MBUNGE wa Kigoma Mjini na Kiongozi Mkuu wa chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Zuberi Kabwe, amedai kuwa kilichoelezwa kwenye waraka uliyotolewa na viongozi wakuu wawili wastaafu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahaman Kinana na Yusuf Makamba, ni sahihi na kinapaswa kuungwa mkono. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).
Katika taarifa yake kwa umma aliyoitoa leo, tarehe 18 Julai 2019, Zitto anasema, waraka uliotolewa na Kinana na Makamba, kuhusu mtu anayeitwa Cyprian Musiba, ni suala zito kuwa kuwa linagusa maslahi ya umma.
Zitto anasema, wana CCM hao wawili, wamewasilisha malalamiko yao kwa baraza lao la wazee, kutaka hatua zichukuliwe. Katika hali ya kawaida, suala hili lilipaswa kuwa jambo la CCM na kushughulikiwa na chama hicho wenyewe.
Hata hivyo, Zitto anasema, “jambo hilo limechukua mkondo wa kitaifa na haswa usalama wa watu na usalama wa taifa. Tamko la Kanali Kinana na Luteni Makamba limeujulisha umma mipango dhalimu ya kubumba kesi za uhaini kwa wanasiasa waandamizi nchini kutoka chama tawala na vyama vya upinzani.”
Anasema, “baadhi ya wana harakati ambao Bwana Musiba amekuwa akiwataja kuwa ni watu hatari kwa nchi ni miongoni mwa wahanga wa mipango hiyo. Kinana na Makamba, wametibua mpango huo ndio maana wafuasi au wanaojiita wanaomwunga mkono Rais John Magufuli wametaharuki na wanajaribu sana mipango yao iendelee.”
Mwanasiasa huyo ambaye ni mmoja wa watu ambao wamevuta wafuasi wa wengi nchini anasema, “…shabaha ya kesi ya uhaini ni kuhakikisha ama mwaka 2020 hapatakuwa na uchaguzi au uchaguzi ufanyike wakati wanasiasa wote waandamizi nchini wakiwa magerezani au wasiwepo kabisa.”
Anasema, “baadhi ya wanasiasa wameanza kujiokoa kwa kujiegemeza upande wa wenye mamlaka. Hata wale ambao kwa muda sasa wamekuwa ni tumaini la wananchi kwa kuwa wakosoaji wakuu wa serikali, wamerudi nyuma na kutoa kauli za kujikosha.
“Kwa mfano, mtu ambaye amekuwa akikosoa vikali serikali kule mwanzo nia ilikuwa ni kumnyima uhalali Rais Magufuli? Mbona wakati wa uongozi wa Rais Jakaya Kikwete alikuwa anashambuliwa sana na wazee kama vile Mzee Joseph Butiku, Joseph Sinde Warioba na wengine, lakini hatukusikia haya? Je, kuna kitu gani ‘special’ wakati huu? Nadhani huu ni wakati kwa wapenda demokrasia wote kutoogopa na kuwa pamoja,” ameeleza.
Anasema, “sisi wengine tunajua kitambo kuwa CCM imeshafika mwisho wake. Bahati mbaya sana CCM ya Magufuli inataka kuondoka na nchi yetu. Tusikubali.
“Tumesoma kuwa kabla ya wazee hao wastaafu wa CCM kuandika, waliomba ushauri na Mzee Pius Msekwa akawaambia ‘jibuni Mapigo.’” Anahoji: “ina maana Msekwa naye anataka kuua Chama chao? CCM ianguke yenyewe na ituachie nchi yetu.”
Zitto anasema, “hofu ya watawala kuhusu 2020, isihatarishe nchi yetu. Mipango ya kesi ya uhaini iachwe mara moja. Ukosoaji ndani au nje ya vyama vya siasa kamwe haiwezi kuwa uhaini. Acha demokrasia ishamiri.”
Leave a comment