May 20, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Zitto akumbushia sakata la Nape, yeye amjibu

Spread the love

 

KIONGOZI wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, ameliibua upya sakata la aliyekuwa waziri wa habari, utamaduni, sanaa na michezo, Nape Nnauye, kunyooshewa bastola na mtu asiyejulikana. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Tukio hilo lilitokea tarehe 23 Machi 2017, nje ya Hoteli ya Protea iliyoko Oysterbay mkoani Dar es Salaam, baada ya Nape kutaka kuzungumza na wanahabari.

Nape alitaka kuzungumza na waandishi wa habari, saa chache kupita baada ya aliyekuwa Rais wa Tanzania, Hayati John Pombe Magufuli, kutengua uteuzi wake.

Kupitia ukurasa wake wa Twitter, Zitto alikumbushia tukio hilo akisema, hatarajii kuona tukio kama hilo linatokea tena katika utawala wa sasa wa Rais Samia Suluhu Hassan.

“Miaka 4 iliyopita siku kama ya leo (23 Machi 2017) Nape alitishiwa bastola hadharani na mwanahabari Maulid Kitenge, akapambana na mwenye bastola bila woga. Nataraji kuwa hatutaona mambo yale ya ajabu tena katika nchi yetu,” ameandika Zitto.

Zitto aliandika ujumbe huo wakati akizungumzia hatua ya aliyekuwa Makamu wa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kuchukua madaraka ya urais kufuatia kifo cha Hayati Rais Magufuli, kilichotokea tarehe 17 Machi 2021, kwenye Hospitali ya Mzena, Makumbusho mkoani Dar es Salaam.

Kufuatia kifo cha Hayati Rais Magufuli, Samia aliapishwa kuwa Rais wa Tanzania, tarehe 19 Machi 2021, Ikulu jijini Dar es Salaam.

Hayati Rais Magufuli alifariki dunia akiwa madarakani, miezi mitano tangu alipoapishwa kuendelea na muhula wake wa mwisho katika Serikali ya awamu ya tano, tarehe 5 Novemba 2021, baada ya kushinda uchaguzi mkuu wa mwaka jana.

Akijibu kauli hiyo ya Zitto, leo tarehe 25 Machi 2021, Nape ambaye ni mbunge wa Mtama (CCM), amesema tukio hilo halitatokea tena.

“Hayata onekana tena, mimi nilikuwa wa kwanza na naamini yataisha pale. Mungu tusaidie,” Nape amejibu ujumbe huo.

Licha ya hoteli hiyo kuzuia mkutano huo usifanyike, Nape alifika katika eneo hilo huku askari polisi waliokuwepo katika eneo hilo wakimzuia asitoke nje ya gari yake.

Jambo lililopelekea mtu huyo asiyejulikana kumnyooshea bastola, akimlazimisha atii agizo la kurudi ndani ya gari.

Nape Nnauye, Mbunge wa Mtama (CCM)

Kufuatia purukashani hizo, Nape alilazimika kufungua mlango wa juu wa gari lake, kisha akasimama na kuanza kuzungumza na wanahabari, huku akihoji sababu za askari hao kumzuia asizungumze na wanahabari.

Katika mazungumzo yake hayo, Nape alisema alitaka kuzungumza na wanahabari ili amshukuru Rais Magufuli kwa kumteua kuwa waziri wa habari, utamaduni, sanaa na michezo, kisha kumpongeza Dk. Harrison Mwakyembe, aliyemteua kushika mikoba yake baada ya kutumbuliwa.

Mwanasiasa huyo alitumbuliwa kufuatia sakata la aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, kuvamia kituo cha TV na Redio cha Clouds, lililotokea mwaka 2017.

Kufuatia sakata hilo, Nape aliunda kamati ya uchunguzi wa tukio hilo, ambapo ripoti ya matokeo ya uchunguzi huo aliipeleka katika mamlaka husika, siku moja kabla ya kuondolewa katika nafasi ya uwaziri huo.

error: Content is protected !!