Friday , 19 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Zitto Kabwe aishika tena pabaya Serikali ya JPM
Habari za SiasaTangulizi

Zitto Kabwe aishika tena pabaya Serikali ya JPM

Spread the love

MBUNGE wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe ameishika vibaya Serikari ya Rais John Magufuli kwa kuichambua bajeti ya Wizara ya Kilimo ambayo imeonyesha imekuwa dhaifu kila mwaka tangu kuingia madarakani Serikali ya Awamu ya Tano. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea). 

Uchambuzi kamili wa Zitto kuhusu bajeti ya Kilimo huu hapa chini

Bajeti ya Kilimo 2018/2019: Serikali ya CCM haina dhamira ya kuendeleza kilimo na haina Mpango na Wakulima 

– Turejee Azimio la Iringa la SIASA NI KILIMO na kuwekeza 5% ya Pato la Taifa ( GDP ) kwenye Kilimo kwa miaka 5 mfululizo

Zitto Kabwe, Mb

Utangulizi

Wabunge wanajadili makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Sekta ambayo imeborongwa zaidi kuliko Sekta zote za uchumi wa nchi yetu. Tangu Serikali ya awamu ya tano iingie madarakani, Wakulima wa Tanzania wameumia zaidi kuliko tabaka lingine lolote la Wananchi.

Bei za mazao ya Wakulima zimeshuka sana ( maharagwe, mahindi, mbaazi, choroko, dengu, giligilani nk), ilhali bei za vifaa vya viwandani zimepanda Sana ( simenti, mabati, nondo, Sukari, mafuta ya kula nk ) na mbolea kutofika kwa wakati na bei yake kuwa kubwa pale inapopatikana.

Sasa Serikali inapigia debe mbegu za GMO ili Wakulima wetu wawe waendeshwe na makampuni ya Mbegu ya Kimataifa. Ubeberu wa Mbegu ni tishio la Uhuru wa nchi yetu.

Takwimu zifuatazo zinathibitisha namna CCM imeamua kupishana njia na Wakulima ambao ndio wengi nchini na ndio tabaka masikini zaidi.

  1. Umuhimu wa Sekta ya Kilimo 

– Sekta ya kilimo inaajiri  67% ya  nguvu kazi ya Watanzania

– Sekta ya Kilimo inachangia 30% ya Pato la Taifa (GDP),

– Sekta ya Kilimo inaingiza $1.2bn ya fedha za Kigeni kupitia bidhaa zinazouzwa nchi za nje

– Sekta ya Kilimo inalisha 65% ya malighafi za sekta  ya viwanda,

– Sekta ya Kilimo inachangia zaidi ya asilimia 100 ya chakula kinachopatikana nchini kwenye kipindi chenye mvua za kutosha.

( takwimu hizi zinatoka Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa FYDP II na Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa 2017 )

  1. Uhalisia wa Sekta ya Kilimo 

– Lengo lililowekwa katika  MKUKUTA  ilikuwa  Sekta ya Kilimo ikue kwa 6%- 8% kwa mwaka  kwa miaka 10 mfululizo ili Watanzania wa vijijini waondokane na Umasikini.

– Hali halisi ni kuwa Kati ya mwaka 2011-2015 kasi ya ukuaji wa Sekta ya Kilimo ilikuwa ni wastani wa 3.4% kwa mwaka

– Mwaka 2016 na 2017 ( miaka 2 ya mwanzo ya Serikali ya CCM ya Awamu ya 5, ukuaji wa Sekta ya Kilimo ulikuwa 1.9% mwaka 2016 na 1.3% mwaka 2017 – kasi ndogo zaidi ya ukuaji kupata kutokea tangu mwaka 1961

– Uzalishaji wa mazao yote makuu ya Biashara isipokuwa Korosho umeshuka Katika miaka ya 2016 na 2017. Kahawa uzalishaji umeshuka kutoka Tani 60,000 mwaka 2015 mpaka Tani 48,000 mwaka 2017. Pamba imeshuka kutoka Tani 50,000 mpaka Tani 40,000. Chai imeshuka kutoka Tani 33,000 mpaka Tani 27,000. Tumbaku imeshuka kutoka Tani 87,000 mpaka Tani 61,000. Katani imeshuka kutoka Tani 41,000 mpaka Tani 36,000.

– Hata mazao ya chakula, wakati mahindi uzalishaji umeongezeka kutoka Tani 6.1 milioni mwaka 2016 mpaka Tani 6.6 milioni mwaka 2017, bei ya Wakulima imeporomoka sana kufuatia Serikali kuzuia mahindi kuuzwa nje na Serikali yenyewe kutonunua kabisa kwa ajili ya Ghala la Taifa. Wakati Mwezi Machi mwaka 2015 Ghala la Taifa lilikuwa na Mahindi Tani  452,000, mwezi kama huo mwaka 2018 kuna tani 86,000 tu. Hii ni kwa sababu NFRA haikupewa fedha za kununua mahindi na hivyo Serikali kuwafukarisha Wakulima na Wafanyabiashara wa mazao ya Wakulima.

– Zao lingine ambalo uzalishaji wake uliongezeka ni Mbaazi ambapo Wakulima walizalisha tani 2.3 milioni za mbaazi mwaka 2017 kutoka tani 1.9 milioni mwaka 2016. Licha ya uzalishaji huu Serikali ilishindwa kulinda soko la Mbaazi ya wakulima na hivyo Mbaazi kubakia inaoza shambani.

– Mchele uzalishaji wake ulishuka kutoka tani 2.2milioni mwaka 2016 mpaka tani 1.5 milioni mwaka 2017. Uzalishaji wa Mchele umeshuka chini ya kiwango cha mwaka 2015 ambapo tani 1.9 milioni zilizalishwa na Wakulima.

( takwimu hizi zinatoka kwenye Taarifa ya Quarterly Economic Bulletin ya Benki Kuu ya Disemba mwaka 2017 na Monthly Economic Review ya Benki Kuu ya Mwezi April mwaka 2018 )

  1. Bajeti ya Sekta ya Kilimo 

– Mwaka 2016/17 Bajeti ya Maendeleo ya Kilimo ilikuwa TZS 101.5 bilioni. Fedha zilitolewa ni TZS 2.25 bilioni Sawa na 2.2% ya Fedha yote iliyoidhinishwa na Bunge.

– Mwaka 2017/18 Bajeti ya Maendeleo ya Kilimo ilikuwa TZS 150.2 bilioni. Fedha zilizotolewa mpaka Mwezi Mei ( Mwezi mmoja kabla ya Mwaka wa Fedha kwisha) ni TZS 16.5 bilioni Sawa na 11% ya Fedha yote iliyoidhinishwa na Bunge.

– Mwaka 2018/19 Serikali inaomba kuidhinishiwa na Bunge jumla ya kiasi cha TZS 170.27 bilioni kwa Wizara ya Kilimo. Hii ni sawa na 0.52% ya Bajeti ya Taifa (TZS 32.47 trillioni) inayoombwa kwa mwaka wa fedha 2018/2019.

– Kiasi kinachoombwa ni chini ya Fedha zilizoidhinishwa na Bunge kwa mwaka 2017/2018 ambapo ilikuwa ni TZS 221.10 billioni. Punguzo hili ni 23% .

– Tangu Serikali ya Awamu ya 5 iingie madarakani uwiano wa Bajeti ya Kilimo kwa Bajeti Kuu umekua ukishuka kila mwaka. Mwaka 2016/17 Bajeti ya Kilimo ilikuwa 0.93% ya Bajeti ya Taifa, Mwaka 2017/18 ikawa 0.85% na sasa ni 0.52%.

– Bajeti ya mwaka huu kwa Kilimo ni ndogo zaidi kwa uwiano na Bajeti Kuu katika kipindi cha miaka 10. Wastani wa Bajeti ya Kilimo kwa Bajeti Kuu wa miaka kumi (10) iliyopita 2008/2009 – 2017/2018 ni 2%.

( takwimu hizi zinatoka Taarifa ya Utekelezaji wa Bajeti kwenye Kamati ya Bunge inayohusika na Kilimo na Uchambuzi wa ForumCC ).

Hitimisho 

– Kutokana na mtiririko huu wa Fedha za Bajeti ya Kilimo itakuwa miujiza Sekta ya Kilimo kukua kwani hakuna uwekezaji unaofanywa ili kuongeza uzalishaji na tija kwenye kilimo.

– Uwekezaji kwenye kilimo unapaswa kuelekezwa kwenye miundombinu ya Kilimo na mnyororo mzima wa thamani kuanzia usambazaji wa pembejeo ( backward linkages) mpaka masoko na uongezaji wa thamani ( forward linkages ).

– Uwekezaji unaofanywa kwenye miradi kama Reli na Ndege ungeweza kubadilisha kabisa hali ya maisha ya 70% ya Watanzania wanaoishi kwa kutegemea kilimo kwenye uchumi wa vijijini ( rural economy).

Serikali ya CCM ya Awamu ya 5 ni Adui wa Sekta ya Kilimo na Adui wa Watanzania. Hii ni Serikali inayowajali 5% ya watanzania wanaotumia usafiri wa ndege na kuwasokomeza kwenye umasikini Watanzania 70% wanaotegemea Kilimo. Turudi kutafakari Azimio la Iringa la Siasa ni Kilimo ili kuondoa umasikini Tanzania. Siasa ni Kilimo maana yake ni kuweka kipaumbele kwenye uzalishaji wa bidhaa za kilimo na kukuza sekta ya Kilimo kwa viwango vya kuweza kuondoa umasikini nchini kwetu. Siasa ni Kilimo pia maana yake uchumi ni kilimo kwani 67% ya Watanzania wanaishi kwa kutegemea Kilimo.

Tufanye nini? 

Tunapendekeza yafuatayo ili kukuza Sekta ya Kilimo. 

– Ili kujenga uchumi shirikishi, ni muhimu kufanya jitihada za makusudi katika kuhakikisha kwamba kilimo chetu kinaanza kuchangia vya kutosha katika ukuaji wa uchumi. Serikali iweke shabaha ya kufikia kasi ya ukuaji wa sekta ya Kilimo kuwa 8% ili Mwananchi wa kawaida kijijini afaidike na ukuaji wa Uchumi. Shabaha hii iendane na mkakati madhubuti wa Utekelezaji unaoeleweka na kukubalika na Wakulima wenyewe kupitia Vikundi vyao vya Ushirika.

– Serikali ITAMBUE kuwa Kilimo ndio shughuli kiongozi katika kutokomeza umasikini. Shughuli za Kilimo lazima ziendeshwe na wananchi wenyewe kwa kuwawezesha kumiliki ardhi, kuongeza tija na hivyo uzalishaji na kupata Mitaji, kwa Mfano, kwa kupitia mfumo wa Hifadhi ya Jamii. Hivyo Serikali inapaswa kuwekeza kwa kutenga Bajeti inayofikia Azimio la Malabo la kuelekeza 10% ya Bajeti ya Taifa kwenye Kilimo. Tunapaswa pia kuwa na Azimio la Kitaifa la kuwekeza 5% ya Pato la Taifa ( ikiwemo uwekezaji wa Sekta Binafsi) kwenye Kilimo pamoja na uwekezaji kwenye Utafiti na Maendeleo ya Kilimo. Hivyo turudi Iringa, Azimio la Iringa Siasa ni Kilimo na Uchumi ni Kilimo.

– Serikali itunge mfumo wa kodi unaoeleweka na usiotetereka   ( stable fiscal regime ) katika sekta ya kilimo ( fiscal regime for agricultural sector ) na kuhakikisha kuwa mkulima anabakia na sehemu kubwa ya mapato baada ya mauzo ya bidhaa zake

– Serikali iunde Mamlaka ya Kilimo ili kusimamia sekta ya kilimo na kutekeleza mikakati yote ya Maendeleo ya Kilimo. Wajibu wa kuhakikisha mazao ya kilimo ya wananchi yote yamenunuliwa kwa bei nzuri utakuwa wajibu wa Serikali kupitia. Uwekezaji katika Kilimo kupitia Sekta ya Umma au Sekta Binafsi uratibiwe na Mamlaka ya Kilimo.

– Serikali ihusike kikamilifu kwenye hifadhi ya mazao na kuanzisha mfumo wa soko kupitia soko la bidhaa (commodities exchange) ambao utashirikisha vyama vya wakulima na hivyo kufuta kabisa watu wa kati (middlemen).

– Mfumo wa usambazaji wa pembejeo za kilimo urekebishwe ili kutoa nguvu kwa vyama vya msingi vya wakulima kununua pembejeo zao wenyewe kwa wakati.

– Serikali ianzishe Skimu ya Hifadhi ya Jamii kwa Wakulima. Mfumo huo  wa Hifadhi ya Jamii uwekewe utaratibu wa kuwepo kwa fao la Bei ya mazao (price stabilization) na Bima ya Mazao na Mifugo ili kufidia Wakulima bei inapoporomoka chini ya gharama za uzalishaji. Skimu pia ihusike na mikopo ya gharama nafuu kwa vikundi vya wakulima au Vyama vya Msingi vya Ushirika ili kununua pembejeo za kilimo na ufugaji.

Bila Maendeleo ya Kilimo, kasi ya ukuaji wa Uchumi wa nchi itaishia kwenye takwimu tu na sio kwenye maisha ya Wananchi wetu.

Mapinduzi ni Lazima

 

Mwami Ruyagwa ZK

15/5/2018

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

KimataifaTangulizi

Mkuu wa majeshi Kenya afariki, Ruto atangaza maombolezo

Spread the loveRais wa Kenya, William Ruto ametangaza maombezo ya siku tatu...

Habari za Siasa

Tume huru ya uchaguzi yatangaza ajira watendaji daftari wapiga kura

Spread the love  TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), imetangaza nafasi...

Habari za SiasaTangulizi

Chadema yatangaza ruti awamu ya pili maandamano

Spread the love  CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema awamu ya...

Habari za Siasa

CCM yamkana mwenyekiti UVCCM aliyetaka wapinzani wapotezwe

Spread the love  CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimejitenga na kauli ya mwenyekiti...

error: Content is protected !!