October 3, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Zitto atibua, Polepole amwita kibaraka

Spread the love

BARUA ya Zitto Kabwe, Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, kwenda Benki ya Dunia (WB), kutaka kuzuiwa msaada wa Dola za Marekani Mil 500, imemchefua Humphrey Polepole, Katibu wa Itikadi na Uenezi (CCM). Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).

Katika barua hiyo, Zitto ameitaka WB kutotoa msaada wa fedha hizo, zilizopangwa kuboresha sekta ya elimu nchini kwa madai, serikali ya Rais John Magufuli, imeshindwa kuheshimu utawala wa sheria na haki za binadamu, ikiwa ni pamoja na kuzuia wanafunzi wa kike wanaopata ujauzito wakiwa shuleni, kuendelea na masomo.

Polepole amesema, watu wa Kigoma Ujiji (Jimbo la Kigoma Mjini analoongoza Zitto) watajisikiaje pale wanaposikia kiongozi wao anaiombea njaa nchini.

“Sijui watu wa Kigoma Ujiji wakisikia ya kwamba huyu bwana ameandika barua Benki ya Dunia, watu wa Kigoma Ujiji, watoto wetu wasiongezewe ubora.

“…sijui watu wa Kigoma Ujiji watajisikiaje, kuwa na muakilishi kama huyu anayeiombea njaa nchi yetu ya Tanzania. Kibaraka mkubwa wa mabeberu,” amesema Polepole.

Hata hivyo, Zitto amemtaka Polepole na wale wanaoungana naye (Polepole), kaucha kulalamika na badala yake wahakikishe serikali irekebishe dosari zilizokuwepo.

Humphrey Polepole, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM

“Mkopo wa Benki ya Dunia utalipwa na kila Mtanzania. Serikali lazima iweke mazingira ya watoto wa kike kupata elimu bila kubaguliwa.

“Watoto waliopata uja uzito shuleni, wawe na fursa kurejea shuleni bila bugudha wala unyanyapaa. Badala ya kulia lia, rekebisheni mkataba wa mkopo,” ameandika Zitto kupitia ukurasa wake wa twitter tarehe 26 Januari 2020 na kuongeza;

“Serikali ambayo inatumia Sh. 1.5 Trilioni kununua ndege kwa cash (fedha taslimu) inalialia wananchi wake wanapohoji mikopo wanayochukua kwa ajili ya elimu kutoka Benki ya Dunia. Fedha za Ndege wanazo lakini za elimu ya watoto wetu wanakwenda kukopa. Heshimuni Demokrasia.”

Kwa mujibu wa mitandao ya kimataifa, Bodi ya Wakurugenzi ya W.B inatarajia kutafakari juu ya maombi hayo, Jumanne ya tarehe 28 Januari mwaka huu.

Mbali na Zitto, wanaharakati na baadhi ya asasi za kira, nazo zimeiandikia barua WB zikiitaka kusitisha kutoa fedha za misaada kwa Tanzania.

Zikituhumu kwamba, serikali iliyoko madarakani, haiheshimu utawala wa sheria na haki za binadamu, pamoja na kuzuia wanafunzi wa kike wanaopata ujauzito wakiwa shuleni, kuendelea na masomo.

error: Content is protected !!