May 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Zitto amtwisha zigo la Mbowe Rais Samia

Spread the love

 

KIONGOZI wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe amemuomba Rais Samia Suluhu Hassan kufuata taratibu zote za kisheria na kumuachia Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo, Freeman Mbowe ili waweze kufanya naye siasa za tija kwa masilahi ya nchi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Zitto ametoa kauli hiyo leo tarehe 15 Disemba, 2021 jijini Dodoma katika kikao cha wadau wa tasnia ya siasa ulioandaliwa na Baraza la Vyama vya Siasa nchini.

Awali akitoa salamu fupi za wadau wa siasa, Zitto amesema mkutano huo ni hatua muhimu kuelekea katika majadiliano ya kiasiasa.

“Na kila jambo lina mwanzo, huu ni mwanzo Mwema ninaamini na Mwenyezi Mungu atatuongoza ili tuweze kuwa na utaratibu huu wa kujadiliana na kutatua changamoto zetu,” amesema Zitto.

Aidha, akinukuu maneno ya Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk. Fredrick Shoo aliyomueleza Rais Samia tarehe 16 Oktoba, 2021 alipokuwa mgeni rasmi katika miaka 50 ya Hospitali ya KCMC Moshi, Zitto alimuomba Rais Samia awaunganishe.

“Askofu Shoo alisema ‘ili Watanzania wawe na ustawi maana yake afya njema, pale ambapo wamejeruhika kwa sababu moja au nyingine Mama umruhusu Mungu akufanye uwe chombo cha kuponya watu majeraha yao’.

“Ni dhahiri kwamba kuna changamoto za hapa na pale na wewe ndio Rais wetu, tunakuomba sana kama ulivyoahidi katika hotuba yako ya kwanza wakati wa kuzindua Bunge, utuunganishe tumeparaganyika, uliweke Taifa pamoja. Na ninaamini utaliweka Taifa pamoja, tunakuomba sana,” amesema Zitto.

Rais Samia Suluhu Hassan

Hata hivyo, amesema licha ya kwamba viongozi wengine wa kisiasa hawapo katika mkutano huo, kwa sababu zao wenyewe, alimkumbusha Rais Samia namna walivyoshughulikia mgogoro mkubwa wa kisiasa Zanzibar mwaka 2001.

“Lakini kuna mwenzetu ambaye hayupo hapa kwa sababu za changamoto za kisheria na tuna utamaduni wa kumaliza haya mambo.

“Haitakuwa mara ya kwanza, tunao akina Hamadi Rashid … wakati umekuwa waziri kwa mara ya kwanza kule Zanzibar, ulikutana na mgogoro mkubwa ukazunguka na Mheshimiwa Rais Kikwete sehemu mbalimbali za dunia kwa ajili ya kutatua lile tatizo la mwaka 2001.

“Watu wote waliokuwa na kesi za jinai waliachiwa kwa lengo la kujenga muafaka kule Zanzibar.

“Tunakuomba sana kwa mujibu wa sheria na kufuata taratibu zote za kisheria tusaidia mwenzetu tuwe naye ili tuweze kufanya kazi kwa pamoja, tuunganishe nchi yetu, tufanye siasa kwa tija kwa masilahi ya nchi yetu,” amesema Zitto ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia Tanzania.

Zitto amekiongoza ACT Wazalendo kuhudhuria mkutano huo licha ya baadhi ya vyama vikuu vya upinzani nchini – Chadema na NCCR Mageuzi kutangaza kususia mkutano huo.

error: Content is protected !!