July 26, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Zitto ataja kosa la Chadema kwa Lowassa, Sumaye

Zitto Kabwe, Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo

Spread the love

ZITTO Kabwe, Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo amesema, chama hicho kimechukua tahadhari kubwa ili kisiingie kwenye makosa yaliyofanywa mwaka 2015. Anaandika Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Zitto amezungumza kwenye mahojiano na Sammy Awami, Mwandishi wa Shirika la Habari la Uingereza (BBC), kuhusu mapokeo ya Bernard Membe, matarajio na hofu ya kurejea yaliyotokea baada ya Chadema kumpokea Edward Lowassa na Frederick Sumaye.

Kwenye mahojiano hayo, Zitto alianza kuzungumzia kazi ya kiongozi. Fuatilia neno kwa neno:-

Zitto: Kazi ya kiongozi sio kukimbia risk (hatari), kazi ya kiongozi ni kujua anapita vipi kwenye hizo risk (hatari).

Sisi tumejifunza kwa wenzetu wa Chadema baada ya kumpokea Lowassa, na baada ya Lowassa na Sumaye kuamua kurudi CCM. Tumejifunza na hatutarejea makosa ambayo wenzetu wameyafanya.

Mwandishi: Makosa gani waliyofanya?

Zitto: Watu wanapaswaa au wajibu wa kiuongozi wa kuhakikisha kwamba watu wanajiona ni sehemu ya movement (harakati).

Mwandishi: …ambalo hilo halikufanyika?

Zitto: Naamini na wataniuwia radhi wenzangu, kwamba hatukuona kina Lowassa, Sumaye (Mawaziri Wakuu wastaafu) wakioekana kuwa ni sehemu famili ya Chadema.

Kwa somo kubwa kwetu ni kuhakikisha, kwamba si Membe tu, na wote watakaokuja kwa sababu wengi ambao wanakuja, wanakuwa ni sehemu kamili ya ACT – Wazalendo.

Mfano mzuri angalia, kina Maalim Seif (Maalim Seif Sharif Hamad, mwenyekiti wa chama hicho) wameingia ACT – Wazalendo, ni mwaka tu sasa, unaweza kumtazama Maalim Seif na wenzake ukadhani walikuwa ACT-Wazalendo toka chama kimeanza, si ndio?

Na unaweza ukanitazama mimi na wenzangu tuliokuwa ACT-Wazalendo, ukadhani kwamba tumekuwa na kina Maalim Seif katika miaka yote ya siasa, sio?

Kwa hiyo kuna kazi ya kiuongozi ya kuwafanya watu kujiona ni sehemu ya movement (harakati).

Mwandishi: Umefanya nini kulifikia hilo?

Zitto: Heshima, heshima. Kitu kimoja ambacho mimi nimekuzwa kisiasa sio tu ndani ya siasa, ndani ya familia mama yangu alikuwa mwanasiasa, alikuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Walemavu Taifa mpaka alipopoteza maisha mwaka 2014.

Lakini pili, na hata makuzi yangu ya siasa kwa watu ambao wala sio sehemu ya chama nilichokuwepo kina Mzee Sita (Samuel Sitta, Jaji Joseph Warioba, kina Dk. Salim (Dk. Ahmed Salim) na kadhalika ni heshima.

Hakuna kitu mwanadamu anathamini kama kuheshimiwa utu wake. Na hili ndio naliona ambalo sitaki kusema, sitaki kusema lakini hilo ndio naliona kama strength (kuvu) kubwa ya ACT-Wazalendo.

Kila mtu anajiona ana heshima, mchango katika ukuaji wa chama ndio maana sasa hivi huoni utofauti. Watu walidhani kutakuwa na tension (hofu) kubwa kati ya waliokuwa CUF na ACT-Wazalendo.

Lakini sasa hivi huoni, unaona kila mtu kama alikuwa ACT-Wazalendo tu, au alikuwa CUF akashusha tanga akapandisha tanga, na hiyo ndio silaha yetu kubwa. Ninaamini hiki ndio kimemvutia zaidi Bernard Membe kujiunga nasi.

Mwandishi: Inaonekana chama na wewe umeweka imani kubwa kwa Membe. Mbali na uzoefu wake kuwa Waziri wa Mambo ya Nje kutumikia serikali, masuala ya usalama na vitu kama hivyo. Kuna kitu gani ambacho Membe anacho wewe na chama chako?

Sisi tumeweka imani kwa mtu yeyote anayeingia kwenye chama chetu, tumeweka imani kwa Maalim Seif na wanachama waliokuwa wanachama wa CUF. Na tunaweka imani kwa Membe baada ya kujiungwa kwa sababu ni mwanachama wetu, na ni sehemu ya ACT-Wazalendo.

Na ukiachana na hilo, kuna faida ambazo umezieleza, uzoefu anaouingiza Membe. Chama chetu huyu sio waziri wa kwanza kuwa sehemu ya chama chetu.

Maalim Seif amekuwa waziri kiongozi, amekuwa makamu wa rais, kuna watu wamekuwa wanasheria wakuu katika Serikali ya Zanzibar, mawaziri wa serikali kama kina Mazrui (Nassor Mazrui ) na watu walioshiriki kwenye michakato ya muda mrefu ya kutengeneza maridhiano Zanzibar kama kina Ismail Jussa.

Kwa hiyo, tunaongeza zaidi ujuzi na uzoefu wa namna gani ya kukabiliana na mambo kwenye siasa kwa sababu, siasa ni majadiliano, hukubaliani kila kitu kwenye siasa lakini mnafika katikati ili muweze kwenda.

Jambo muhimu kuliko yote ni kutorejea makosa, makosa yaliyofanywa mwaka 2015 na tuhakikishe tunajenga, sio tu upinzani lakini tujenge mazingira tunayoweza kuunda Serikali Zanzibar na tutaweza kuunda Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania bila changamoto. Hili ndio naliona kubwa zaidi ambalo Membe anaweza kusaidia.

Amekuwa kwenye serikali kwa muda mrefu, amekuwa kwenye vyombo vya ulinzi na usalama kwa muda mrefu. Kama vyombo vya ulinzi na usalama vinaogopa vikidhani kama upinzani ukiingia watafukuzwa kazi na vitavunjwa, sasa mmoja wao ni sehemu ya upinzani.

Ndio wawe assured (uhakika) kwamba sisi tutakachokifanya ni kufanya maboresho, marekebisho, kubadilisha mfumo ili dola iweze kuwatumikia watu badala ya watu kuitumikia dola.

Mwandishi: Kama wenzenu wa upinzani wakikataa kuungana nanyi kusimamisha mgombea mmoja ambaye ni Membe, mtawaelewa?

Zitto: Siamini kama tutashindwa kuweka mgombea mmoja, mimi nina matumaini makubwa sana na Membe, mwenyewe amesema wazi kabisa kuwa ikitokea kuna mtu mwingine wa upinzani ambaye ataweza kuleta ushindi na kuiondoa CCM madarakani, yeye atakuwa tayari kumuunga mkono.

Lakini muhimu sana, tumeingia kwenye huu uchaguzi na vita mbili; Mfumo wetu wa demokrasaia ya vyama vingi upo hatarini, na ni hatari ambayo ipo wazi kabisa.

Tukikaa vibaya, tusiposimama kidete nchi yetu inaweza kurudi kwenye mfumo wa chama kimoja. Tumeona Zanzibar baada ya uchaguzi wa mwaka 2015, kwa muda wote toka 2016 mpaka mwaka huu, lile ni Baraza la Wawakilishi wa chama kimoja.

Tumeona uchaguzi wa Serikali za Mitaa, baada ya asilimia 94 ya wagombea wetu kuenguliwa na sisi kugomea uchaguzi ule, mabaraza yote ya vijiji, serikali zote za vijiji na kamati za mitaa zote zimekuwa ni za Chama Cha Mapinduzi.

Tukikaa vibaya tutaenda kuipa CCM wanachokitafuta ya kuwa na bunge ambalo asilimia 100 ni CCM, na nchi kurudi kwenye mfumo wa chama kimoja.

Kazi ambayo wazee wetu walikuwa wameishaifanya kuirejesha nchi kwenye mfumo wa vyama vingi, kina Prince Bagenda, kina Mbatia (James Mbatia), Anthon Komu, Ismail Jussa kina Maalim Seif hawa.

Wameishafanya kazi ya nchi kuingia kwenye mfumo wa vyama vingi, sasa hapa kuna hatari ya kurudi kwenye mfumo wa chama kimoja.

Kazi ya kwanza tunayoenda kuifanya kwenye uchaguzi wa mwaka huu ni kuzuia nchi kurudi kwenye mfumo wa chama kimoja. Hatuwezi kuifanya hii kazi kama hatuna ushirikiano.

Pili; ni kuwarejeshea furaha Watanzania, kwa kuiondoa serikali ya Chama Cha Mapinduzi ili kuingiza serikali ambayo itaundwa na vyama vya upinzani, ambapo itatekeleza sera zitakazowafanya wananchi wawe na furaha.

Wafanyakazi wapandishwe mishahara kama sheria inavyosema, wakulima wapandishwe bei za mazao yao bila shida yoyote wala kudhani ipo siku jeshi lichukua mazao yao kwa amri ya amiri jeshi mkuu.

Wavuvi wasiogope kuchomewa nyavu zao, wafanyabiashara wawe na uhuru wa kufanya biashara katika nchi yetu, waandishi wa habari waandike habari bila woga, kwamba kesho watatekwa au watapotea.

Hizi kazi mbili haziwezi kufanikiwa kama hatutashirikiana, kwa hiyo ushirikiano sio mjadala tena. Ushirikiano ni jambo la lazima. Mjadala hapa ni nani atapeperusha bendera ya upinzani katika urais wa Jamhuri ya Muungano na Zanzibar. Kwa wabunge wa Bunge la Muungano, wajumbe wa baraza la wawakilishi Zanzibar na madiwani nchi nzima. Huo ndio mjadala.

error: Content is protected !!