Friday , 19 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Zitto aichongea CCM kwa WanaKigoma
Habari za SiasaTangulizi

Zitto aichongea CCM kwa WanaKigoma

Spread the love

ZITTO Zuberi Kabwe, mgombea ubunge Kigoma Mjini kupitia ACT-Wazalendo, ametoa sababu tano ambazo wananchi wa Mkoa wa Kigoma wanapaswa kutokichagua Chama Cha Mapinduzi (CCM). Anaripoti Mwandishi Wetu, Kigoma … (endelea).

Amesema, katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Jumatano tarehe 28 Oktoba 2020, wana Kigoma wanapaswa kuwachagua wagombea wa vyama vya upinzania.

Zitto ambaye pia ni Kiongozi wa chama hicho, amesema hayo jana Ijumaa tarehe 11 Septemba 2020 wakati akizindua kampeni zake za ubunge Kigoma Mjini.

Mambo hayo matano ambayo Zitto aliwaeleza wananchi wa Kigoma ni;

1.Umasikini: Mkoa wa Kigoma ni moja ya mikoa mitano masikini zaidi nchini Tanzania. Licha ya Utajiri mkubwa katika Kilimo, Uvuvi, Utalii na Biashara ya Kimataifa, Serikali ya CCM imeitenga Kigoma Kwa kuinyima Miradi ya Maendeleo ya Watu.

Mfano kwa miaka mitano Serikali imechelewesha Mradi wa Umwagiliaji Bonde la Mto Luiche wa Hekta 3000 unaofadhiliwa na Serikali ya Kuwait. CCM inaiweka Kigoma kwenye umasikini.

2. Bandari ya Kigoma: Uchumi wa Mkoa wa Kigoma ni Bandari ya Kigoma. Serikali ya CCM imeua Bandari ya Kigoma na hivyo kuua Biashara katika Mji wa Kigoma.

Wakati Bandari inaendeshwa na Kampuni ya AMI mzigo mwingi wa Kongo ( DRC ) ulikuwa unapita Bandari ya Kigoma. Sasa Bandari haipati mizigo.

Juhudi za kuboresha bandari zimekwamishwa na Serikali ya CCM kwa makusudi. Serikali ya CCM imezuia, kwa miaka mitano sasa, mradi mkubwa wenye thamani ya Shs Bilioni 100 kupanua Bandari ya Kigoma.

Msaada huu kutoka Serikali ya Japan umezuiwa Kwa makusudi ili kuhamisha Bandari kwenda Karema na kujenga Meli ya mizigo huko Karema. CCM inahujumu Bandari ya Kigoma. Hata Uwanja wa Ndege wa Kigoma ( Gombe/Mahale International Airport ) umehujumiwa na kupelekwa Chato.

3. Reli ya Kisasa: Wakati Serikali ya Awamu ya Nne iliyoongozwa na Jakaya Mrisho Kikwete inaondoka madarakani tarehe 5 Novemba 2015 mpango wa Ujenzi wa Reli ulikuwa ni kujenga Reli kutoka Dar – Tabora – Uvinza – Musongati ( Burundi ) ili kuifanya Uvinza kuwa Bandari Kavu na Kituo kikubwa cha Mizigo kutoka Nchi za Maziwa Makuu.

Serikali ya CCM ya awamu ya tano imebadilisha njia na kuamua kupeleka Reli Mwanza.

Bandari ya Kigoma inaweza kuhudumia 40% (kwenda Burundi na DRC) ya mizigo yote inayoingia Bandari ya Dar es Salaam wakati Bandari ya Mwanza inahudumia 6% tu (kwenda Uganda).

CCM imehamisha Mradi wa Reli na kuihujumu Kigoma.

4. Umeme: Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2015-2020 iliahidi Mradi wa Umeme wa Mto Malagarasi 44MW.

Baada ya Serikali ya awamu ya tano kuingia madarakani imeufuta mradi huo kwa kisingizio cha kujenga Bwawa la Rufiji (Stigler’s Gorge).

Mkoa wa Kigoma haupo Gridi ya Taifa na hivyo kukosa Umeme wa Uhakika Kwa ajili ya Maendeleo ya Viwanda.

Hata mradi wa sekta binafsi wa Umeme wa Jua (5MW ) ambao ungepunguza gharama za kuzalisha umeme hapa Kigoma Kwa 50% Serikali ya CCM imekataa kuutumia licha ya mradi huo kumalizika tangu Septemba 2017.

Benki ya Maendeleo ya Afrika ilitoa Fedha za Mradi wa Umeme wa Malagarasi lakini Serikali ya CCM ikalazimisha zipelekwe Stigler’s Gorge badala ya Igamba II. Hujuma za CCM dhidi ya Mkoa wa Kigoma hazimithiliki.

5. Barabara: Mkoa wa Kigoma ndio Mkoa Pekee ambao Wilaya zake Kongwe ( Kasulu, Kigoma na Kibondo ) hazijaunganishwa kwa lami.

“CCM wanaufanya Mkoa wa Kigoma kuwa wa mwisho kwa kila kitu. Barabara ya Uvinza – Malagarasi darajani Ina fedha za ufadhili wa Abu Dhabi Fund lakini Serikali kwa makusudi haifuatilii,” amesema Zitto

“Barabara ya Kigoma – Nyakanazi ndio sasa imepata fedha kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika kupitia Jumuiya ya Afrika Mashariki baada ya ucheleweshaji mkubwa uliofanywa na Serikali ya CCM ya awamu ya tano.”

Zitto amesema “Serikali ya Rais Magufuli imemaliza miaka mitano haijajenga hata kipande cha kilomita 1 ya barabara katika Mkoa wa Kigoma. CCM haiipendi Kigoma.”

“Kwa sababu hizi tano, mtu wa Kigoma anayechagua CCM hana mapenzi na Mkoa wa wake. Kila mwana Kigoma anapaswa kuikataa CCM ili Serikali iamke. Wana Kigoma wamefanya hivyo mara kadhaa na kufanikiwa.”

“Barabara za Mwandiga – Manyovu na Kigoma – Kidahwe, Pia daraja la Mto Malagarasi vimejengwa wakati Kigoma ilipoamua kuchagua wabunge wa upinzani na kuwanyima kura wagombea urais wa CCM,” amesema Zitto

Zitto amesema “wembe ule ule wa 2005, 2010 na 2015 tuugeuze upande wa pili kwa faida ya Kigoma. Kigoma bila CCM inawezekana. Mpende anayekupenda, asiyekupenda achana naye. CCM haipendi Kigoma, wana Kigoma tuachane na CCM.”

1 Comment

  • Watanzania wa Kigoma mjiepushe na hadaa za wanasiasa wenye malengo yao binafsi.
    Sikilizeni na kuchambua kwa kina kila kinachotamkwa na wanasiasa.
    Msikubali kutenganishwa ktk umoja wenu na watu hawa. “Akili ya.kuambiwa changanya na za kwako”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

KimataifaTangulizi

Mkuu wa majeshi Kenya afariki, Ruto atangaza maombolezo

Spread the loveRais wa Kenya, William Ruto ametangaza maombezo ya siku tatu...

Habari za SiasaTangulizi

Tanzania, Uturuki zanuia kukuza biashara, uwekezaji

Spread the loveSERIKALI za Tanzania na Uturuki zimekubaliana kuendeleza dhamira ya kuimarisha...

Habari za Siasa

Tume huru ya uchaguzi yatangaza ajira watendaji daftari wapiga kura

Spread the love  TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), imetangaza nafasi...

Habari za SiasaTangulizi

Chadema yatangaza ruti awamu ya pili maandamano

Spread the love  CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema awamu ya...

error: Content is protected !!