November 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Zitto amweka njia panda Dk. Mwinyi

Spread the love

ZITTO Kabwe, Kiongozi wa Chama cha  ACT-Wazalendo amesema, hadi sasa chama hicho hakijafanya uamuzi kuhusu ushiriki wake katika uundwaji wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar (SUK). Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Ametoa kauli hiyo leo tarehe 23 Novemba 2020, alipoulizwa swali na wanahabari kuhusu msimamo wa ACT-Wazalendo katika ushiriki wa SUK baada ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika tarehe 28 Oktoba 2020 kukamilika.

Akijibu swali hilo, Zitto amesema uamuzi wa mwisho kuhusu suala hilo utatolewa katika vikao vya chama hicho, ikiwemo cha Kamati Kuu ya ACT-Wazalendo ambayo itaketi hivi karibuni.

“Chama tuna demokrasia yetu ya ndani katika kufanya maamuzi ya mwisho.  Kama tulivyosema mwanzo kwa umma chama kitafanya vikao vyake vya ndani kisha tutatoa tamko kama tutashiriki au hatutashiriki. Hilo litategemea maamuzi ya vikao vya chama,” amesema Zitto.

Hivi karibuni wakati anatangaza Baraza la Mawaziri, Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi alisema ameacha nafasi za mawaziri kwa ajili ya ACT-Wazalendo, akieleza kwamba alipeleka barua kwa chama hicho ili kiwasilishe majina ya watu wake.

Dk. Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar

Dk. Mwinyi alisema, anatekeleza takwa la kikatiba baada ya Chama cha ACT – Wazalendo kufikisha asilimia 10 ya kura za rais na kukifanya chama hicho kuwa na sifa ya kujumuishwa kwenye serikali hiyo.

Hata hivyo, Zitto amesema ACT-Wazalendo haitashiriki katika serikali hiyo kwa kuwa, haitambui matokeo ya uchaguzi huo.

“Katiba ya Zanzibar inaeleza uundwaji wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, lakini suala ni kwamba haiwezi kuundwa kwa sababu mchakato wa uchaguzi haukuwa huru na haki. Ni wazi kwamba uchaguzi Zanzibar na Bara haukuwa wa haki na hili lilishasemwa na Maalim Seif (Maalim Seif Shariff Hamad, Mwenyekiti wa Chama cha ACT – Wazalendo),” amesema Zitto.

Maalim Seif Sharrif Hamad, Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo

Akisisitiza amesema, ACT-Wazalendo hakijapeleka majina ya wanachama wake wanaopaswa kuteuliwa katika Baraza la Mawaziri na hata kuruhusu walioshinda uwakilishi kuingia katika Baraza la Wawakilishi Zanzibar, kwa kuwa hawatambui uchaguzi huo.

Lakini Zitto  amesema chama chake hakikufanya makosa kuipokea barua hiyo kwa kuwa kiliwajibika kuipokea kwani iliwasilishwa kwake.

Zitto amesema, kupokelewa kwa barua hiyo haimaanishi kwamba wamekubaliana na matakwa ya Rais Mwinyi ya kjukitaka chama chake kuwasilisha majina.

“Ilishawekwa wazi na mwenyekiti wetu kwa nini tuliipokea barua. Na kwa nini tusingeipokea barua? Bado hatuutambui uchaguzi ndio maana hatukupeleka barua,” amesema Zitto.

error: Content is protected !!