May 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Zungu arejea uenyekiti wa Bunge, wawili wapya

Mussa Zungu

Spread the love

 

BUNGE la Tanzania, limewathibitisha, Mbunge wa Ilala, Mussa Azan Zungu; Mbunge Viti Maalum, Najma Murtaza Giga na Mbunge wa Mufindi Kusini, David Mwakiposa Kihenzile kuwa wenyeviti wa mhimili huo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Zungu ni Mwenyekiti Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Giga ni Makamu Mwenyekiti Kamati ya Kudumu ya Bunge, Katiba na Sheria pamoja na Kihenzile ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge, Viwanda, Biashara na Mazingira, wamethibitishwa kushika nafasi hizo leo Jumatano tarehe 12 Mei 2021, bungeni jijini Dodoma.

Wabunge hao walipitishwa bila kupingwa, baada ya idadi yao kukidhi mahitaji ya nafasi zilizokuwa zinagombaniwa, pamoja na kukidhi vigezo vinavyohitajika hasa jinsia na uwakikishi wa watu kutoka katika pande zote mbili za muungano, Tanzania Bara na Zanzibar.

Awali, Naibu Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson aliwasilisha majina yao ambayo yalipitishwa na Kamati ya Uongozi wa Bunge, Jumatatu tarehe 10 Mei 2021.

Akiwasilisha majina hayo, Dk. Tulia alisema Kamati ya Bunge ya Uongozi ilipendekeza majina matatu, ambayo yanakidhi idadi ya nafasi zilizokuwa zinagombaniwa.

“Bunge liliweka utaratibu kwamba chaguzi zinazofanyika, iwapo iddi ya wagombea inalingana na nafasi zilizopo na vigezo vinavyohitajika vimetimizwa basi wagombea hao wanapita bila kupingwa,” amesema Dk. Tulia.

Naibu Spika huyo wa Bunge amesema utaratibu huo wa wagombea uenyekiti wa Bunge kuoita bila kupingwa, ulifanyika katika chaguzi za Bunge la 10 na 11.

Baada ya kueleza hayo, Dk. Tulia aliwahoji wabunge kama wanawathibitisha, ambao kwa kauli moja walikubali.

error: Content is protected !!