November 30, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Zitto Kabwe ‘afukuzwa Bungeni’

Zitto Kabwe, Kiongozi wa ACT-Wazalendo na Mbunge wa Kigoma Mjini

Spread the love

MBUNGE wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Zuberi Kabwe, amefurushwa bungeni. Ni baada ya kuamriwa kutoka nje ya Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria. Anaripoti Mwandishi Wetu kutoka Dodoma … (endelea).

Zitto alikumbwa na mkasa huo, majira ya saa saba mchana, kufuatia mwanasiasa huyo kuzuiwa kuchangia muswada wa sheria ya vyama vya siasa.

Taarifa kutoka ndani ya Kamati ya Katiba na Sheria zinasema, Zitto aliingia katika ukumbi wa mikutano wa Pius Msekwa kunakoendeshwa vikao vya kamati, kutaka kushiriki mjadala huo.

Lakini ghafla aliyekuwa mwenyekiti wa kikao hicho, makamu mwenyekiti wa Kamati ya Katiba na Sheria, Najma Giga, alimzuia mwanasiasa huyo kuchangia kwa madai kuwa siyo mjumbe wa kamati hiyo.

Kufuatia maamuzi hayo, Zitto alimuomba mwenyekiti huyo kumpa ufafanuzi kutoka kwa mwenyekiti wa Kanuni anazotumia kufikia maamuzi hayo.

“Ndipo Giga alipomueleza Zitto kuwa hayo ni maamuzi ya Kamati. Kwamba wabunge ambao siyo wajumbe wasipewe nafasi ya kuzungumza,” ameeleza mtoa taarifa wa MwanaHALISI Online.

Amesema, “mwenyekiti alimueleza Zitto kuwa wabunge ambao siyo wajumbe wa Kamati ya Katiba na Sheria, wataruhusiwa kutoa maoni yao siku ya Jumamosi na Jumapili.”

Mjadala juu ya muswaada wa sheria ya vyama vya siasa, uliopelekwa bungeni Novemba mwaka jana, umeibua malumbano makubwa kati ya baadhi ya wanasiasa wa upinzani, wanaharakati na wananchi wengine wanaojitanabisha kuwa wana mabadiliko kwa upande mmoja na wale wa chama tawala – Chama Cha Mapinduzi (CCM).

error: Content is protected !!