October 2, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Zitto amkaribisha Membe ACT-Wazalendo

Zitto Kabwe, Kiongozi wa ACT-Wazalendo akibadilishana mawazo ya Bernard Membe, Waziri wa zamani Mambo ya Nje Tanzania

Spread the love

KIONGOZI Mkuu (KC) wa chama cha ACT- Wazalendo, Zitto Zuberi Kabwe, amemkaribisha rasmi mwanadiplomasia mashuhuri nchini Tanzania, Bernard Kamillius Membe, kujiunga na chama chake. Anaripoti Faki Sosi, Kilwa …  (endelea).

Akizungumza na mamia ya wafuasi wa chama hicho, katika eneo la Njia Nne, wilayani Kilwa, mkoani Lindi, leo tarehe 30 Juni 2020, Zitto alisema, anamkaribisha Membe ndani ya ACT- Wazalendo kwa mikono miwili, “ili kuihami demokrasia nchini.”

Amesema, Membe ni mtu muhimu sana katika kipindi hiki ambako demokrasia na utawala bora, vimesiginwa na chama kilichoko madarakani.

“Tunamtaka Membe kujiunga na chama chetu, ili kuihami demokrasia na kupigania haki za wananchi,” ameeleza Zitto na kuongeza, “mtu yoyote anayeona ukandamizaji haufai, anapaswa kuungana na wenzake, kupinga vitendo hivyo.”

Soma zaidi:-

Zitto amesema, waziri huyo wa zamani wa mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa, amekuwa mstari mbele kupigani haki, jambo ambalo chama chake kimeona muhimu kumuomba kujiunga nacho.

Amesema, “mtu yeyote ambaye anaona demokrasia inakandamizwa afanye uamuzi sasa wa kuangana na wenzeke kuihami, na kwamba muda wa kufanya uamuzi huo ni sasa.”

Katika miaka ya karibuni, Membe amekuwa mstari wa mbele kupinga ukandamizaji na kutetea demokrasia.

Miongoni mwa maandishi yake ya karibuni kabisa, ni lile lililohusu utaratibu wa sasa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), katika kupata mgombea wake wa urais wa Jamhuri ya Muungano.

Katika maoni yake hayo, Membe alisema, hatua ya chama hicho tawala, kuzuia wanachama wengine, kujitosa katika mbio za urais, ili kusindana na rais wa sasa, John Pombe Magufuli, “ni uminyaji wa demokraisa.”

Zitto Kabwe, Kiongozi wa ACT-Wazalendo akiwa katika mkutano wa ndani wilayani Kilwa, Lindi

Alisema, hata chama cha Republicans cha Marekani, kimempitisha rais wa sasa, Donald Trump, kugombea tena nafasi ya urais, lakini baada ya kushinda katika kura za maoni.

Membe ambaye anadaiwa kuwa amefukuzwa uanachama wa CCM, amekuwa kwenye mgogoro na chama hicho, kufuatia madai kuwa anakihujumu.

Akiongea kwa sauti ya uenyenyekevu, Zitto aliwambia wananchi wa Njia Nne, kuwa ameulizwa sana kuhusu Membe, kwa hiyo “namwambia wakati wa uamuzi ni sasa.”

Amesema, wanajua kuwa anapigania uanachama wake ndani ya CCM, na kwamba hiyo ni haki yake.

Lakini Zitto anasema, “anafahamu kwa namna umasikini ulivyokithiri ndani ya nchi kwa namna CCM ilivyowatia umasikini wananchi wa mikoa ya Kusini …itakuwa uhaini kwa Membe kuking’ang’ani chama hicho.

“Nina msihi ndugu yangu Membe, wakati sasa umefika tuungane, tushirikiane. Watanzania wanataka mabadiliko. Naomba tuungane tuwape mabadiliko.”

Amesema, chama hicho kinasikitishwa na namna serikali ilivyosababisha umasikini kwa wavuvi kwa kutokana kuchomwa moto kwa nyezo zao.

“Nimeambiwa shughuli zenu ni uvuvi, kwa mara ya kwanza nashuhudia Waziri anatembea na rula kupima samaki , tumeshuhudia mkitiwa umasikini kwa vifaa vyenu ypvya uvuvi kuchomwa”

“Ni kiongozi gani kwenye nchi anataka wananchi wawe masikini. Haya ndio mambo ambayo sisi yanatutia unyonge ndio yanayotufanya sisi tuungane nanyi kuleta mabadiliko.”

Zitto yuko mkoani Lindi kwa ziara ya kikazi ya siku tatu ya kujenga chama chake. Katika ziara hiyo, Zitto amefuata na katibu mkuu wa chama hicho, Ado Shaibu na baadhi ya wabunge, akiwamo mbunge wa Kilwa Kusini, Selemani Bungara (Bwege).

Endelea kufuatilia MwanaHalisi ONLINE & MwanaHALISI TV kwa habari zaidi

error: Content is protected !!