January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Zitto Kabwe ajipalia makaa ACT

Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (kulia) akiwa na David Kafulila (katikati) Mbunge wa Kigoma Kusini na Deo Filikunjombe mbunge wa Ludewa.

Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (kulia) akiwa na David Kafulila (katikati) Mbunge wa Kigoma Kusini na Deo Filikunjombe mbunge wa Ludewa.

Spread the love

ZITTO Kabwe – kiongozi wa Chama cha ACT – Wazalendo, ameonywa kwamba hana uwezo wa kuamua nani awe mbunge majimbo ya Kigoma kama anavyojitapa kwenye vyombo vya habari. Anaandika Pendo Omary …. (endelea).

“Wabunge wengi wa Kigoma walishinda kwa uwezo na akili zao. Kama Zitto Kabwe alishidwa kuipatia Chadema majimbo hayo kwenye uchaguzi wa mwaka 2010 na kuishia kupata jimbo moja lake, ataweza sasa hivi?

Kauli hiyo inakuja baada ya gazeti la Mwananchi kumnukuu Kabwe akisema “Nahitaji majimbo yote ya Kigoma kuchukuliwa na ACT bila kukosa hata moja na hili hata Serukamba (Mbunge wa Kigoma Mjini – CCM anajua). Mwanasiasa anayetaka kuwa mbunge Kigoma lazima aje ACT”.

Akizungumza na MwanaHALISI Online, David Kafulila – Mbunge wa Jimbo la Kigoma Kusini amesema, “Kigoma ni ngome ya NCCR – Mageuzi. Chama hichi ndicho chenye majimbo mengi kigoma”.

Kuhusu madai ya Kabwe kwamba baadhi ya wabunge wamekuwa wakiichangia ACT na ndio maana inaweza kujiendesha, Kafulila amesema, “Kama chama cha Zitto ni cha uwazi,  awataje kwa majina hao wanaomchangia. Maana anaweza kuchangiwa hata na wauza madawa ya kulevya kisha akasema ni wabunge”.

Naye Felix Mkosamali – Mbunge wa Jimbo la Muhambwe (NCCR-Mageuzi), ambaye jimbo lake lipo kwenye orodha ya majimbo yanayotakiwa kinguvu na Kabwe, ameiambia MwanaHALISI Online “Tulishafunga mjadala kuhusu ACT”.

“Tuliitisha press conference (mkutano na waandishi wa habari) na kukana taarifa zinazotolewa na ACT kila siku kwenye magazeti,” amesema Mkosamali.

Wabunge wengine Peter Serukamba (Kigoma Mjini), Albert Obama (Manyovu) na Christopher Chiza (Buyungu) wote CCM na Moses Machali (Kasulu Mjini) na Agripina Buyogela (Kasulu Vijijini) NCCR-Mageuzi hawakupatikana kuzungumzia tambo hizo za Zitto.

Hata hivyo, kiongozi mmoja mwandamizi wa NCCR-Mageuzi aliyeomba kuhifadhiwa jina, amesema kauli hiyo ya Zitto imehalalisha kwamba amebakia kufanya siasa kwenye vyombo vya habari.

“Hivi huyo kama alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chadema kwa miaka 10, ameshindwa kukisaidia chama kipate mbunge walau mbunge mwingine Kigoma. Isitoshe hata jimboni kwake alishinda kwa taabu, leo ACT anayoizungumza na kutambia ni ipi?

“Huyu ndio maana kakimbia jimbo lake, sasa anatangatanga kubabaisha watanzania akidhani bado hawajui undumilakuwili wake. Alifanya siasa magazetini miaka 10 akasahahu jimbo, leo anawaonea wenzake gere,”amesema.

Kwa mujibu wa kigogo huyo, kauli ya Zitto ni ya kuwachonganisha wabunge wa Kigoma na wapigakura wao.

“Huyu ni mpinzani gani kama si kibaraka wa CCM? Chadema wamemtimua kwa usaliti, watu wasiomjua wakawa wanamtetea kwa kudhani kaonewa lakini sasa ameanza kujidhihirisha,” amesema.

error: Content is protected !!