July 28, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Zitto: Prof. Lipumba na aje

Spread the love

“CHAMA chetu hakibagui mtu.” Hiyo ni kauli ya Zitto Kabwe, Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo mbele ya waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, anaandika Charles William.

Zitto alitoa kauli hiyo baada ya wanahabari kumuuliza kuhusu ujio wa Prof, Ibrahim Lipumba, aliyekuwa Mwenyekti wa Chama cha Wananchi (CUF) kwenye chama hicho.

Kumekuwepo na taarifa kwamba, Prof. Lipumba amehamia ACT Wazalendo, Zitto amesema kuwa, hakuna taarifa hizo mpaka sasa na kwamba, kama mwanasiasa na mchumi huyo akitaka kuhamia ACT Wazalendo, atapokelewa kama watu wengine.

Zitto amesema, katika chama hicho milango ipo wazi kwa Mtanzania yoyote anayetaka kujiunga ili mradi tu, awe tayari kuzingatia na kufuata miiko na utaratibu wa chama hicho.

“Ningeshangaa sana kama swali hili lisingeulizwa, sisi kama chama pia tumezisikia tetesi hizi siku nzima ya jana, lakini kama chama hatukujadili jambo lolote kumuhusu yeye katika kikao chetu cha jana wala kingine chochote,” amesema Zitto na kuongeza;

“Ingawa sisi kama ACT Wazalendo hatuzuii mtu yoyote kujiunga na chama chetu ili mradi tu mtu huyo awe tayari kufuata na kuzingatia maadili, miiko na katiba ya chama, kwasababu hiyo ndiyo misingi ya chama chetu.”

Hata hivyo Zitto ameeleza kuwa, usambazaji wa tetesi hizo unaweza kuwa na nia ovu kwasababu ya fukuto la kidemokrasia linaloendelea ndani ya CUF.

“Ndani ya CUF kuna yanayoendelea, ambayo sisi tunapenda yamalizike kwa amani na tuendelee kushirikiana kuimarisha upinzani hapa nchini na kukabiliana na CCM. Tunadhani wanaosambaza tetesi hizo ambazo sisi hatuna taarifa nazo wanaweza kuwa na nia ovu,” ameeleza.

Kuhusu tamko la Jeshi la Polisi, kuzuia mikutano ya hadhara na ile ya ndani, Zitto amesema; “tumesikia wamepiga marufuku lakini hatujasikia wakipiga marufuku mikutano ya ndani ya kikatiba ya vyama vya siasa. Ndiyo maana sisi tulifanya Kikao cha Kamati Kuu jana.”

error: Content is protected !!