October 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Zitto azidi kuwavuruga CCM, Wabunge wake waazimia kumkabili

Spread the love

WABUNGE wote wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wameazimia kwa pamoja kuhakikisha wanakabiliana na mbunge wa Kigoma Mjini, Zito Kabwe (ACT-Wazalendo) kwa madai kuwa amekuwa kinara wa upotoshaji Umma pamoja na kuwa mstari wa mbele kupinga Mamlaka ya Spika kufanya kazi. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma … (endelea).

Mbali na kujipanga kukabiliana na Zitto pia wamesema kuwa watahakikisha wanajibu hoja za Zitto na wapinzani kwa njia yoyote na kutoruhusu kuendelea kusikilizwa na kusambazwa kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kama ilivyo sasa.

Kamati ya wabunge wa Chama cha Mapinduzi (Caucas) wakizungumza na waandishi wa habari Jijini Dodoma walisema kuwa wabunge wanaotokana na chama hicho wamejipanga kukabiliana na Zitto kutokana na hoja zake anazozitoa ikiwa ni pamoja na kuonesha nia yake ya kukimbilia mahakamani kwa ajili ya kuzuia shughuli za Bunge kuendelea.

Kwa niaba ya kamati hiyo mbunge wa Mbinga, Sixtus Mapunda, alisema kuwa wabunge hao wameshangazwa na hatua za Zitto kufanya juhudi za kuzuia Mamlaka ya Spika kutekelezwa.

Mapunda alisema kuwa katika hali ya kushangaza na iliyokinyume cha sheria Zitto akishirikiana na na baadhi ya wanasheria, walifanya jitihada za kuzuia Mamlaka ya Spika kutekelezwa.

Wakieleza nia ambayo wabunge hao wamekusudia kukabiliana na Zitto kwa namna yoyote ni pamoja na Zitto kufungua kesi katika mahakama kuu kanda ya Dar es Salaam ili kuzuia CAG asihojiwe na Bunge, kesi ambayo ilitupiliwa mbali kwa kukosa vigezo vya kusikilizwa mahakamani.

Jambo lingine ambalo limeonekana kuwa kero kwa wabunge wa CCM ni Mbunge huyo wa Kigoma Mjini kuandika barua kwa Katibu mkuu wa Mabunge ya Jumuiya ya Madola (CPA)  na kutuma nakala kwa maspika wa mabunge yote ya Afrika kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola na Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Janngwa la Sahara(SADC) pamoja na wadhibiti na Wakaguzi Wakuu wa Hesabu za Serikali wa Jumuiya ya Madola.

“Kitendo cha Zitto ambaye ni mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mbali ya kuwa ni kinyume cha Sheria za Nchi na Kanuni za Bunge pia ni kitendo cha kudharau  Mamlaka ya Spika, mbunge huyo anayo nafasi kupitia kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kumshauri Spika katika kamati ya Uongozi kuhusu uendeshaji wa shughuli za Bunge kama inavyoelekeza kanuni ya 2(3) na nyoneza ya nne ya kanunu ya kudumu za Bunge.

“Hatua ya Zitto kukimbilia mahakamani kupinga Mamlaka ya Spika au kuandika barua kwa mabunge ya nchi nyingine kupinga uamuzi wa Spika au kujadili Mamlaka yake kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii ni dharau kubwa kwa Mamlaka ya Spika na Mhimili wa Bunge kwa Ujumla,” alisema Mapunda.

Mapunda alisema kuwa kanuni ya 5(4) na (5) ya kanuni za Bunge imeweka utaratibu ambao mbunge ambaye hakuridhishwa na uamuzi wa Spika anaweza kupinga uamuzi huo na mbunge atawasilisha sababu za kutoridhishwa kwake kwa katibu wa Bunge na malalamiko hayo yatafanyiwa kazi na kamati ya kanuni za Bunge na baadaye Bunge litajulishwa kuhusu uamuzi utakaotolewa.

Mbunge huyo kwa niaba ya wengine alisema kuwa si mara ya kwanza Zitto kufanya upotoshaji kwa Umma na kueleza kuwa hivi karibuni kwa kushirikiana na baadhi ya wanasiasa walipeleka mahakamani kesi Na 31 ya kwaka 2018 kaika mahakama Kanda ya Dar es Salaam, kupinga Mswada wa Marekebisho ya sheria ya vyama vya siasa wa mwaka 2018 kesi ambayo nayo ilitupiliwa mbali kwa kukosa uhalali wa kisheria.

Kuhusu taarifa iliyotolewa na Kambi rasmi Bungeni, Kmati ya Wabunge wa CCM imesema kuwa siyo kweli kuwa Spika amevunja Kamati za kudumu za Bunge ambazo zinaongozwa na Upinzani kwa maana ya LAAC na PAC.

Mapunda alisema kuwa kamati hizo hazijafutwa bali wajumbe wake wamesambazwa katika kamati nyingine hadi hapo wito wa CAG utakapotekeleza kwa mujibu wa mashariti ya kanuni za Bunge.

Katika hali ya kuonesha kuwa wabunge wa CCM wamejipanga kukabiliana na Zitto mbunge wa Mtera, Livingiston Lusinde alisema kuwa kwa sasa Zitto amepoteza mwelekeo na anatakiwa kujitafakari ili arudishe heshima yake ya kisiasa badala ya kupambana na siasa za upotoshaji.

Hata hivyo alisema anamshauri mke wa Marehemu Mchungaji Christopher Mtikila, kumshitaki Zitto kwa madai kuwa amegeuka kuwa mbunge wa kukimbilia mahakamani kazi ambayo alikuwa akiifanya Mchungaji Mtikila.

Naye mbunge wa Viti Maalum kutoka Zanzibar, Taohida Nyimbo, alisema kuwa wabunge wa CCM watahakikisha wanapambana na Zitto kwa gharama yoyote ili kuhakikisha wanajibu hoja zake ambazo amekuwa akizitoa kwenye vyombo vya habari pamoja na mitandao mbalimbali ya kijamii.

Alisema kuwa siyo kweli  kuwa wabunge wa CCM ni makasuku kama anavyoeleza Zitto kwa madai kuwa wapo kwa ajili ya kulinda chama chao na kulinda maslahi ya wakubwa jambo ambalo Nyimbo alisema kuwa siyo sahihi kuendelea kumvumilia Zitto.

Katika hatua nyingine kamati ya wabunge wa Chama cha Mapinduzi (CAUCUS) wamesema kuwa wanampongeza CAG kwa kuitikia wito wa Spika wa Bunge kwa kukubali kufika kwenye kamati ya haki, Kinga na maadili ya Bunge tofauti ilivyokuwa kizungumzwa kuwa spika hana haki ya kumwita CAG kwa ajili ya kuhojiwa.

error: Content is protected !!