Saturday , 15 June 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Zitto, Kubenea wamwaga sumu Mafia
Habari za Siasa

Zitto, Kubenea wamwaga sumu Mafia

Saed Kubenea
Spread the love

ZITTO Zuberi Kabwe, Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo na Saed Kubenea, mgombea ubunge wa Kinondoni, jijini Dar es Salaam, wameongoza mashambulizi dhidi ya utawala wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Jimbo la Mafia, kwamba wamewatelekeza wananchi wa kisiwa hicho. Anaripoti Hamis Mguta, Mafia … (endelea).

Wanasiasa hao wameeleza, Mafia iko nyuma kwa maendeleo licha ya kwamba, ina rasilimali za kutosha kwa ajili ya kufanya shughuli za kiuchumi, kwasababu ya kukosa wabunge wa kuwatetea.

Zitto na Kubenea wametoa kauli hiyo jana Alhamisi tarehe 17 Septemba 2020, wakati wakimnadi gombea ubunge wa Mafia kupitia chama hicho, Rizili Ngwali katika uzinduzi wa kampeni zake kuelekea uchaguzi mkuu utakaofanyika Jumatano tarehe 28 Oktoba 2020.

Kubenea ambaye ni mzaliwa wa kisiwa hicho alisema, hadi sasa Mafia inakabiliwa na changamoto za miundombinu ya barabara, hospitali na ghati.

“Hapa Mafia, wabunge wengi wamepita tangu mwaka 1965 hadi 2020 kutoka Chama Cha Mapinduzi.”

“Mafia ina nini cha kujivunia? Uwanja wa Ndege Mafia umejengwa na fedha za Marekani, Hospitali ya Mafia wilayani ina wodi mbili tu, mochwari na wodi ya uzazi,” alisema Kubenea.

Kubenea alisema, kwa kuwa uchumi wa Mafia unaendeshwa na shughuli za uvuvi, ilitakiwa iwe na Ghati kubwa lenye uwezo wa kuhudumia meli kubwa za mizigo.

“Nimesoma hapa, nimekulia hapa, naijua Mafia mbele nyuma, kuna kitu kimoja kinaitwa ghati lakini lile sio gati ni daraja, ghati inakaa meli kubwa inashusha mzigo, maji yakipada meli haifiki pale,” alisema Kubenea.

Kubenea amewaomba wananchi wa Mafia wamchague Riziki Shahali Ngwali kwa kuwa, alikuwa mbunge mzoefu anayefahamu vyema changamoto za kisiwa hicho na kwamba atawatetea bungeni.

“Kwa hiyo, wananchi wa Mafia mnakosa maendeleo kwasababu mmekosa wabunge wa kuwatetea, ndugu zangu wa Mafia mmeelewa sifa za Bi Riziki, ni mwanamama shupavu, tumekuwa naye bungeni, tunamjua jinsi alivyotetea Mafia,” alisema Kubenea.

Kwa upande wake, Zitto alisema, kisiwa hicho kama kingepata viongozi wanaofaa, kingekuwa na maendeleo kwa kuwa kina rasilimali za kutosha kujiendesha kiuchumi na kuwaendeleza wananchi ikiwemo bahari na ardhi inayofaa kwa kilimo.

“Visiwa vya Shelisheli wana fukwe kwa ajili ya utalii, Mafia mna fukwe kwa ajili ya utalii na maeneo mengine ambayo hayajaguswa na mtu, changamoto kubwa Mafia haiendelei ni kwasababu mmeikumbatia CCM.”

“Toka mfumo wa vyama vingi umeanza, hamjawahi kupata mbunge kutoka upinzani, hamjawahi kupatachangamoto mpya. wabunge wenu walewale,” alisema Zitto

“Kwa hiyo, lazima mngeona, hakuna bandari ya uvuvi wala hakuna meli ya uvuvi, hawajatekeleza hata moja, mkichagua ACT -Wazalendo mnachagua mbunge na mtetezi kwasababu ataweza kusema ambayo watawala hawataki kusikia, mbunge wa CCM hawawezi.”

Zitto ambaye anagombea ubunge Kigoma Mjini alisema, Mafia inatakiwa ibadili uongozi ili waone tofauti ya uongozi wa upinzani na ya CCM.

“Mafia mnahitaji kubadii chama cha siasa, hamhitaji kubadili mtu mshabadilisha sana mnahitaji kubadili chama cha siasa, muone tofauti ya wabunge wa CCM na wanaotoka upinzani.”

“Nikihesabu ahadi za CCM kuhusu masuala ya uvuvi wana ahadi 16 hawajatekeleza hata moja, na wangetekeleza yoyote ninyi Mafia mngefaidika,” alisema Zitto.

Kiongozi huyo wa ACT-Wazalendo aliwaomba wananchi wa Mafia wamchague Riziki na mdiwani wa chama hicho ili waunde Halmashauri, kwa ahadi ya kwamba wakifanya hivyo shughuli zao za kiuchumi zitaboreshwa.

“Ndio maana tunaomba mtupe miaka mitano ACT-Wazalendo, mbunge na madiwani wake, kuna baadhi ya mambo ya kawaida hayahitaji Serikali Kuu, mfano soko halihitiaji Serikali kuu ni kazi ya halmashauri.

“Mnahitaji mbunge mwenye maono, madiwani wasikivu, watendaji wazuri na tunaweza kupata miradi mikubwa,” alisema Zitto.

Alisema, ahadi ya ACT-Wazalendo kwa wananchi wa Mafia ni kuwapa bima ya afya wananchi wote, kukarabati Soko la Mafia.

“Nawaomba mumkubali Riziki alete mabadaliko na nitashirikiana naye ili mafanikio yawepo, ninachowaomba, mtupe madiwani wa kutosha tuunde halmashauri mambo yote yatakwisha, shuli za kiuchumi uvuvi tutaboresha,” alisema Zitto na kuongeza.

“Sisi tunakenda kwenye bima ya afya kwa wote na tumeeleza tutatekeleza namna gani watu wa Mafia wako 70,000 na wapiga kura 35,000 tunaweza kuunda mfumo wa hifadhi ya jamii ya Mafia ili kila MwanamMafia awe na bima ya afya.”

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaHabari za Siasa

Tanesco yawasha mtambo namba 8 Bwawa Julius Nyerere

Spread the loveNaibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko...

Habari MchanganyikoHabari za SiasaTangulizi

Samia: Wakuu wa mikoa, wilaya wanaendeleza ubabe

Spread the loveRAIS Samia Suluhu Hassan amesema bado wakuu wa wilaya na...

Habari za SiasaKimataifaTangulizi

Ramaphosa achaguliwa tena kuwa rais Afrika Kusini

Spread the loveRais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa amechaguliwa na wabunge wa...

Habari za SiasaKimataifaTangulizi

DA, ANC waridhia kuunda serikali ya mseto Afrika Kusini

Spread the loveChama tawala nchini Afrika Kusini cha African National Congress, ANC,...

error: Content is protected !!