January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Zitto Kabwe: Msaliti aliyejivika ukondoo

Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe

Spread the love

MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Zitto Zuberi Kabwe, ameanza kuweweseka. Anasema kisichopo na kusingizia wasiohusika. Anaandika Saed Kubenea … (endelea).

Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara, jimboni kwake Jumapili iliyopita, Zitto alisema, hatua yake ya kushupalia wizi katika akaunti ya Tegeta Escrow, ndiyo chanzo cha kesi yake dhidi ya Chadema kutupwa na Mahakama Kuu.

Amesema, kesi hiyo imetupwa kwa kuwa amethubutu kuwataja baadhi ya majaji kwenye wizi wa mabilioni ya shilingi katika akaunti ya Tegeta Escrow, ndani ya Benki Kuu (BoT).

Alirejea kauli hiyo, Jumatatu wiki hii, wakati akihojiwa na Kituo cha Televisheni cha ITV, kupitia kipindi cha Dakika 45.

Zitto alifungua shauri mahakamani, kuomba amri ya kuzuia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kumjadili. Alikuwa akikabiliwa na tuhuma za “usaliti, kukashifu viongozi wakuu wa chama na uchonganishi.”

Hakuna shaka kuwa kila aliyemsikiliza Zitto kwa makini na wanaofahamu mwenendo wake vizuri ndani na nje ya Chadema, atakuwa amebaini kuwa yote aliyoeleza na kukoleza, hayakuwa na ukweli. Amepotosha. Sababu ni hizi:

Kwanza, safari ya kisiasa ya miaka 10 ya Zitto Kabwe, ndani ya Chadema, ilisheheni ghiliba, ubinafsi na usaliti.

Ndani ya Chadema, Zitto amekuwa akishirikiana na wanaokivuruga chama. Wanaotuhumiwa kutaka kuangamiza maisha ya viongozi wakuu wa chama na wanaotajwa kuwa maadui wa chama.

Amekuwa akitajwa kuhusika na njama za kutaka kuondoa viongozi kinyume na taratibu. Amekuwa akitajwa kuasisi matumizi ya rushwa kipindi cha uchaguzi.

Katika kipindi chake chote cha kuwa naibu katibu mkuu na mbunge, Zitto hakukisaidia Chadema mkoani Kigoma bali alitumia Chadema kujijenga binafsi.

Kwa mfano, katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2000, Chadema ilifanikiwa kupata madiwani watano katika jimbo la Kigoma Kaskazini.

Lakini katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2005, ambapo Zitto aligombea kwa mara ya kwanza, pamoja na yeye kushinda, chama chake kilianguka kwa kupata madiwani watatu katika kata 11 zilizokuwapo.

Hii ni kwa sababu, mara baada ya kumalizika uchaguzi mkuu wa mwaka 2005, Zitto hakufanya tena kazi ya kisiasa jimboni kwake. Alikuwa na kazi ya kuvuruga Chadema.

Zitto alizunguka nchi mzima kuunda mtandao wa kusaka uenyekiti wa chama hicho; na kuhujumu baadhi ya wenzake ndani ya chama ili kujinufaisha binafsi.

Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, Chadema iliporomoka Kigoma ambako ilikuwa ngome; mkoa ukaangukia mikononi mwa NCCR- Mageuzi.

Jimboni kwa Zitto, Chadema ikaambulia madiwani wawili katika kata 15 zilizoko katika jimbo hilo. Yeye mwenyewe, pamoja na kupata msaada mkubwa kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) na serikali yake, akajikuta anashinda kwa mbinde.

Ushindi wake ulipatikana kwa maelekezo mahususi kutoka kwa Yusuf Makamba, aliyekuwa katibu mkuu wa chama hicho. Zitto mwenyewe amewahi kumtaja hata Rais Jakaya Kikwete kuwa alimsaidia “kufanikisha” ushindi wake.

Makamba aliamrisha viongozi na watendaji wa chama chake mkoani Kigoma, kumuachia ubunge huo Zitto. Amri hii ilitekelezwa na kumuacha kama yatima, Rodinson Lembo, aliyekuwa amepitishwa na CCM kuwania ubunge katika jimbo la Kigoma Kaskazini.

Naye mgombea wa urais wa CCM – Jakaya Mrisho Kikwete – pamoja na kwenda Kigoma zaidi ya mara mbili kutafuta kura na kunadi wagombea wa chama chake – hakukanyanga jimboni kwa Zitto.

Ni matokeo hayo yanayomsukuma kukimbilia jimbo jirani la Kigoma Mjini. Anabadilishana na swahiba wake, Peter Selukamba anayekwenda Kigoma Kaskazini.

Pili, Zitto siyo mwasisi wa hoja ya ukwapuaji wa mabilioni ya shilingi katika akaunti ya Tegeta Escrow. Mwasisi wa hoja hii, ni David Kafulila, mbunge wa NCCR- Mageuzi, katika jimbo la Kigoma Kusini.

Kafulila aliibua hoja ya Escrow kwa mara ya kwanza bungeni, tarehe 9 Mei 2014. Alikuwa akichangia bajeti ya ofisi ya waziri mkuu.

Alisema kiasi cha zaidi ya Sh. 200 bilioni zimechotwa katika Akaunti ya Tegeta Escrow, kinyume cha taratibu. Akataja waliohusika. Miongoni mwao, ni Prof. Sospeter Muhongo, aliyekuwa waziri wa nishati na madini; Saada Mkuya, waziri wa fedha na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Fredrick Werema.

Wengine aliowataja, ni Eliakim Maswi, katibu mkuu nishati na madini; mkurugenzi wa Shirika la umeme la taifa (Tanesco) na viongozi wengine kutoka BoT na serikalini.

Ni Kafulila aliyetaka jambo hilo lichunguzwe kwa kuwa linahusu BoT na viongozi wengine serikalini, akiwamo mwanasheria mkuu wa serikali, mawaziri wa nishati na madini na fedha, pamoja na makatibu wakuu wa wizara hizo. Tangu wakati huo na hadi sasa, Kafulila ameendelea “kufia” hoja yake hiyo.

Siyo Zitto, bali Halima Mdee, mbunge wa Chadema katika jimbo la Kawe, aliyejitokeza kusimama na Kafulila. Mdee alisimama bungeni, baada ya Mussa Zungu, mwenyekiti wa bunge hilo, kumtaka Kafulila kufuta kauli yake katika kikao cha jioni ya siku hiyo.

Kafulila aligoma. William Lukuvi, aliyekuwa waziri wa nchi, ofisi ya waziri mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), akasimama na kukana tuhuma hizo. Akamtaka Kafulila kuzifuta na kuacha kutuhumu watu.

Kumbukumbu za Bunge zinamuonyesha, Mdee akitaka spika wa Bunge kuunda Kamati Teule kuchunguza tuhuma hizi. Alisema, Kafulila ana ushahidi wa kutosha wa jambo hili. Akahoji, “…kwa nini hamtaki athibitishe?” Huyo alikuwa Mdee. Siyo Zitto Zuberi Kabwe.

Mkolezo wa Mdee na king’ang’anizi cha Kafulila, ndivyo vilivyomsukuma Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kuliahidi Bunge kufanyika uchunguzi juu ya tuhuma hizo za wizi.

Pinda alisema uchunguzi, ungefanyika kupitia ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG). Ndivyo ilivyokuwa.

Baada ya uchunguzi kufanyika na ripoti kuwasilishwa kwa spika wa Bunge, taarifa ya uchunguzi huo ikapelekwa mbele ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC). Ndivyo kanuni zinavyoelekeza.

Hapa ndipo anaingia spika Anne Makinda. Alitoa hadidu za rejea kwa PAC. Ilikuwa kazi rahisi: Soma Ripoti ya CAG, chambua vielelezo, andika taarifa na baadaye wasilisha taarifa hiyo bungeni. Hiyo ndiyo kazi ambayo “kamati ya Zitto” ilipewa kufanya. Basi!

Hakuna chochote kipya ambacho kamati hii ilileta nje ya kile ambacho CAG amekieleza. Hakipo.

Tatu, kuna mambo muhimu sana ambayo Zitto hataki kuyaeleza. Miongoni mwao ni kwamba, bila wabunge kutoka UKAWA, kuzuia mapendekezo ya kamati yake, hakuna mtuhumiwa wa Escrow ambaye angewajibishwa.

Mkakati tayari ulikuwa umeandaliwa na Zitto kwa kushirikiana na wabunge wa CCM na serikali, kuzuia watuhimiwa kuwajibika.

Hili linathibitishwa na kukwama kwa azimio la kwanza lililomhusu Stephen Masele; naibu waziri nishati na madini ambaye alikuwa anatuhumiwa kukaa kimya hadi mabilioni ya shilingi yakachotwa BoT.

Masele alikuwa anatuhumiwa pia kumshabulia, balozi wa Uingereza nchini, Dianna Melrose, kuwa anaingilia mambo ya ndani ya Tanzania; na anazishauri nchi wahisani kukata misaada, jambo lililosababisha mgogoro wa kidiplomasia.

Ni hapa ambako, Andrew Chenge – mmoja wa watuhumiwa wa Escrow – alipopewa fursa ya kupendekeza mfumo wa kuandika Maazimio ya Bunge; akilenga kuepusha tuhuma nzito zilizoibuliwa na CAG na Kafulila.

Katika hali isiyo ya kawaida; na ilikuwa karibu na usiku wa manane; Zitto Kabwe, mbele ya Bunge na kwa sauti ya unyonge na kunyenyekea, aliridhia mapendekezo ya Chenge.

Mapendekezo ya Chenge yalitaka Bunge lisiagize Rais Kikwete kuwachukulia hatua watuhumiwa.Alitaka rais ashauriwe.Akadai kuwa hiyo ndiyo kazi ya Bunge – kutoa ushauri.

Spika Makinda alipouliza iwapo maazimio yote yachukue mkondo huo wa “kushauri,” Zitto alijibu kuwa anaafiki mfumo wa mapendekezo aliotoa Chenge na kutamka kuwa yeye sasa alikuwa amechoka ubongo!

Alisema, “…nakubaliana na mapendekezo ya Chenge na naomba mapendekezo yote yafuate mkondo huo.”

Kama ni kutafuta waliofanikisha hatua za sasa kwa wanufaika wa fedha za Tegeta Escrow, Freeman Mbowe, kiongozi wa upinzani bungeni, hawezi kuachwa bila kutajwa.  Alisimama bungeni na kupinga utaratibu wa Zitto wa kujisalimisha na kutaka kubeba watuhumiwa.

Mbowe akiungwa mkono na wabunge wenzake wa UKAWA na baadhi ya wabunge kutoka CCM. Kauli ya Mbowe kwamba yeye na wenzake hawawezi kushiriki au kuonekana wanashiriki katika uamuzi batili juu ya fedha za umma; ndiyo ilifanya spika kusimamisha Bunge usiku wa manane.

Alicholenga Zitto na baadhi ya wenzake katika CCM; ambacho ni kutaka mapendekezo ya kamati yake yasikilizwe na kupitishwa kwa kura ya wengi; kilizolewa na kimbunga cha hotuba ya Mbowe.

Maazimio yaliyokuja kusomwa baadaye na Zitto, kwa kile kilichoitwa, “kupatikana kwa maridhiano,” hayakuandikwa na Zitto. Yaliandikwa na wabunge wa UKAWA. Ushahidi upo.

Lakini kama hiyo haitoshi, ni Zitto huyuhuyu aliyetetea kwa nguvu zake zote, watuhumiwa wa Kafulila – gavana wa BoT, waziri wa fedha na baadhi ya watendaji kutoka ndani ya benki kuu.

Alidai kuwa maofisa hao wa BoT na serikali, walisaidia kamati yake kupata taarifa muhimu kuhusu wizi huo. Kumbe mwizi akishiriki kukupa taarifa anasamehewa?

Katika mazingira hayo, majigambo ya Zitto kuwa amefukuzisha kazi watuhumiwa wa Tegeta Escrow, yanatokea wapi? Mbona maazimio yake yalikuwa tayari yamezikwa na Chenge?

Aidha, mpaka sasa, Zitto Zuberi Kabwe, hajaeleza juu ya madai kuwa alimegewa zaidi ya Sh. 500 milioni na Singasinga wa Pan African Power (T) Tanzania Limited (PAP).

Fedha hizi zinadaiwa kuchukuliwa na Zitto kupitia wakili wake, Albert Msando. Zitto ameishia kudai kuwa anaomba achunguzwe.Nani anayeweza kumchunguza? Marafiki zake?

Nne, kama kuna jaji aliyehusishwa na fedha za Escrow, basi si mwingine, bali ni Jaji John Utamwa. Hukumu zake mbili – Septemba 2013 na Januari 2014 – ndizo ziliruhusu kuchukuliwa kwa mabilioni ya shilingi kutoka BoT.

Lakini ni Jaji Utamwa huyohuyo, aliyetoa amri ya zuio la Zitto dhidi ya Chadema. Alitaka Zitto asikilizwe kwanza kabla ya kuhukumiwa. Aliyefuta kesi ya Zitto, ni Jaji Richard Mziray, hakutajwa katika orodha ya watuhumiwa wa Escrow.

Jaji Mziray alihamishiwa Mahakama Kuu kutoka Mahakama ya Ardhi. Alikabidhiwa faili la kesi ya Zitto baada ya Jaji Utamwa na majaji wenzake zaidi ya 60 kupata uhamisho wa kawaida wa vituo vyao vya kazi.

Zitto, akiwa raia huru wa nchi hii, ana haki ya kutoa kauli yake juu ya mambo yanayomhusu na mengine. Lakini kudai, kama anavyonukuliwa katika vyombo vya habari – na yeye hajakanusha – kuwa mahakama imesukumwa na fedha za Escrow ili kufuta kesi yake; ni kwenda mbali sana. Ni kutukana majaji.Ni kutukana mahakama.

Angalia msululu wa walioibua na kukomalia Escrow – CAG Ludovick Uttoh (kiongozi) na wafuasi, Mbunge Kafulila – hadi akaitwa “tumbiri,” mbunge Halima Mdee na mmoja wa viongozi wa UKAWA, Freeman Mbowe.

Wanufaikaji wa ukwapuaji wa mabilioni ya shilingi za Escrow, waache kuangalia orodha hiyo hapo juu, wakimbilie kudhuru PAC na Zitto, ambaye alikuwa anawakinga? Huu, ni mzaha mchafu!

Kwa msingi huu basi, ni muhimu wote wanaomsikiliza Zitto wakarejea historia hii ya Escrow. Wakarejea ndani ya chama chake. Wakarudi nyuma na kuangalia mienendo yake na wakawaangalia waliomzunguka – wale ambao anawaambia wanachotaka kusikia!

Wakifanya hivyo, watagundua kuwa bwana huyu, hajawahi kuwa mtu mwenye kutetea maslahi ya taifa kama anavyojitambulisha. Huyu amekuwa akijitetea binafsi. Amekuwa akisaliti hata harakati za mabadiliko; na amekuwa wakala wa baadhi ya maofisa wa usalama wa taifa (TISS).

error: Content is protected !!