January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Zitto apigwa ‘stop’ ACT-Tanzania

Aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe akitangaza rasmi kujiunga na ACT-Tanzania

Spread the love

BAADA ya kutimuliwa Chadema na kukimbilia Chama cha ACT-Tanzania, Zitto ameanza kuwekewa vigingi akitakiwa kutogombea nafasi yoyote ya uongozi wa kitaifa utakaofanyika 28 Machi mwaka huu.

Kigingi hicho, kimewekwa na Mwenyekiti wa ACT aliyesimamishwa uongozi, Kadawi Limbu, alisema Zitto aliyejiunga na chama hicho siku nne zilizopita anapaswa kusubiri mpaka atakapotimiza miezi sita ya uwanachama wake.

Limbu ambaye bado anajitambua kama mwenyekiti halali wa ACT-Tanzania, ametoa tamko hilo wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

 “Mimi bado ndiye mwanyekiti wa ACT- Tanzania kwa vile barua inayodaiwa kuniondoa katika nafasi ya uenyekiti haikuwa halali na ilinifanya nipeleke suala hilo mahakamani kwa ajili ya kupata muongozo,”amesema.

Kwa mujibu wa Limbu, katiba ya chama hicho inaelekeza wazi kwamba mwanachama yeyote anayetaka kugombea nafasi ya uongozi ni lazima uwanachama wake uwe umetimiza zaidi ya miezi sita tangu ajiunge na chama hicho.

“Mkiangalia mtaona Zitto ambaye amejiunga na chama hicho hivi karibuni katika mazingira tata, katiba haimruhusu kugombea nafasi yeyote katika chama chetu, nimuombe kwamba andelee kuwa mwanachama wa kawaida tu,”amesema Limbu.

Pia, amemtaka Katibu Mkuu wa ACT-Tanzania, Samson Mwigamba kuacha kuwapotosha wanachama kuhusu uchaguzi huo kwani sio wa halali kutokana na Limbu kufungua kesi ya kikatiba mahakamani kupinga kuondolewa katika nafasi ya uenyekiti.

Akizungumzia chanzo cha mgogoro huo, Limbu amesema yote hayo yamechangiwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, kutokana ofisi hiyo kufanya kazi kwa utashi huku ikitoa taarifa zinazokanganya.

Limbu amefafanua kuwa ameamua kumpeleka Msajili katika Ofisi za Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kwa madai kuwa amekula njama katika kumpa barua ya kumzuia kuwa mwenyekiti wa chama hicho.

Ametoa angalizo kwamba atapigana hadi kufa kuliko kuona chama hicho walichokianzisha kwa gharama kubwa, kikiangukia mikononi mwa mafisadi.

“Kuna watu wanajiita wazalendo lakini ukiwafuatilia utabaini kuwa wamejivika kofia hiyo kwa ajili ya kunyang’anya haki za wenzao. Watu hao ni sawa na majambazi,”amesema.

Hata hivyo, uongozi wa ACT-Tanzania, umesema katiba yao, iliyoko kwa Msajili wa vyama vya siasa, inaonesha kwamba mwanachama yeyote anaweza kugombea nafasi yoyote ya uongozi endapo ametimiza siku saba tangu ajiunge na chama hicho.

error: Content is protected !!