January 17, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Zuhura Yunus kuondoka BBC

Spread the love

 

MTANGAZAJI maarufu wa Shirika la Utangaza la Uingereza (BBC), Zuhura Yunus ametangaza kuondoka ndani ya shirika hilo alilolitumika kwa miaka 14 kwa mafanikio makubwa. Inaripoti BBC…(endelea).

Habari iliyoandikwa na na BBC imesema, Zuhura ambaye ni raia wa Tanzania, alijiunga na shirika hilo mwaka 2008 kama mtangazaji wa redio na mzalishaji wa vipindi.

Atatangaza kipindi chake cha mwisho cha Dira ya Dunia leo Ijumaa saa 3:00 usiku.

Habari hiyo inasema, mtangazaji huyo amesema anataka kuutumia muda wake sasa kuendelea na uandishi na mambo mengine nje ya BBC.

Taarifa ya Zuhura kuondoka BBC inakuja miezi kadhaa baada ya kuandika kitabu chake cha wasifu wa Biubwa, Amour Zahor mwanaharakati mwanamke wa kisiasa wakati wa mapinduzi ya Zanzibar mwaka 1964.

Zuhura mwaka wa 2014 alihamia Swahili TV na akawa mwanamke wa kwanza kutangaza Dira ya Dunia.

Miongoni mwa kazi za kipekee alizofanyia BBC World Service ni pamoja na makala kuhusu meli kuu zaidi iliyoundwa na Ujerumani wakati wa vita vya kwanza duniani ambayo bado inatumika huko Kigoma Tanzania.

Mwaka wa 2019 aliweka historia nyingine kama mtangazaji wa kwanza kutangaza kipindi cha Focus kwenye Afrika TV na kuwa Mtanzania wa kwanza kutangaza katika BBC World News akiwa amevalia hijab.

Mhariri wa Africa TV, Ian Booth kupitia ujumbe wa barua pepe akitangaza kuondoka kwa Zuhura alisema ‘Zuhura tutakukumbuka sote na tunakutakia kila la kheri kwa siku zijazo. Nina hakika kwamba hivi karibuni tutakuona ukifanikisha mambo makubwa!’

Mhariri wa BBC Swahili, Caroline Karobia alimtaja kama “mwanahabari wa kipekee ambaye mahojiano yake na viongozi wa nchi, upinzani na wanaharakati yalikuwa ishara ya uanahabari wa kuigwa.”

“Tutakosa sana mchango wake na kufanya kazi naye, tabasamu lake ilimpa kila mtu uchangamfu,” amesema Caroline
Mtangazaji mwenzake, Mariam Omar naye alikumbuka safari yake na Zuhura tangu walipokuwa katika Swahili radio. Mariam katika ujumbe wake ameandika;

“Nina historia nzuri na Zuhura tangu alipojiunga na Swahili Radio, nilipewa jukumu la kuwa mshauri wake sijawahi kuwa na wakati mgumu naye- tumetoka mbali…ni historia ndefu.”

Mwandishi mwingine wa BBC Dinah Gahamanyi alimtaja Zuhura kama mtu mkarimu na mcheshi.

“Huwezi kukosa furaha ukifanya kazi na Zuhura na ilikuwa rahisi kushirikiana naye mkifanya kazi,” amesema Gahamanyi

error: Content is protected !!