Saturday , 22 June 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Zitto, Lissu wateta mazito Ubelgiji
Habari za SiasaTangulizi

Zitto, Lissu wateta mazito Ubelgiji

Spread the love

MBUNGE wa Kigoma Mjini, kupitia chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Zuberi Kabwe, yuko nchini Ubelgiji, alikokwenda kumjulia hali mwanasiasa mahiri nchini, Tundu Antipas Lissu. Anaripoti Mwandishi wetu…(endelea).

Taarifa kutoka kwa watu waliokaribu na viongozi hao wawili zinasema, mbali na kwenda kumjulia hali, Zitto ametumia ziara hiyo pia kujadiliana na Lissu jinsi ya ushiriki wa vyama vyao katika uchaguzi mkuu unaokuja.

Lissu ambaye yuko nchini Ubelgiji kwa matibabu, kufuatia kushambuliwa kwa risasi na wanaoitwa na serikali, “watu wasiofahamika,” Septemba mwaka 2017, ndiye anayatajwa ndani ya chama chake, kuwa aweza kukabiliana na Rais John Pombe Magufuli, katika uchaguzi wa 2020.

“Kwa sasa, Lissu ndiye mtu pekee na sahihi, ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na vyama vingine makini vya upinzani, kupambana na mgombea wa CCM. Hivyo mkutano wake na Zitto, hiyo ni moja ya ajenda zilizojadiliwa,” amenukuliwa kiongozi mmoja wa ACT- Wazalendo, ambaye hakupenda kutajwa.

Kauli ya kiongozi huyo wa ngazi ya juu wa ACT- Wazalendo, imekuja muda mfupi tokea Mshauri Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad, kunukuliwa akisema, chama chake kipo tayari kushirikiana na vyama vingine vya upinzani katika uchaguzi ujao.

Akizungumza wakati akifungua mkutano mkuu wa uchaguzi wa chama hicho katika jimbo la Mbagala, Maalim Seif amesema, ACT -Wazalendo, kipo tayari kushirikiana na vyama vingine vyovyote kuiondoa CCM madarakani, “ili mradi vyama hivyo viwe makini na visivyo na chembechembe ya usaliti.”

Amesema, kazi ya kuindoa CCM madarakani inahitaji mshikamano wa pamoja na madhubuti wa vyama vya upinzani na kwamba kazi hiyo haiwezi kufanywa na chama kimoja pekee yake.

Lissu na Zitto, ni miongoni mwa viongozi wa upinzani wanaoamini kuwa bila kuwapo ushirikiano madhubuti, CCM itaendelea kulitawala taifa hili kwa miaka mingine mingi ijayo.

Lissu amemuhakikishia Zitto kuwa anatarajia kurejea nyumbani muda wowote kutoka sasa, ili kusaidia ujenzi wa chama chake na kuchagiza harakati za kuwapo kwa uhuru wa vyombo vya habari, haki ya kujieleza na mikutano ya hadhara ya kisiasa na maandamano.

Katika mazungumzo yao wawili hao, mbali na kujadiliana masuala ya uchaguzi ujao, taarifa zinasema, walipata muda wa kuzungumza suala la ujio wa Lissu nchini.

Inaelezwa kuwa Lissu alimuomba Zitto, kushiriki yeye na chama chake, katika maandalizi na hata mapokezi yake na kwamba mbunge huyo wa zamani wa Singida Mashariki, alimhakikishia kiongozi mwenzake kwamba angependa ujio wake nchini, “ushirikishe kila mmoja na kila kundi.”

“Nilipokutwa na madhira yake, kila mmoja aliguswa kwa njia tofauti. Vyama vyote, vikiwamo vya siasa, mashirika ya kidini na kijamii, wote walishikamana na kuniombea kwa Mwenyezi Mungu aniponye. Nataka ninaporejea, kama ilivyokuwa nilipoondoka, iwe hivyo hivyo,” amenukuliwa Lissu akimueleza Zitto.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoTangulizi

Padre anayetuhumiwa mauaji ya Asimwe, asimamishwa

Spread the loveKanisa Katoliki Jimbo la Bukoba limemsimamisha kutoa huduma za kichungaji...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Serikali yaahidi kushirikiana na Prof. Ndakidemi kuhamasisha zao la kahawa

Spread the loveSerikali imeahidi kuungana na Mbunge wa Moshi Vijijini, Profesa Patrick...

BiasharaHabari MchanganyikoHabari za Siasa

IMF yaimwagia Tanzania trilioni 2.4 kukabili mabadiliko ya hali ya hewa

Spread the loveShirika la Kimataifa la Fedha (IMF) jana Alhamisi limesema bodi...

Habari za SiasaKimataifa

Mmoja afariki, 30 wajeruhiwa maandamano Kenya

Spread the loveMtu mmoja ameripotiwa kuuawa na wengine zaidi ya 30 kujeruhiwa...

error: Content is protected !!