July 1, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Zitto Kabwe: Historia haiheshimu wanaojikweza

Viongozi wa ACT-Tanzania

Spread the love

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), hatimaye kimetua mzigo uliokielemea kwa muda mrefu. Ni kuondoka kwa Zitto Zuberi Kabwe katika chama hicho.

Zitto, aliyepata kuwa naibu katibu mkuu, mbunge wa Kigoma Kaskazini na naibu kiongozi wa upinzani bungeni, “alifukuzwa” uanachama wa Chadema, Januari mwaka jana.

Alituhumiwa usaliti. Naye akakiri: Kushiriki njama za kuhujumu chama. Kushirikiana na maadui wa chama. Kuandaa “mapinduzi ya uongozi” kinyume na taratibu za chama.

Kwa mwaka mmoja na miezi miwili na siku kadhaa, Zitto alibaki ndani ya Chadema kwa amri ya mahakama. Sasa msikilize Zitto. Ni muhimu kurekodi uzandiki wake; uongo wake; ubinafsi wake na ubabaishaji wake, ili huko tuendako Watanzania na dunia nzima waweze kumwelewa na kumhukumu ipasavyo.

Katika andishi lake alilosambaza kwa vyombo vya habari, Ijumaa iliyopita, Zitto anadai:

  • Kwamba alikuta Chadema na wabunge wanane na sasa anaiacha na wabunge 48; na kwamba hayo ni mafanikio makubwa na anajivuna kuwa yamepatikana kutokana na kuwapo kwake.
  • Kwamba amejitahidi kwa kadri alivyoweza, kumaliza mgogoro wake na wenzake ndani ya Chadema, lakini jitihada zake hazikufanikiwa.
  • Kwamba kuondoka kwake bungeni kumetokana na kushindwa katika kesi aliyofungua Mahakama Kuu kupinga kuvuliwa uanachama; na kwamba hilo pia ni matokeo ya kazi zake bungeni.
  • Kwamba, hali aliyomo sasa inatokana na msimamo wake wa kutaka kuundwa kwa tume huru ya mahakama, kuchunguza tuhuma dhidi ya majaji “waliopata mgawo” kutoka kwa James Rugemalira, mmoja wa wanahisa katika kampuni ya kufua umeme ya IPTL.

Huyo ndiye Zitto. Sasa tujadili bila makengeza:

Kwanza, ni kweli yapo mafanikio yaliyopatikana wakati Zitto na wengine waliofukuzwa, wakiwa ndani ya Chadema. Bali hakuna mzani wa kujua kila kiongozi au mwanachama alichangia kiasi gani.

Akitokea mtu mmoja akasema, “Mimi ndiye nilisababisha kuchaguliwa wabunge wengi,” kama alivyokuwa akidai Augustine Mrema kabla ya kutimuliwa NCCR-Mageuzi; basi ujue ana walakini mkubwa na anastahili kupimwa afya.

Mafanikio hayashuki kutoka juu na hayaoti kutoka ardhini. Yanatokana na ushirikiano wa pamoja ndani ya chama. Yanatokana na mipango iliyobuniwa na kutekelezwa kwa mbinu thabiti na usimamizi imara.

Siri ya mafanikio ya Chadema, ikiwa ni pamoja na kupatikana kwa wabunge wengi, ni wananchi kukikubali chama na kukiunga mkono.

Wananchi wameelewa kuwa Chadema imedhihirisha uwezo wa kupambana na Chama Cha Mapinduzi (CCM); ina uwezo mkubwa wa kushinda CCM katika uchaguzi uliohuru na wa haki; na kuweza kuleta mabadiliko ambayo wamelilia kwa miongo minne.

Mafanikio yametokana na umoja miongoni mwa viongozi wa Chadema – katika ngazi zote za chama – kuanzia matawi hadi vyombo vyake vya uongozi kitaifa. Mchango wa Zitto umo humo.

Ni muhimu kueleza hapa kuwa mafanikio yamechangiwa, kwa kiasi kikubwa pia, na umoja na ushirikiano wa mwenyekiti Freeman Mbowe na katibu mkuu, Dk. Willibrod Slaa.

Zitto na genge lake walifanya juhudi kubwa kuwatenganisha Mbowe na Dk. Slaa. Ni akina nani walikuwa wanawatuma, lini na wapi; kila kitu kimerekodiwa. Usichezee rekodi!

Bali kwa ufasaha zaidi, mtu angeweza kusema kuwa Chadema imepoteza zaidi kuliko kujijenga, pale ilipokuwa na Zitto. Kama Zitto angekuwa nje ya Chadema mapema zaidi, chama hicho kingekuwa mbali zaidi kuliko kilipo sasa.

Hii ni kwa sababu, Zitto ametumia Chadema kujinufaisha binafsi kuliko kuitumikia. Amejineemesha kuliko kuneemesha chama. Amekiumiza kuliko kukilinda. Amekidhoofisha kuliko kukijenga.

Mathalani, katikati ya kampeni za urais, wabunge na madiwani mwaka 2010, Zitto badala ya kusaidia chama chake kushinda uchaguzi, aliingiza ubinafsi.

Akiwa jimboni kwake Kigoma Kaskazini, aliacha kampeni zilizoko mbele yake na kutangaza kugombea urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 kupitia Chadema. Akagawa wapigakura wake.

Wakati Zitto anatangaza atajitosa katika kinyang’anyiro cha urais mwaka 2015, alijua kuwa bado hataweza kutimiza masharti ya katiba ya kuwa mgombea. Bado “kichanga” kwa urais.

Wachunguzi wa mambo walitafakari hilo na kusema, Zitto alitoa kauli hiyo ili “kuaminisha wananchi kuwa mgombea wa chama chake – Dk. Slaa – hataweza kushinda uchaguzi huo.”

Zitto alikuwa kazini. Bila shaka hiyo haikuwa kazi ya Chadema. Alikuwa anatekeleza kazi ya aliyomtumwa; kazi ya kutibua kampeni za Chadema.

Si hivyo tu. Zitto alitumia madaraka yake ya naibu katibu mkuu, kuwaengua baadhi ya wagombea ubunge wa chama chake ili kunufaisha “maswahiba wake.”

Miongoni mwa walioeng’uliwa kwa maelekezo ya Zitto, ni pamoja na aliyekuwa mgombea ubunge wa Chadema, katika jimbo la Mpanda Mashariki, linaloshikiliwa na Mizengo Pinda – waziri mkuu.

Barua ya Zitto iliyotumwa kwa mkurugenzi wa halmashauri ya Mpanda ilisisitiza kuwa Chadema haikuwa imeweka mgombea katika jimbo hilo. Pinda akapita bila kupigwa. Bila shaka Zitto alilipwa ujira wake.

Wengine walionufaika na “mradi wa Zitto,” ni Nimrod Mkono; huku Mohammed Dewji na Lawrance Masha, wakiambulia patupu baada ya wagombea walioenguliwa kwa maelekezo ya Zitto kurejeshwa na Tume ya uchaguzi (NEC).

Hata yule anayejiapiza kuwa yuko tayari “kufa na Zitto na kuzikwa naye kaburi moja” – Msafiri Mtemelwa – amenukuliwa akilalamikia usaliti wa “mzishi wake.”

Amesema, katika kipindi chote cha kampeni, Zitto hakwenda jimboni kwake Urambo Mashariki kumnadi, kutokana na kile kinachoitwa, “undugu wa damu” kati yake na Samwel Sitta.”

Mara baada ya kumalizika uchaguzi mkuu wa 2010, haraka Zitto akatangaza kugombea nafasi ya kiongozi wa upinzani bungeni.

Zitto anajua kanuni zinazoongoza mabunge ya Jumuiya ya Madola. Kwa mujibu wa kanuni hizo, chama kinachounda kambi ya upinzani, iwapo kiongozi wake mkuu akiwa mbunge, ndiye moja kwa moja huwa kiongozi wa kambi ya upinzani.

Zitto anajua kuwa Mbowe ameshinda na kutangazwa kuwa mbunge wa Hai, mkoani Kilimanjaro. Hakuwahi kutangaza kuwa hatashika madaraka hayo; wala chama chake hakikuwa kimetangazia wabunge wake kugombea nafasi hiyo.

Aidha, katikati ya kutafuta mbunge wa Arumeru Mashariki, huku chama tawala kikiwa kimekabwa koo, Zitto aliibuka tena na kutangaza kuwa atajitosa katika kinyang’anyiro cha urais mwaka 2015.

Alilenga kudhoofisha Chadema ili kishindwe katika uchaguzi huo. Alitaka kutumia kushindwa Arumeru kumsaidie “kuteka chama.”

Hivyo ndivyo unavyoeleza waraka wa Zitto na wenzake – akina Dk. Mkumbo Kitika – uliopewa jina la “mkakati wa mabadiliko” – wakilenga kuondoa uongozi halali wa Chadema.

Pili, siyo kweli kuwa Zitto Zuberi Kabwe alifanya juhudi kumaliza mgogoro kati yake na wenzake ndani ya Chadema. Huu ni uongo mkavu.

Kuna ushahidi usio na shaka wa jinsi Zitto alivyokuwa kikwazo cha kutafuta maridhiano. Kuna orodha ndefu ya watu wanaoheshimika ndani na nje ya Chadema, waliotaka “kumrejesha Zitto kundini.” Alishindikana.

Hata hivyo, Zitto alipaswa kufungua njia kwanza. Haitoshi kukiri kujua mpango wa kuondoa uongozi halali wa chama. Alipaswa kuwa muwazi zaidi na hata kuapa kuwa hatarudia kushiriki njama; na wakati huohuo kutaja wote waliokuwa katika genge lake.

Wala Zitto hakuwahi kupenda Chadema kama ambavyo amekuwa akitaka kuaminisha wengi. Hakuwahi kuitetea na hajawahi kuwa miongoni mwa walioumizwa kwa ajili ya chama hicho. Alikuwa Chadema kulinda maslahi yake binafsi.

Ni hapa basi alipoona kile anachokitaka hawezi kukipata; akaamua kukibomoa. Bila shaka ndivyo itakavyokuwa pia katika chama alichokimbilia – Alliance for Change and Transparency (ACT-Tanzania).

Tatu, Zitto hana lolote la kujivunia katika sakata zima la kushughulikia ukwapuaji wa mabilioni ya shilingi katika akaunti ya Tegeta Escrow. Kama kipo, basi akiri kuwa ni naye alipata “mgawo.”

Kamati ya PAC haikufanya kazi ambayo Zitto anaitumia kujivika “utukufu.” Kazi ya kamati hii, ilikuwa ni kusoma ripoti ya Mdibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG); kuchambua vielelezo, kuandika mapendekezo na baadaye kuwasilisha mapendekezo hayo bungeni. Basi! Hiyo ndiyo ilikuwa kazi yake na wenzake.

Lakini hata hayo mapendekezo yaliyoandikwa na kamati ya Zitto, karibu yote yalizikwa bungeni. Aliyekuwa naibu waziri wa sheria na katiba, Angellah Kairuki, alipangua hoja moja baada ya nyingine zilizowasilishwa na kamati ya PAC.

Kairuki, akitumia kanuni ya 57 ya Kanuni za Bunge, Toleo la mwaka 2013, aliwasilisha mapendekezo ya kufuta baadhi ya maneno; kuandika upya na kuongeza maneno mengine ambayo yanapendeza watawala.

Waziri alipomaliza kuwasilisha, alikuwa tayari amefuta maazimio yote ya Kamati ya Zitto – Azimio Na. 1 hadi Azimio Na. 6.

Wachunguzi wa siasa wanahoji: Kwanini Zitto na kamati yake walipeleka mapendekezo nyororo na dhaifu kiasi cha kupondwa; na yote kufutwa kwa hoja za “waziri mdogo?”

Zitto alikuwa na fursa ya kutafuta ushauri kutoka kwa wabunge wenzake na hasa katika UKAWA. Hakufanya hivyo.

Ni kutokana na hali hiyo, mapendekezo ya PAC yalionekana kama “makubaliano kati ya Zitto na anaowatumikia.” Atahitaji muda zaidi kujibu mbele ya umma.

Siyo siri kwamba maazimio yaliyokuja kusomwa baadaye na Zitto, yaliandaliwa na Tundu Lissu, mwanasheria wa UKAWA. Na hii ni baada ya wabunge wa upinzani kuchachamaa bungeni. Rekodi zipo na ziko wazi.

Hata wakati wa kuwasilisha mapendekezo mapya, bado Andrew Chenge – mmoja wa watuhumiwa wa Escrow – alipewa fursa ya kupendekeza “mfumo wa kuandika Maazimio ya Bunge;” akilenga kuepusha tuhuma nzito zilizoibuliwa na CAG.

Katika hali isiyo ya kawaida; na ilikuwa karibu na usiku wa manane; Zitto Kabwe, mbele ya Bunge na kwa sauti ya unyonge na kunyenyekea, aliridhia mapendekezo ya Chenge.

Mapendekezo ya Chenge yalitaka Bunge lisiagize Rais Jakaya Kikwete kuwachukulia hatua watuhumiwa. Alitaka rais ashauriwe. Akadai kuwa hiyo ndiyo kazi ya Bunge – kutoa ushauri.

Spika Makinda alipouliza iwapo maazimio yote yachukue mkondo huo wa “kushauri,” Zitto alijibu kuwa anaafiki mfumo wa mapendekezo aliotoa Chenge na kutamka kuwa yeye sasa alikuwa amechoka ubongo!

Zitto alinukuliwa akisema, “…nakubaliana na mapendekezo ya Chenge na naomba mapendekezo yote yafuate mkondo huo.” Huu ulikuwa mkondo au makusudi ya kukamilisha alichonuia? Watanzania bado wanaendelea kudai majibu.

Kama siyo Freeman Mbowe, kiongozi wa upinzani bungeni, kusimama na kuchachamaa kuwa Chadema haiwezi kuwa sehemu ya “uchafu huo” –hata hatua ya sasa katika kukabili wanufaika wa fedha za Tegeta Escrow, isingekuwa imefikiwa.

Ni kauli ya Mbowe na wabunge wenzake wa UKAWA na baadhi ya wabunge kutoka CCM iliyookoa jahazi. Spika Anne Makinda aliridhika na kusimamisha Bunge karibu na usiku wa manane.

Alicholenga Zitto na baadhi ya wenzake katika CCM; ambacho ni kutaka mapendekezo ya kamati yake yasikilizwe na kupitishwa kwa kura ya wengi; kilizolewa na kimbunga cha hotuba ya Mbowe.

Huu ulikuwa ushindi wa wanamageuzi na wapenda maendeleo ndani ya CCM. Uko wapi ujasiri na majigambo ya Zitto. Hitoria itasema mengi. Historia haiheshimu waongo na wanaojikweza. Huwaumbua.

error: Content is protected !!