April 17, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Zitto afungua kesi kupinga Prof. Assad kuondolewa madarakani

Spread the love

ZITTO  Kabwe, Kiongozi  Mkuu wa ACT wazalendo, amefungua kesi ya Kikatiba katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, kupinga Uteuzi wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) uliofanywa na Rais John Magufuli. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Kesi hiyo ya Kikatiba namba 1/2020 iliyofunguliwa na Wakili Rugemeleza Nshala, kwa niaba ya Zitto, imepangwa kusikilizwa na Majaji Mlacha, Dk. Benhajj Masoud na Masabo katika mahakama hiyo.

Zitto amefungua kesi hiyo kupinga Sheria ya Ukaguzi namba 11/2008 na pamoja na uteuzi wa CAG Charles Kichere, kwa madai kwamba, ulikuwa kinyume na masharti ya Katiba.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na Suphian Juma, Afisa Habari wa ACT-Wazalendo, Zitto anaiomba mahakama hiyo kubatilisha uteuzi wa CAG Kichere.

“Zitto anaiomba Mahakama kutamka kuwa,  kifungu cha 6(1) cha Sheria ya Ukaguzi namba 11 ya mwaka 2008 inaenda kinyume na Katiba. Kwa kukiuka Ibara ya 144(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na pia kupingana na kifungu 62(a) cha Sheria ya Ukaguzi, ambacho kinaendana na Katiba,” inaeleza taarifa ya Suphian na kuongeza;

“Aidha Zitto anaiomba Mahakama kutamka pia,  uamuzi wa Rais Magufuli wa kumwondoa Ofisini Prof.  Mussa Assad ulikuwa kinyume na Katiba. Kwa sababu Prof. Assad hakuwa ametimiza miaka 65 ya kisheria wala miaka 60 ya Kikatiba. Pia kwamba uteuzi wa Bwana Kichere ufutwe kwa sababu ya kukiuka Katiba.”

Kwa mujibu wa taarifa ya Suphian, Shauri hilo litaitwa kwa mara ya kwanza tarehe 28 Januari , 2020.

error: Content is protected !!