October 3, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Zitto aikaba koo NEC, ZEC

Zitto Kabwe, Kiongozi wa ACT-Wazalendo

Spread the love

SAKATA la Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kutaka wakurugenzi wa halmshauri na manispaa kusimamia uchaguzi, linachukua sura mpya. Anaripoti Regina Mkonde … (endelea).

Zitto Kabwe, Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo akitoa taarifa ya Kamati Kuu ya chama hicho amesema, chama hicho kimeagiza wanasheria wake kufungua kesi ya kikatiba katika hati ya dharura.

Katika taarifa hiyo aliyoitoa leo tarehe 11 Juni 2019, wakati akitangaza maazimio ya kamati hiyo iliyoketi Jijini Dar es Salaam kwa mmuda wa siku mbili, kuanzia tarehe 9 hadi 10 Juni 2019.

Kamati hiyo imewaagiza wanasheria kufungua kesi kuomba tafsiri ya kimahakama, kuhusu hukumu iliyotolewa na Mahakama Kuu katika kesi ya kikatiba ya kupinga wakurugenzi kusimamia uchaguzi.

Zitto amesema, chama hicho kitafungua kesi hiyo ili kujua kama hukumu hiyo inaathiri ushiriki wa wakurugenzi wa halmashauri kama wasimamizi wa uchaguzi kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa.

“Kwa uzito wa kipekee, Kamati Kuu imeendelea kuwapongeza mwanaharakati Bob Chacha Wangwe na Wakili Fatma Karume kwa kusimamia vema kesi.

“…Mahakama Kuu ya Tanzania ilibatilisha vifungu kwenye sheria ya uchaguzi, ambavyo vilikuwa vinawapa nafasi wakurugenzi wa halmashauri ambao wengi ni makada wa CCM kuwa wasimamizi wa uchaguzi,” amesema Zitto.

Amesema, Kamati Kuu imewaagiza wanasheria wa ACT-Wazalendo kufungua mashtaka mahakamani ili kupinga baadhi ya vifungu vya Sheria ya Uchaguzi kwa madai kwamba, vinaipa mamlaka makubwa ZEC.

“Kwa upande wa Zanzibar, mabadiliko ya Sheria ya Uchaguzi yameipa ZEC mamlaka makubwa ya kuvuruga uchaguzi. Pia yameruhusu wanajeshi na watu wa usalama kupiga kura kabla ya siku ya uchaguzi jambo ambalo laweza kutumika vibaya, na hivyo kuiba uchaguzi iwapo halitawekewa utaratibu bora na wa haki kwa wadau wa uchaguzi,” amesema Zitto.

Wkati huo huo, Zitto amesema Kamati Kuu ya chama hicho imeazimia kuimarisha ushirikiano na vyama vingine vya upinzani, kwenye uchaguzi ujao wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu.

“Kamati Kuu imewaagiza viongozi wakuu wakuu wa chama kuendelea kushiriki kikamilifu kwenye ushirikiano na vyama vingine na pia kuhakikisha utekelezaji thabiti wa Azimio la Zanzibar lililoutangaza mwaka huu kuwa mwaka wa mapambano ya kudai demokrasia.

 “Pia, Kamati Kuu imemuagiza Katibu Mkuu wa Chama kuwaandikia makatibu wakuu wa vyama vyote tunavyoshirikiana navyo kuitisha kikao cha viongozi wakuu kutafakari namna bora ya vyama vya upinzani kushirikiana kwenye uchaguzi ujao wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu,” amesema Zitto.

error: Content is protected !!