September 29, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Zitto, Meya wa ACT mkutanoni Marekani

Spread the love

ZITTO Kabwe, Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo na Hussein Juma, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kigoma-Ujiji wanatarajia kuhudhuria mkutano wa siku mbili nchini Marekani utakaojadili masuala mbalimbali ikiwemo uendeshaji wa shughuli za maendeleo kwa uwazi, anaandika Charles William.

Katika safari hiyo mbali na kuambatana na Meya wa Manispaa ya Ujiji pia Zitto ameambatana na Sultan Ndoliwa ambaye ni mwajiriwa wa Manispaa hiyo.

“Watakuwa jijini Washington DC, Marekani kuhudhuria mkutano wa OGP Subnational Government Pioneers Meeting ambao utafanyika kwa siku mbili mfululizo kuanzia tarehe 15 mpaka 16 Septemba, 2016,” amesema John Patrick Mbozu, Katibu wa Kamati ya Mambo ya Nje wa ACT Wazalendo.

Akieleza shughuli watakazofanya viongozi hao katika safari hiyo, Mbozu amesema, “Pamoja na mambo mengine viongozi hao watapata fursa ya kutoa mada kuhusu uzoefu wao katika kuendesha shughuli za umma kwa uwazi.”

Katika taarifa yake hiyo kwa umma, Mbozu amefafanua kuwa, Manispaa ya Kigoma-Ujiji ambayo iko chini ya ACT Wazalendo ni miongoni mwa miji 15 duniani iliyoteuliwa kushiriki mpango wa Open Government Partnership ikiwa ni Manispaa pekee hapa nchini kuteuliwa kutokana na kufanikiwa kuiendesha Manispaa kwa uwazi mkubwa ndani ya muda mfupi toka ilipokabidhiwa.

error: Content is protected !!