANANA
Guterres apongeza sitisho la vita
Hongereni Wananchi mmeilinda Iran-Mojtaba Khamenei
Trump ajigamba kushinda vita dhidi ya Iran baada ya makubaliano