Friday , 9 June 2023
Home Gazeti Habari za Siasa Zitto: Nitampigia kura Lissu, ubunge…
Habari za SiasaTangulizi

Zitto: Nitampigia kura Lissu, ubunge…

Spread the love

ZITTO Zuberi Kabwe, Kiongozi wa ACT-Wazalendo, ametangaza kumpigia kura Tundu Lissu, mgombea urais wa Tanzania kupitia Chadema katika Uchaguzi Mkuu wa 28 Oktoba 2020. Anaripoti Mwandishi Wetu, Kigoma … (endelea).

“Kwa nafasi ya Rais wa Tanzania, mimi Zitto Kabwe, nitapiga kura kwa Tundu Lissu. Huyu ndiye mgombea wa upinzani ambaye ana nguvu ya kumshinda mgombea wa chama tawala, amefanya kampeni nchi nzima, mwitikio wa wananchi kwake ni mkubwa, ameeleza kwa ufasaha dhamira yake ya kuleta mabadiliko, sina mashaka na dhamira hiyo,” amesema Zitto

Zitto ambaye pia ni mgombea ubunge Kigoma Mjini kupitia ACT-Wazalendo, ametoa kauli hiyo leo Ijumaa tarehe 16 Oktoba 2020 alipowahutubia wananchi wa Bangwe Jimbo hilo katika mkutano wa kampeni.

“Anayotaka kuyafanya Lissu kama Rais, ni mambo hayo ndiyo yaliyonipa msukumo wa kumpigia Kura Lissu. Zaidi ninamuIni Lissu kutokana na historia yake ya kupigania haki za watu. Ninaomba kila mpenda haki na mabadiliko nchini ampigie kura ya urais ndugu Tundu Lissu ili awe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” amesema Zitto.

ACT-Wazalendo imemsimamisha, Bernard Kamilius Membe kuwa mgombea wake wa urais ambaye hata hivyo haendelei na kampeni zozote za nafasi hiyo.

Membe aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania katika utawala uliopita wa Rais mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete aliwahi kunukuliwa akisema, atakuwa tayari kumuunga mkono mgombea wa upinzani atakayekuwa na nguvu ya kuiondoa CCM madarakani.

Wakati, Zitto akitangaza kumpigia kura Lissu, hivi karibuni, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alitangaza uamuzi wa kamati kuu ya chama hicho wa kumuunga mkono Maalim Seif Sharif Hamad, mgombea urais wa Zanzibar kupitia ACT-Wazalendo.

Bernard Membe-ACT-Wazalendo

Mbowe alisema, walizungumza na mgombea wao wa urais Zanzibar, Said Issa Mohamed aliyekubali kujitoa kwa hiari ili kumuunga mkono Maalim Seif.

Kwa kauli ya Mbowe na Zitto ina maana kwamba Chadema wameiachia ACT-Wazalendo Zanzibar na ACT-Wazalendo wameiachia Chadema Tanzania kwa nafasi ya urais.

Katika mkutano wake wa leo, Zitto amesema mabadiliko ni lazima yatokee kwa sababu “nchi yetu imeumia sana Katika miaka hii mitano iliyopita. Kamwe hatuwezi kuendelea na ukandamizaji wa haki, uhuru pamoja na maisha magumu kiasi hiki.”

Maalim Seif Sharrif Hamad, Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo

“Tunapaswa sote kwa pamoja kusema sasa basi. Twende tukachague mabadiliko 28 Oktoba 2020 iwe ni siku mpya ya haki, uchuki mpya na uhuru kwa Watanzania,” amesema Zitto

Amesema, ACT Wazalendo kiliamua kushiriki kikamilifu katika Uchaguzi huu wa mwaka 2020 kwa kuweka wagombea kila ngazi, pamoja na kuzalisha Ilani ya uchaguzi iliyofanyiwa kazi vizuri na kwa umakini mkubwa.

“Hata hivyo, vikao vya chama kupitia Halmashauri Kuu na Mkutano Mkuu viliazimia kwamba viongozi wa kitaifa waendelee na juhudi za kuunganisha nguvu ya vyama vya upinzani ili kuwa na ushirikiano dhidi ya chama tawala.”

“Kutokana na uwepo wa sheria kandamizi ya vyama vya siasa, ushirikiano wa kisheria tumeona hauna maana kwetu kama chama kwani msajili wa vyama hawezi kuidhinisha jambo linalokwenda kuiondoa CCM madarakani,” amesema.

Tundu Lissu-Chadema

Zitto amesema, Kamati ya Uongozi ya chama hicho imeshauriana na kuona huu ni mwaka wa kihistoria kwa Watanzania, mwaka wa kuamua hatma ya maisha yao.

“Ni mwaka wa Watanzania kuchagua Kiongozi atakayerejesha furaha katika maisha yao, atakayeheshimu Katiba ya nchi yao, atakayejali maendeleo ya watu badala ya vitu, atakayeheshimu wanawake wa Tanzania na atakayerejesha uhuru wa watu.”

“Sisi ACT Wazalendo hatupo tayari kuwa kizuizi cha safari hii ya mabadiliko, nami kama Kiongozi wa ACT-Wazalendo,ninao wajibu wa kulieleza hilo kwa uwazi kwa niaba ya viongizi wenzangu wa Kamati ya Uongozi,” amesema Zitto huku akishangiliwa na mamia ya wananchi kwenye mkutano huo

Baada ya maelezo hayo, Zitto akatangaza kumpigia kura Lissu hali iliyoibua shangwe zaidi na kusisitiza “pale kwenye Kata ama Jimbo ambalo ACT Wazalendo tuna mgombea, tunaomba muwapigie kura wagombea wa ACT Wazalendo.”

“Pale ambapo kwenye Kata au Jimbo la Uchaguzi hakuna Mgombea wa ACT Wazalendo, lakini kuna wagombea wengine wa Vyama vya Upinzani, ACT Wazalendo tunawaomba mpigie kura mgombea wa chama cha upinzania mwenye nguvu zaidi ili kutokutawanya kura,” amesema

Amehutubia mkutano huo akitoka katika matibabu jijini Dar es Salaam baada ya kupata ajali ya gari 6 Oktoba 2020 eneo la Kalya Jimbo la Kigoma Kusini akiwashukuru kwa dua na sala walizomwombea.

“Tunamshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kutupa nafasi ya kuendelea kuishi. Ilikuwa ajali mbaya sana, Lakini Mungu hakutaka nife. Mola alitaka niishi ili nione Watanzania wakifanya Mabadiliko makubwa ya Uongozi wa Taifa letu,” amesema Zitto ambaye aliumia bega la mkono wa kushoto.

Kabla kwenda kuhutubia, amepokewa na umati wa watu katika Uwanja wa Ndege Kigoma.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaTangulizi

Ngoma bado mbichi mkataba wa Bandari

Spread the love  SAKATA la mkataba wa uendeshaji, uendelezaji na uboreshaji wa...

BiasharaTangulizi

Mkurugenzi TPA: Mkataba unaweza kuvunjwa

Spread the loveMKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA),...

BiasharaTangulizi

Mkurugenzi TPA: Mikataba ya utekelezaji bado haijasainiwa

Spread the loveMKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA),...

Habari za Siasa

Lussu: Mkataba wa DP bandarini si wa miaka 100

Spread the loveMAKAMU Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, amesema hakuna ukweli wowote...

error: Content is protected !!