Saturday , 22 June 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Zitto: Tusiishangilie Bajeti 2019/20, ashusha data
Habari za SiasaTangulizi

Zitto: Tusiishangilie Bajeti 2019/20, ashusha data

Spread the love

ZITTO Kabwe, Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, ameeleza kwamba, kuna mashaka makubwa katika takwimu za serikali kuhusu ukuaji wa pato la taifa na la mtu mmoja mmoja. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).

Amesema, takwimu zilizoelezwa na Dk. Philip Mpango, Waziri wa Fedha na Mipango wakati wa kuwasilisha Makadirio na Mapato kwa Mwaka wa Fedha 2019/20 kwamba, uchumi umekuwa kwa asilimia 7, zina mashaka kulinganisha na takwimu zingine za serikali.

Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kigoma Mjini, amechambua bajeti ya 2019/20 mbela ya wanahabari leo tarehe 16 Juni 2019, Makao Makuu ya chama hicho yaliyopo Kijitonyama, jijini Dar es Salaam.

Kwenye uchambuzi wake amesema, takwimu halisi zinaonesha kwamba, mapato ya serikali yamekuwa yakishuka mara kwa mara kinyume na inavyoelezwa.

“Kuna mashaka makubwa na kasi ya ukuaji wa mapato ya serikali, tumejaribu kuangalia miaka iliyopita, yaani mwaka 2013/14, 2014/15, 2015/16, 2016/17, 2017/18 na 2018/19, tunaona kasi ya ukuaji wa mapato imeshuka mpaka asilimia 2. Kwa hiyo ukisema serikali inaongeza mapato, ni ulaghai mtupu, ni uongo.

“Na sasa hivi utaona ndio maana wanakutana na wafanyabiashara, wanawafurahisha furahisha kwasababu wamegundua mapato yameshuka, na haya ni matokeo ya maamuzi ya kwanza kwenye bajeti ya kwanza ya serikali hii,” amesema Zitto.

Kiongozi huyo wa ACT-Wazalendo, ameeleza kushangazwa na kauli ya serikali kwamba, pato la taifa linakuwa kwa asilimia saba na kuwa, mwaka jana lilikuwa asilimia 6.8.

“Tumefanya marejeo. Tunatilia mashaka hizi takwimu. Hesabu za Benki ya Dunia zinaonesha ukuaji ni wa asilimia sita. Hesabu za Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) zinaonesha ni asilimia 4.2 kwa mwaka huu 2019, lakini mwaka jana kwenye asilimia 5 hivi,” amesema.

Akieleza sababu za mashaka hayo amesema, uchambuzi wao umekuja na hoja mbili ambazo ni takwimu zilizopo kwenye kitabu cha serikali kinachoitwa ‘Kitabu cha Hali ya Uchumi wa Taifa’ katika mwaka husika, na pili ni mtiririko wa kipato cha mtu mmoja mmoja kuanzia mwaka 2014.

Zitto amesema, kwenye kitabu hicho ‘Kitabu cha Hali ya Uchumi wa Taifa’ cha mwaka 2018, vichocheo vingi vya uchumi ambao matokeo yake ni ukuaji wa uchumi, vimeporomoka.

“Ukitazama vitu gani vinavyochochea uchumu, ni mambo matatu ambayo ni uwekezaji wa nje, misaada kutoka nje na biashara za nje zinazoingiza fedha za kigeni.

“Kwa hiyo, hivi vichocheo vyote vitatu vimeporomoka, mwaka 2017 wawekezaji kutoka nje waliingiza nchini kwetu fedha kiasi cha Dola za Marekani Bil 5. Mwaka 2018 fedha zilizoingizwa nchini kwetu (Dola za Marekani) zilikuwa 2.8. Hii maana yake zilishuka kwa takriban asilimia 44,” amesema.

Akizungumzia misaada kama kichocheo cha kukua kwa uchumi na namna ilivyoporomoka amesema, kwa mwaka 2017 misaada hiyo kutoka nje ilikuwa pesa za Tanzania Sh. 2.6 Tilioni ambapo mwaka 2018 fedha hizo zilikuwa Sh. 19. Trilioni 1.9 ikiwa zimeporomoka kwa asilimia 27.

“Nazungumzia urari wa biashara. Urari wa biashara kwa mwaka 2017 ulikuwa hasi kwa Dola za Marekani Bilioni 1.2, katika mwaka huu zimekuwa hadi kuwa Dola za Marekani 1.9 Bilioni.

“Kwenye mauzo ya Fedha za Kigeni, mwaka 2017 ziliuzwa Dola za Marekani Bilioni 2 lakini mwaka 2018 zilizouzwa ni Dola za Marekani Bilioni 1.3 tu,” amesema.

Kutokana data hizo Zitto ameeleza kuwa, hata kwenye taarifa ya Waziri wa Fedha imeeleza kuwa, mwaka huu kwenye akaunti ya akiba ya fedha za kigeni, imeporomoka kutoka zaidi ya Dola za Marekani Bilioni 5.9 mwaka 2017 mpaka Dola za Marekani Bilioni 4 mwaka jana.

“Sasa kama vichocheo hivi vya uchumi vinaonesha kuporomoka, iweje uchumi ukue kwa silimia saba kama waziri anavyosema?” amehoji Zitto.

Akizungumzia sababu ya pili amesema, kuanzia mwaka 2014, ukuaji wa pato la mtu mmoja mmoja ulikuwa ukiendana na takwimu zilizokuwepo kwa miaka hiyo mfululizo tofauti na takwimu za sasa.

“Mwaka huo (2014), wakati ukuaji wa pato la taifa ukiwa asilimia 7, ukuaji wa pato la mwananchi ulikuwa asilimia 8.9. Mtiririko huo ulikuwa kwa mwaka 2015, 2016, 2017 hivyo hivyo unaona iko juu. Sasa cha kushangaza, takwimu za mwaka 2018 zinaonesha kinyume na mwenendo huo mliouona hapo juu.

“Serikali imetangaza pato la taifa limekuwa kwa asilimia 7 mwaka 2018, wakati ukuaji wa pato la mwananchi ni asilimia 5.6. Takwimu hizi za mwaka 2018 zinatia mashaka makubwa,” amesema.

Amesema, kwa kuangalia mienendo ya miaka ya nyuma na kuangalia ripoti mbalimbali kutoka mashirika ya kimataifa, kuna uwezekano mkubwa sana kasi ya ukuaji wa uchumi ni chini ya asilimia 5.

Akizungumzia fedha za maendeleo amesema kuwa, fedha zinazotengwa kwa ajili hiyo, serikali imekuwa haizitoi zote kama ambavyo Bunge linavyopitisha na kwamba, imekuwa ikitoa chini ya asilimia 60.

“Pamoja na kwamba, bungeni tunapitisha matrilioni ya fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo, fedha ambazo zinatolewa kwa ajili ya miradi ya maendeleo hazijawahi kufikia silimia 60.

“Kwa hiyo, tusishangilie sana kwamba tumeona bajeti wametenge trilioni 33.1, na wametenga Sh. 12 trilioni kwa ajili ya maendeleo, lakini kimsingi fedha inayokwenda kule ni ndogo sana,” amesema.

Amefafanua kuwa, pamoja na serikali kutenga fedha kwa ajili ya maendeleo, zinazoelekezwa kwenye miradi ya maendeleo ni pungufu zaidi ya kile kiasi kinachotamkwa wakati wa usomaji wa Bajeti.

Amesema, serikali ya sasa tangu iingie madarakani, mpaka bajeti ya mwaka 2019/20 itakuwa imekabidhiwa zaidi ya Sh. 126 trilion na kwamba, ni wakati wa kujiuliza, je maendeleo hayo nayaoelezwa na serikali wananchi wanayaona?

“Tangu mwaka 2016, serikali imeanza kupewa fedha za wananchi kwa ajili ya maendeleo. Ni vema kupima fedha ambazo Bunge limeipa serikali na maendeleo gani serikali imefanya. Je, mwananchi wa kawaida anayaona maendeleo hayo?

“Fedha za maendeleo zinakwenda wapi? Mwaka 2016 fedha zilizotumika kwa ajili ya maendeleo zilikuwa asilimia 57, mwaka 2017 zilizotumika ni asilimia 60 na mwaka 2018 fedha za maendeleo zilizotumika zilikuwa asilimia 45.5, zingine zinakwenda wapi?”

Amesema kuwa, pamoja na bungeni kupitisha matrilioni ya fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo, fedha ambazo zinatolewa kwa ajili ya miradi ya maendeleo hazijawahi kufikia asilimia 60 ya fedha zinazotajwa kutengwa bungeni.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoTangulizi

Padre anayetuhumiwa mauaji ya Asimwe, asimamishwa

Spread the loveKanisa Katoliki Jimbo la Bukoba limemsimamisha kutoa huduma za kichungaji...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Serikali yaahidi kushirikiana na Prof. Ndakidemi kuhamasisha zao la kahawa

Spread the loveSerikali imeahidi kuungana na Mbunge wa Moshi Vijijini, Profesa Patrick...

BiasharaHabari MchanganyikoHabari za Siasa

IMF yaimwagia Tanzania trilioni 2.4 kukabili mabadiliko ya hali ya hewa

Spread the loveShirika la Kimataifa la Fedha (IMF) jana Alhamisi limesema bodi...

Habari za SiasaKimataifa

Mmoja afariki, 30 wajeruhiwa maandamano Kenya

Spread the loveMtu mmoja ameripotiwa kuuawa na wengine zaidi ya 30 kujeruhiwa...

error: Content is protected !!