January 19, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Zitto anajua makosa yake Chadema

Sehemu ya wanachama wa ACT-Tanzania, chama kipya alichohamia Zitto Kabwe

Spread the love

UPO msemo uliotoholewa kutoka kwenye lugha ya Kiingereza –“Ukishindwa kupigana nao, ungana nao”.

Kwa kutumia maneno mengine mepesi unaweza kusema, jifunze kukubaliana na matokeo. Kwamba asiyekubali kushindwa siyo mshindani.

Inavyoonesha, aliyekuwa mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Zuberi Kabwe ambaye kwa sasa, amejiunga na chama kipya cha ACT, ameshindwa kukubaliana au kuendana na misemo hii.

Alipoamua kujiunga na chama chake kipya cha ACT baada ya kufukuzwa Chadema, taarifa zilizowafikia wananchi, Zitto alifukuzwa uanachama wa chama hicho kutokana na kuvunja kanuni, taratibu, sheria na miongozo ya chama chake.

Zitto anajua makosa yake hayo. Lakini ameendelea kuwahadaa wananchi kuwa amefukuzwa Chadema kwa uonevu. Siyo kweli.

Tuhuma dhidi ya Zitto ziko wazi.

Ametuhumiwa kupanga njama za kukivuruga chama; kuanzisha chama ndani ya chama na amekiri kushirikiana na maadui wa chama na kutaka kufanya mapinduzi ya uongozi ndani ya chama.

Tuhuma zote hizi zimedhihirika pale Zitto aliposhirikiana na “wasaliti wa chama” kuanzisha chama cha ACT.

Kitendo hiki hakina lugha nyingine zaidi ya usaliti, ambao umempambanua na kumwonesha sura yake halisi na rangi zake.

Sababu zilezile ambazo Zitto zimemfanya atoke Chadema, ndizo zitamfanya atoke ACT. Kile anacholalamikia Chadema, ndivyo hivyo hivyo atakavyolalamikia wengine katika ACT.

Kwa mtazamo wangu, Zitto amejimaliza mwenyewe kisiasa kama si “kujikaanga kwa mafuta yake mwenyewe.”

Hii ni kwa sababu, ukilinganisha aina ya ‘nyodo’ za jinsi alivyoaga bungeni na ukisoma kwa makini maneno yake, “…tutaonana bungeni Novemba hii,” ni uthibitisho kuwa kijana huyu anahitaji bado anahitaji ushauri wa kitabibu. Amezidi majivuno.

Ushupavu wa Zitto na maapizo yake yanatokana na kuungwa mkono na Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Jakaya Kikwete. Lakini kama hakujiandaa mapema na kupanga mbinu zake za usaliti, aweza kuishia mtaani.

Mwenye masikio na asikie neno hili, maana huenda ni mpango wa Mungu kuwafunulia wanadamu kwa msaada wa Roho Mtakatifu juu ya usaliti wa baadhi ya viongozi kama hawa.

Mwandishi wa makala hii ni Adam Mwambapa anapatikana kwa namba 0713/0765 937 378/ adammwambapa@ymail.com

error: Content is protected !!