Friday , 29 September 2023
Home Gazeti Habari za Siasa Zitto Kabwe amuumbua Jaji Mutungi   
Habari za SiasaTangulizi

Zitto Kabwe amuumbua Jaji Mutungi   

Spread the love

ZITTO Zuberi Kabwe Ruyangwa, “ameivua nguo,” ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini. Ameionyesha kutokuwa makini katika kushughulikia masuala yanayohusu ofisi yake; na au kutumiwa na baadhi ya vyama, kutaka kuangamiza vyama vingine. Anaripoti Kelvin Mwaipungu … (endelea).

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Zitto amesema, taarifa ya msajili kutaka kukifuta Chama cha ACT-Wazalendo, imesheheni tuhuma za kupika na zenye nia ovu.

Amesema, “tumepokea barua kutoka ofisi ya msajili, ambayo kiongozi wake mkuu, ni Jaji wa Mahakama Kuu. Lakini ukisoma maudhui yaliyomo kwenye barua hiyo na kinachoendelea nyuma ya pazia, unashangaa kama kweli ofisi ile inaongozwa na mtu mwenye hadhi ya ujaji.”

Zitto anasema, barua iliyoka ofisini kwa Jaji Mutungi inaituhumu ACT- Wazalendo, kukiuka sheria ya vyama vya siasa kwa kutopeleka kwake, hesabu zilizokaguliwa kwa mwaka wa fedha 2013/2014.

Lakini Zitto anasema, rekedi zilizopo kwenye ofisi ya msajili zinaonyesha kuwa ACT Wazalendo kilianzishwa na kupewa usajili wa kudumu tarehe 5 Mei 2014 na kwa hivyo, kwa mwaka huo wa fedha (2013/14) chama hicho kilikuwa na miezi miwili tu ya kukaguliwa.

“Kazi yetu kama chama cha siasa ni kuwasilisha ripoti kwa ajili ya kukaguliwa na CAG. Ripoti ya hesabu za 2013/14 imewasilishwa kwa CAG kwa barua. Kwa kutumia Kanuni za Kimataifa za Kihasibu na kwa ushauri wa CAG, chama chetu kilielezwa kinaweza kuunganisha hesabu za mwaka 2013/2014 na 2014/2015 katika ripoti moja,” anafafanua Zitto.

Anasema, “CAG amewieleza kwa barua kuwa hilo ni jambo la kawaida kabisa katika kanuni za uhasibu. Unaruhusiwa kuunganisha hadi hesabu za miezi 18, na kwamba kwa kuunganisha huku hesabu, ACT ilikuwa na miezi 14 tu.”

Katika barua yake kwenda ACT – Wazalendo ya tarehe 25 Machi 2019, pamoja na mengine, msajili anaeleza kuwa “kusudio la serikali, ni kutaka kukifuta Chama cha ACT Wazalendo.” Barua ya Msajili kwenda ACT-  Wazalendo, imebeba Kumb. Na. HA. 322/362/20/98.

Zitto ambaye pia ni mbunge wa Kigoma Mjini anasema, “kabla ya kuchukua uamuzi wa kukubali ushauri huu wa kuunganisha hesabu kutoka ofisi ya CAG, Chama chetu kilimwandikia Msajili (kwa barua mbili zenye kumbukumbu Namba AC/HQ/MSJ/2015/006 na AC/HQ/MSJ/2015/008 za tarehe za tarehe 22 na 29 Januari 2015) naye akajibu na kuridhia hesabu za miezi miwili ya mwaka 2013/2014 kuunganishwa kwenye mwaka wa fedha 2014/2015 (kwa barua yenye kumbukumbu Na. KA/ 322/20/60 ya tarehe 16 Februari 2015).

“Taarifa zote hizi ziko wazi kwa kwake mwenyewe Msajili na kwenye Ofisi ya CAG, kuanzia barua za kutaarifiwa juu ya kukusanywa kwa pamoja kwa taarifa ya ukaguzi wa Mahesabu kwa miezi 14 ya mwanzoni (miezi miwili ya mwaka 2013/14 na miezi 12 ya mwaka 2014/15), mpaka ripoti husika ya ukaguzi kutoka kwa CAG.”

Hata hivyo, Zitto anasema, ACT Wazalendo inajua kuwa ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa haina utaalam wa masuala ya ukaguzi wa fedha na matumizi ya vyama. Anasema, anajua kuwa upo uwezekano kwa ofisi ya msajili imeshindwa kuisoma, kuichambua na kuielewa ripoti hiyo kwa mwaka wa fedha wa 2014/15, hatuwalaumu kwa jambo hilo. Ndio maana kisheria kazi hiyo ya ukaguzi amepewa CAG.

Lakini Zitto anasema, “kama msajili angekuwa na nia njema, angeweza tu kuomba ufafanuzi au uchambuzi wa taarifa husika kutoka kwa CAG au hata kwa ACT Wazalendo, Chama chenye uzoefu wa kuchambua hizo ripoti za CAG, na angepewa taarifa husika.”

Anaongeza, “taharuki hii aliyoisababisha haikuwa na sababu yeyote, ni suala la uelewa tu. Tunawaahidi wanachama wetu kuwa sisi viongozi wao tutajibu barua hii ya msajili kwa kumuelewesha. Zaidi tunaishauri ofisi ya Msajili kuwa ni vyema basi, wakishindwa kuzielewa taarifa tunazowapelekea warudi kwanza kwa CAG ama kwetu kuomba ufafanuzi na uchambuzi kabla ya kuandika hizi barua za kutishia kutufuta.”

Msajili anataja sababu nyingine ya kutaka kuifuta ACT, ni kile alichoita, “vitendo vya kuchomwa moto hadharani bendera na kadi za Chama cha Wananchi (CUF) na matumizi ya neno takbira kama yalivyoonekana katika baadhi ya video zilizosambaa katika mitandao ya kijamii.”

Akijibu tuhuma hiyo, Zitto anasema, “barua yenyewe ya Msajili iliyotufikia inasema kwamba imeona picha zinazoonyesha “wanaodaiwa” kuwa wanachama wa ACT Wazalendo wakichoma bendera na kadi za chama cha CUF. Katika hili, Msajili mwenyewe anaonyesha kwamba hana uhakika kama kweli wahusika ni wanachama wa ACT.

“Si ilibidi Msajili ajiridhishe kwanza kuwa wale ni wanachama wa ACT Wazalendo? Kama hajaridhisha anawezaje kutangaza NIA ya kutaka kufuta Usajili wa Chama chetu kwa jambo hilo,” anahoji.

Anasema, “Watanzania waone Ofisi ya Msajili ilivyo na NIA Mbaya na Chama chetu, Watanzania waone namna Ofisi ya Msajili, inayoongozwa na Jaji inavyotoa tuhuma pamoja na kutoa hukumu bila hata ya kuwa na ushahidi.”

Anasema, “chama chetu HAKIHUSIKI kabisa na uchomaji wa bendera wala kadi za Chama chochote. Kihistoria sisi ni Chama cha Masuala, tunaojikita juu ya Utetezi wa Wakulima wa Korosho, Mahindi, Giligilani, Karafuu, Mkonge na Mbaazi wanaokosa masoko ya bidhaa zao. Sisi tumezoeleka kuwa ni wapaza Sauti za Wafuagaji wanaotaifishiwa Mifugo yao na Wavuvi wanaonyang’anywa nyavu zao.

“ACT Wazalendo tunatambulika kwa Uchambuzi wa Bajeti na kupinga Sera za mbaya za kuongoza Uchumi zinazowafanya wananchi waishi maisha magumu. Matumaini ya wananchi kwetu ni kwa sababu wamezoea kutuona tukichambua ripoti za CAG na kuhoji kutokuonekana kwa TZS 1.5 Trilioni na kusimamia uwajibikaji wa Serikali. Chama chetu utambulisho wake ni utetezi wa wanyonge wanaoonewa popote pale duniani, iwe ni Sahara Magharibi, Palestine au MKIRU (Mkuranga, Kibiti na Rufiji). Rekodi zetu zinatutambulisha hivyo.

“Tumesikitika sana Ofisi ya Msajili hata kuwaza tu kuwa Chama cha Masuala cha namna hiyo kinaweza kuhusika na mambo ya Uchomaji wa bendera na kadi za vyama vingine. Tumesikitika sana.”

Akizungumzia juu ya tuhuma za “Takbir,” Zitto anasema, Msajili anaeleza pia kwamba chama chetu kimevunja sheria ya vyama vya siasa kwa sababu “wanaodaiwa kuwa wanachama wetu” wametumia maneno takbira kwenye shughuli za kichama na kwamba maneno hayo yana udini.

Majibu ya hili ni kama kwenye suala la kudaiwa kuchoma kadi na bendera. Msajili hajaainisha hao wanaodaiwa kuwa ni wanachama wetu wana kadi namba ngapi za uanachama na ni kutoka tawi gani la chama chetu.

Anasema, “ACT Wazalendo ni chama cha siasa cha watu wa matabaka na dini zote na hata wale wasio na dini. Katika Katiba yetu ya chama tumeonyesha wazi kwamba hatufungamani na dini yoyote na ndiyo sababu tumeruhusiwa kufanya shughuli za kisiasa.

“Tuna ushari tu kwa Ofisi ya Msajili, katika nchi ambayo viongozi karibu wote wa Serikali wanaanza hotuba zao kwa salamu za kidini za “Bwana Yesu Asifiwe, Tumsifu Yesu Kristo na Assalaam Aleykum” ni rahisi kwa “wanaodaiwa kuwa wanachama wa ACT Wazalendo” kutumia kaulimbiu za dini zao kama wanavyofanya viongozi wa Serikali.”

Zitto anasema, kwa maoni yake, barua ya msajili haina nia njema kwa chama chake na wapenda demokrasia wote nchini. Anasema, kukosekana kwa nia njema kulionekana mapema kabisa baada ya barua iliyotakiwa kutumwa kwetu kusambazwa kwanza katika mitandao ya kijamii kabla hata haijatufikia.

“Taswira tunayopata ni kwamba ilivujishwa makusudi na ofisi ya msajili kutimiza dhamira ovu waliyonayo dhidi yetu,” anaeleza.

Anasema, “serikali na Chama cha CCM vimepata mchecheto na ufuasi mkubwa wa chama chetu, hasa baada ya Maalim Seif Sharif Hamad na waliokuwa viongozi wenzake kutoka chama cha CUF kuhamia ACT Wazalendo. Wameogopa zaidi kuwa sasa ACT Wazalendo ndio kimbilio la Wazanzibari wote waliomchagua Maalim Seif kuwa Rais wao kwenye uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, 2015.”

Anasema, ushauri wetu kwa CCM na Serikali yake, “hata wasiwaze tu kuifuta ACT Wazalendo, hatua mbaya ya namna hiyo ya kionevu itawanyima fursa karibu theluthi moja ya Watanzania ya kufanya siasa kwa njia halali za kisheria.

“Watu hawa wakinyimwa fursa hii kionevu kupitia ACT Wazalendo watatumia njia nyengine zinazoweza hata kuleta mpasuko kwa Taifa letu. Ikifika hatua hiyo, sisi Viongozi wa ACT Wazalendo hatutakuwa na sauti ya kuwakataza watu hawa watakaodhulumiwa fursa ya kufanya siasa kwa njia halali za kisheria.

“Tunachukua nafasi hii pia kuzitaka Taasisi za Dini, Asasi za Kiraia, Nchi marafiki na wahisani kupaza sauti juu ya jambo hili. Wasikae kimya wanapoona uonevu unataka kufanyika.”

Zitto anasema, yeye na wenzake ndani ya ACT- Wazalendo, “barua ya Msajili haijatutisha wala kuwatikisa. Na tutaazima busara za mwanachama wetu mwandamizi, Maalim Seif, kuwa TUSICHOKOZEKE. Na hatutachokozeka.”

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Kapinga: Usambazaji umeme vijijini mwisho Desemba 2023

Spread the love  NAIBU Waziri wa Nishati, Judith Kapinga, amesema ifikapo mwezi...

Habari za Siasa

Mgongano wa kimasilahi wamhamisha Chande TTCL

Spread the love  ALIYEKUWA Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO),...

Habari za SiasaTangulizi

Mgawo wa umeme: Rais Samia ampa miezi sita bosi mpya TANESCO

Spread the love  RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, amempa miezi sita Mkurugenzi...

Habari za Siasa

Rais Samia avunja bodi ya REA

Spread the loveRAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, amemteua Balozi Jacob Kingu, kuwa...

error: Content is protected !!