Monday , 26 February 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Zitto: Serikali inaua viwanda vya ndani
Habari za SiasaTangulizi

Zitto: Serikali inaua viwanda vya ndani

Zitto Kabwe, Mbunge wa Kigoma Mjini
Spread the love

MBUNGE wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe ameitaka serikali kusimamia ipasavyo sekta ya viwanda ili kuhakikisha kinachozalishwa nchini kinakuwa na maana kwa faida ya Watanzania, anaandika Dany Tibason.

Amehimiza serikali kuvilinda viwanda vya ndani dhidi ya kuvurugwa na bidhaa za nje ambazo zinaingizwa kinyemela, vinginevyo ikubali kuwa inaviua makusudi.

Zitto ambaye ni kiongozi mkuu wa Chama cha ACT –Wazalendo, alisema serikali imekuwa ikishindwa kusimamia ushauri inaopewa na wabunge, akitolea mfano wa alichokieleza bungeni wakati wa mkutano wa bajeti mwaka jana kuhusu umuhimu wa kulindwa viwanda vya ndani.

Alikuwa akichangia hoja ya makadirio ya bajeti ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji iliyowasilishwa bungeni jana na Waziri Charles Mwijage.

“Wito wangu kwenye hili bado ni uleule, naamini ni muhimu mno kuhakikisha tunaweka utaratibu wa kisera na kisheria wa kulinda bidhaa zetu za ndan. Bado nasisitiza kuwa Serikali iendelee na juhudi za kuhakikisha kuwa tunaongeza uzalishaji wa mafuta ya kula nchini,” alisema.

Amesema amekuwa akihimiza viwanda vilivyopo nchini kulindwa na njia nzuri zaidi ya kutekeleza hilo, hususan kwa viwanda vya mafuta ya kula, ni kuzuia uagizaji wa mafuta ya kula kutoka nje ya nchi. “Uzuiaji huu utasisimua uzalishaji wa ndani wa mafuta ya kula, hasa mafuta ya mawese na alizeti,” amesema.

“Kasi ya kulinda viwanda vyetu hivi, inapaswa iwe kubwa na ya haraka sana, bado kuna maeneo yamefichika sana, tukiyakalia kimya kwa sasa madhara yake kwa nchi ni makubwa. Mfano mzuri ni bidhaa ya betri. Kuna smuggling (uingizaji wa bila kulipa kodi/magendo) kubwa ya betri kutoka nje na kuathiri kabisa hata mauzo ya ndani ya viwanda vya betri vilivyopo nchini,” amesema Zitto.

Amegusia kiwanda cha betri cha Panasonic alichosema kimeathiriwa mno na uingizwaji wa betri kutoka nchi za Asia wakati betri hizo hazilipiwi kodi hivyo bei yake kuwa ndogo kuliko betri zinazozalishwa nchini.

Mwenendo huo umesababisha kiwanda cha Panasonic kuwa hatarini kufungwa, hatua itakayolazimu Watanzania wanaofanya kazi hapo kukosa ajira, bali pia na serikali itakosa mapato ya kodi yaliyokuwa yakipatikana kutokana na kiwanda hicho kuzalisha.

“Kwa mujibu wa takwimu kutoka Ofisi ya Takwimu ya China, mwaka 2016 jumla ya betri zenye thamani ya Dola milioni 36.5 (zaidi ya Sh. milioni 81) zililetwa Tanzania. Lakini kwa upande wa Tanzania, takwimu za TRA na TBS zinaonesha Tanzania iliagiza betri za thamani ya Dola milioni 5.3 tu (wastani wa Sh. bilioni 11) kutoka China,” amesema.

Zitto amesema mtindo huo unamaana kwamba zaidi ya asilimia 80 ya betri zinazoingizwa kutoka nchini China haziingizi kodi. Kwa upande mwingine, ina maana serikali inaruhusu bidhaa za ndani ya nchi kunyimwa fursa ya ushindani wa haki na bidhaa zinazotoka nje ambazo hazilipiwi kodi.

“Jambo hili lina athari kubwa sana kwa Taifa, hasa kwenye mapato ya kodi yanayopotea. Lakini wanaoathirika zaidi ni wazalishaji wa ndani wa betri. Maana bei za bidhaa za magendo ni pungufu zaidi, na hivyo huleta ushindani zaidi kwenye soko,” amesema Zitto ambaye amehimiza ujenzi wa viwanda vipya kwa vile vilivyojengwa zamani haviendesheki mpaka kwanza mifumo yake ya uzalishaji ibadilishwe kutokana na teknnolojia ya sasa.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Hamahama Ngorongoro kutikisa maandamano ya Chadema Arusha

Spread the loveMAELFU ya wanachama na wafuasi wa Chama cha Demokrasia na...

Habari za SiasaTangulizi

Waliofariki ajalini Arusha kuagwa siku ya maandamano Chadema

Spread the loveMIILI ya watu 25 waliofariki dunia katika ajali iliyohusisha lori...

Habari za SiasaTangulizi

Serikali kuiburuzwa mahakamani ajali iliyoua 25 Arusha

Spread the loveMTANDAO wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), imeitaka...

Habari za SiasaTangulizi

Samia atoa pole ajali iliyoua 25, kujeruhi 21 Arusha

Spread the loveRais Samia Suluhu Hassan ametuma salamu za rambirambi kwa Mkuu...

error: Content is protected !!