Thursday , 28 March 2024
Home Habari Mchanganyiko Zitto amchambua bilionea Mufuruki, amuombea makazi mema Peponi 
Habari MchanganyikoTangulizi

Zitto amchambua bilionea Mufuruki, amuombea makazi mema Peponi 

Mwili wa Ali Mufuruki ukiagwa
Spread the love

MWILI wa mfanyabiashara mzalendo na ambaye amejipatia umashuhuri mkubwa nchini, Ali Abdul Mufuruki, aliyefariki dunia Jumapili iliyopita, nchini Afrika Kusini, unaagwa leo jijini Dar es Salaam. Unatarajiwa kuzikwa leo leo Jumanne, tarehe 10 Desemba, katika makaburi ya Kisutu. Mufuruki alikuwa mwenyekiti mwanzilishi wa jukwaa la wakurugenzi watendaji (CEO roundtable).  Zitto Zuberi Kabwe, mbunge wa Kigoma Mjini na Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT- Wazalendo, ni mmoja wa watu waliokuwa na ukaribu na Mufuruki. Hapa anaeleza jinsi alivyomfahamu…(endelea).

“Zitto mnahitaji mgombea urais anayeijua sekta binafsi vizuri, ili asaidie kuijenga Tanzania; ongea na Ali Mufuruki agombee urais.”

Haya yalikuwa maneno kutoka kwa mmoja wa marafiki zangu, mwaka jana katikati ya sakata la zao la Korosho. Nikamjibu kuwa Ali hawezi kukubali. Yeye ni mfanyabiashara. Hata hivyo, katika mazungumzo mbali mbali na watu wangu wa karibu, Ali Mufuruki amekuwa akiibuliwa.

Nakumbuka tulipopewa changamoto ya kuunda baraza la mawaziri linaloweza kuendesha nchi Chama Cha Mapinduzi (CCM), ikiondoka madarakani, Ali Mufuruki tumekuwa tukimtaja kama waziri wa fedha.

Hivi ndio namna Ali Mufuruki amekuwa akijadiliwa pengine bila hata yeye mwenyewe kujua kuwa alikuwa akijadiliwa. Siku moja nilipokutana naye Nairobi, nikamchokoza hilo la urais, akacheka sana. Akaniambia hayo ni mambo ya wengine. Mimi mfanyabiashara na ninasaidia nchi kupitia biashara.

“Buriani Mzee Ali Abdul Mufuruki, mhandisi mwenye mapito mengi kwenye biashara.”

Ali Abdul Mufuruki ametangulia mbele ya haki. Kwa wengi wetu ni msiba wa ghafla kwani hivi karibuni ameonekana akiendelea na shughuli zake kama kawaida.

Mara ya mwisho nimemwona katika mjadala alioufanya AzamTV akiwa vizuri tu (kwa macho ya mwanaadamu). Hata hivyo, sisi sote ni wake Allah na kwake tutarejea. Ali ametangulia kwa mola wetu na leo Watanzania wanamuaga kwa heshima zote anazostahili.

Mwaka 2019 umekuwa mwaka wa majonzi sana. Wafanyabiashara wakubwa wawili nchini wamefariki bila kumsahau ndugu Ruge Mutahaba ambaye naye kwa hakika alikuwa katika’ligi’ za Ali na Mzee Mengi, lakini kwa namna yake ya kukuza vipaji na kujenga himaya ya habari na burudani.

Ali Mufuruki sio tu alikuwa mfanyabiashara, bali alikuwa mfanyabiashara Mtanzania ambaye njia yake ni mafunzo makubwa sana kwa wengi.

Ninaamini kuwa Ali ameacha mapito yake kwenye maandishi na hivyo Watu wengi na hasa kizazi kijacho wataweza kujifunza kutoka kwake.

Septemba 30, 2019 Ali aliniandika ujumbe wa simu kuwa “nina mradi wa Kitabu changu na nataka nitulie kuhakikisha kuwa ninamaliza kitabu hiki ifikapo mwakani.” Allah alikuwa na mipango yake amemchukua kabla ya mwaka kuisha.

Nataraji familia itaweza kumaliza mradi huu ili vizazi vimsome Ali na mapito yake mpaka kuwa mfanyabiashara mkubwa nchini na mtu mwenye heshima tele.

Hata hivyo, Ali alikuwa na maono ya mbali na ameandika maono yake hayo kwenye Kitabu chake (pamoja na wenzake) kuhusu Viwanda. Kitabu hicho “Tanzania’s Industrialisation Journey 2016-2056:

From an Agrarian to a Modern Industrialized State in 40 Years” kina mawazo mazuri sana ya kuisaidia nchi yetu kutoka hapa ilipo na kuwa Taifa lenye maendeleo ya Watu wake.

Mapitio ya Kitabu hicho yaliyofanywa na Andrew Coulson (https://ceo-roundtable.co.tz/wp-content/uploads/ 2018/08/Tz-Industrialisation-Book-Review.pdf ) yanakupa ufupisho mzuri sana wa Kitabu hicho.

Ali alikuwa anapigia chepuo Tanzania kuwa dola la maendeleo (developmental state) na hasa umuhimu wa Tume ya Mipango ya Taifa. Bahati mbaya sana Serikali ya Awamu ya Tano imevunja tume hiyo.

Ni nadra sana hapa Tanzania na labda Afrika nzima  mfanyabiashara kama Ali Mufuruki kusisitiza umuhimu wa utamaduni wa taifa katika kile alichoita ‘National Exceptionalism‘ ikiwemo mavazi, chakula, historia yetu, ushairi nk.

Ali anaona utamaduni ni zaidi ya kutambulisha nchi, ni biashara. Wakati nadurusu hotuba ya Mwalimu Julius Nyerere ya 10 Desemba 1962, nilikuta anavyosisitiza kuhusu utamaduni wa taifa alipokuwa anaeleza sababu za kuunda wizara ya utamaduni.

Miaka 55 baadaye, Ali Mufuruki, mfanyabiashara sio mwanasiasa, aliandika kukumbusha namna utamaduni ulivyo ni mali. Bahati mbaya sana hatukumsikiliza Mwalimu Nyerere na sidhani kama tumemsikiliza Ali Mufuruki. Muhimu ni kuwa wote wameandika.

Nimesoma andiko la shahada ya Uzamivu la Chambi Chachage ambamo Ali Mufuruki amezungumzwa katika Sura ya Tano na Sita. Chambi ameeleza kwa ufasaha sana kukua kwa Ali Mufuruki kama mfanyabiashara kuanzia chini kabisa mpaka mafanikio aliyoyapata.

Natamani sana Chambi azalishe eneo hili kama makala kwa umma badala ya andiko la kitaaluma. Watanzania na Waafrika watajifunza jambo kubwa sana kutoka kwa Ali.

Kwamba Ali alikuwa mtumishi wa shirika la umma liitwalo Shirika la Uhandisi la Taifa (NECO), baada ya kutoka masomoni nchini Ujerumani. Aliamua kustaafu akiwa na miaka 30 tu na kuanzisha kampuni yake binafsi mwaka 1988 nchi ikiwa na uchumi hodhi wa dola, huo ni ujasiri ambao wengi wetu hatuna.

Kwamba aliweza kupenya katika ushindani wa biashara ya teknolojia mpaka kupanua biashara kwenye maeneo mengine, kama maduka ya nguo na majengo hadi kuwa utajiri wake ni simulizi yenye mafunzo makubwa.

Ali ameacha mchango Mkubwa sana kwa Tanzania haswa kwa Shirika letu la Ndege (ATCL). Alipoingia kama mwenyekiti wa Bodi wa ATCL mwaka 2002, nchi yetu ilikuwa ikimiliki asilimia 51 ya hisa za shirika, lakini alipotoka mwaka 2007, ameacha Nchi ikimiliki asilimia 100 ya hisa za kampuni hiyo ya umma.

Pamoja na kuwa kinara wa sekta binafsi nchini, Ali aliona ubinafsishaji wa ATCL ulishindwa kulifufua shirika hilo. Aliamua  kulirudisha shirika mikononi mwa umma.

Hata hivyo, Ali alipinga namna ATCL inayomilikiwa kwa asilimia 100 na umma namna inavyoendeshwa, kwa kuwa aliona uendeshaji husika hautaongeza tija na ubunifu, badala yake ungeturudisha kwenye matatizo yaliyosababisha ATCL ibinafsishwe. Ushauri wake hatujausikiliza.

Kitendo chake hiki akiwa Mwenyekiti wa Bodi ya ATCL, ni ishara ya imani yake ya “Dola la Kimaendeleo la Tanzania,” na kwamba tunapaswa kurekebisha mapungufu ya ubinafsishaji nchini, maoni ambayo pia Rais Mkapa (ambaye ubinafsishaji ulifanyika chini yake), ameyatoa kwenye kitabu chake kilichotoka hivi karibuni.

Nikiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mahesabu, moja ya kazi niliyokutana nayo ilikuwa ni kurejesha heshima ya Benki Kuu baada ya ufisadi mkubwa wa EPA.

Aliyekuwa gavana wa BoT wakati huo, Benno Ndulu, alifanya kazi kwa karibu nami katika kuhakikisha Bunge linasaidia kuzuia EPA nyengine kutokea. Wakati huo wote, Ali alikuwa kwenye Bodi ya BoT.

Mara kadhaa nilipokutana naye amekuwa akiniambia namna kipindi kile tulisaidia BoT kutimiza wajibu wake. Waliofaidika na EPA walikuwa mstari wa mbele kutaka Ndulu ashindwe kazi, PAC haikukubali na Ali alikuwa msaada mkubwa kwangu katika changamoto hii. Ali alitumikia BoT kwa weledi wa hali ya juu sana.

Maisha ya Ali ni mafunzo. Namna alivyoshirikiana na mkewe, Bi Saada Ibrahim katika kukuza biashara zao ni ushuhuda wa namna Ali alivyoishi na kuthamini nafasi ya mwanamke katika jamii. Ni Mfano bora kwetu tuliobaki duniani.

Mungu ampe Subira Saada na watoto katika wakati huu mgumu sana kwao. Mola amlaze Pema Ali Abdul Mufuruki.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

CAG: Wastaafu, wenza wao chanzo NHIF kufilisika

Spread the loveRIPOTI ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu...

Habari za SiasaTangulizi

Vikundi hewa 851 vyalamba bilioni 2.6 mikopo ya halmashauri

Spread the loveVIKUNDI hewa vya wajasirimali wadogo 851 kutoka katika halmashauri 19...

Habari za SiasaTangulizi

Mashirika matano yapata hasara mabilioni ya fedha

Spread the loveMASHIRIKA matano ya Serikali yanayojiendesha kibiashara, yamepata hasara ya mabilioni...

Habari Mchanganyiko

Mtandao watetezi wa haki za mazingira Tanzania waundwa

Spread the loveMTANDAO wa watetezi wa haki za mazingira nchini Tanzania, umeundwa...

error: Content is protected !!