October 3, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Zitto, wenzake wasafirishwa usiku kwa karandinga

Spread the love

JESHI la Polisi Mkoa wa Lindi limemsafirisha usiku kwa usiku Zitto Kabwe, kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo na wenzake kutoka Kilwa Masoko kwenda Lindi mjini. Anaripoti Faki Sosi, Kilwa … (endelea).

Wengine kwenye msafara huo ni Akida Mawanja, Mlinzi wa Zitto, Shaweji Mketo Mkurugenzi wa Oganaizesheni, Swalehe Mketo, aliyekuwa diwani wa CUF Kibata na Abubakari Kama, Mwenyekiti wa Jimbo Kilwa Kusini.

Pia, Isihaka Mchinjika, Mwenyekiti wa Mko wa Lindi, Selemani Bungara maarufu Bwege Mbunge Kilwa Kusini, na Mahadhi Mangona Katibu Mwenezi wa jimbo hilo.

Viongozi hao wote  walisafirishwa pamoja na Zitto isipokuwa Bwege baada ya kukamatwa jana Jumanne asubuhi tarehe 23 Juni 2020 walipokuwa wakiendelea na kikao cha ndani Kilwa Masoko.

Bwege hakusafirishwa kwa kile kilichoelezwa aliugua ghafla akiwa kituoni Kilwa Masoko na kupelekwa hospitalini kwa matibabu.

Zitto Kabwe, Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo akiwa ndani ya gari ya Polisi wilaya ya Kilwa baada ya kukamatwa akiwa katika mkutano wa ndani

Baada ya kukamatwa waliwekwa kituoni Kilwa tangu asubuhi ya jana hadi ilipofika saa 2 usiku ndipo wakasafirishwa kwenda Lindi Mjini zaidi ya kilomita 190.

Gari ya Polisi iliyompakia Zitto na wenzake ilifika Lindi Mjini saa 7:05 usiku tangu ilipoanza safari saa 2:00 usiku kutoka Kilwa Kivinje.

Baada ya kufika Lindi mjini, wafuasi wawili wa ACT-Wazalendo waliwapelekea chakula kituoni hapo lakini Polisi waliwakatilia.

Polisi wanawatuhumu viongozi hao kufanya mkutano na maandamano bila kibali na huenda wakapandishwa kizimbani leo Jumatano.

Zitto alifikwa na kanzia hiyo akiwa katika siku ya pili ya ziara yake katika mikoa ya Kusini yenye lengo la kujiimalisha kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 2020.

Endelea kufuatilia MwanaHALISI ONLINE na MwanaHALISI TV kwa habari zaidi

error: Content is protected !!