Friday , 3 February 2023
Home Gazeti Habari Mchanganyiko Zuio uvuvi Kambamiti: Serikali yatoa matumaini
Habari Mchanganyiko

Zuio uvuvi Kambamiti: Serikali yatoa matumaini

Spread the love

 

SERIKALI imeagiza Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI), irudie upya utafiti iliyoufanya kuhusu uvuvi wa samaki aina ya Kambamiti. Anaripoti Nasra Bakari, DMC…(endelea).

Agizo hilo limetolewa leo Jumatano tarehe 19 Mei 2021, bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega, akimjibu Mbunge wa Kibiti (CCM), Twaha Mpembenwe,aliyeitaka Serikali iondoe zuio la uvuvi wa Kambamiti, ili kunusuru uchumi wa wananchi wa jimbo lake.

Mwaka 2018, TAFIRI ilifanya utafiti juu ya uvuvi wa samaki aina ya Kambamiti, uliobaini upungufu wa samaki hao baharini, kitendo kilichosababisha Serikali izuie kwa muda uvuvi wake.

Akizungumzia zuio hilo, Ulega amesema Serikali imeagiza utafiti huo urudiwe upya, ili suluhu ya kudumu ipatikane badala ya kuzuia watu wasivue samaki hao.

“Tumeshaelekeza TAFIRI kwa kushirikiana na idara yetu kuu ya uvuvi, ifanye mapitio ya utafiti tulioufanya na sasa tutakwenda kuufanya zaidi, kwa kushirikiana na wananchi wenyewe na wadau katika maeneo yote haya ili tupate suluhu ya kudumu,” amesema Ulega.

Ulega amesema kuwa, lengo la hatua hiyo ni kuhakikisha wananchi wa Jimbo la Kibiti na Mkuranga wanaotegemea uvuvi wa samaki hao, wanufaike na rasilimali za nchi pamoja na kuchangia pato la Taifa.

“Katika miaka mitano iliyopita wananchi Mkuranga na Kibiti wamezalisha tani 1,200 za Kambamiti, zenye thamani ya Sh. 16 Bil. na zikaingiza serikalini Sh. 600 Mil. Tunataka tutoke hapo, tuongeze uzalishaji zaidi ili waondokane na umasikini ulioenea eneo hili wakati wamekalia rasilimali kubwa sana,” amesema Ulega.

Naibu Waziri huyo wa Mifugo na Uvuvi amesema, utafiti huo utabainisha mbinu mbadala za kuwasaidia wavuvi hao kuzalisha katika majira yote ya mwaka.

“Ni ukweli usiopingika kwamba wananchi wa maeneo wamekuwa wakihifadhi maeneo haya, samaki wanapokuwa wamekua wanaondoka katika bahari kuu. Matokeo yake wavuvi wanakosa uwezo kuwafikia samaki hawa,” amesema Ulega.

Ulega amesema “Nimelekeza pamoja tufanye kazi ili kuondokana na mazoea ya kuwazuia, badala yake tutafute njia mbadala kuwafanya wananchi wawe na uwezo wa kufaidi rasilimali hii.”

Naibu Waziri huyo amesema, awali Serikali iliweka vipindi maalum vya uvuvi wa Kambamiti ili waweze kuzaliana na kukua.

“Serikali imeweka utaratibu kwa ajili ya uvuvi wa Kambamiti kwa wavuvi wadogo na wakubwa, uvuvi huo kwa mujibu wa Sheria na Kanuni zilizopo unaruhusiwa kufanyika kuanzia mwezi Machi hadi Septemba kila mwaka kwa ukanda wa Kaskazini unaohusisha Wilaya za Bagamoyo, Pangani na Chalinze,” amesema Ulega na kuongeza:

“Na kuanzia mwezi Aprili hadi Agosti kila mwaka, kwa ukanda wa Kusini unaohusisha Wilaya za Mkuranga, Kibiti na Kilwa. Kipindi kilichobaki kimeachwa ili Kambamiti waweze kuzaliana na kukua. Maamuzi haya yamefanyika baada ya taarifa za utafiti wa Kisayansi na kuzingatia uendelevu wa Rasilimali hii.”

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari Mchanganyiko

Wadau wataka kasi iongezeke marekebisho sheria za habari

Spread the love  WADAU wa tasnia ya habari wametakiwa kuongeza juhudi katika...

Habari Mchanganyiko

TEF yawatuliza wadau wa habari marekebisho vifungu kandamizi

Spread the love  JUKWAA la Wahariri Tanzania (TEF), limewataka wadau wa habari...

Habari Mchanganyiko

Ndege ya Precision Air yaahirisha safari kwa hitilafu, nyingine yatua kwa dharura

Spread the love  NDEGE ya Shirika la Precision Air imeshindwa kufanya safari...

Habari Mchanganyiko

NMB yakabidhi vifaa tiba hospitali Mtwara  

Spread the loveBENKI ya NMB Kanda ya Kusini imetoa msaada wa vifaa...

error: Content is protected !!