December 2, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Zitto aeleza tume huru uchaguzi ilivyogonga mwamba kikosi kazi cha Rais

Zitto Kabwe, Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD)

Spread the love

KIONGOZI wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, amesema baadhi ya mapendekezo yaliyotolewa na wanasiasa wa vyama vya upinzani katika Kikosi Kazi cha Rais Samia Suluhu Hassan, yalishindwa kukubaliwa, ikiwemo upatikanaji wa tume huru ya uchaguzi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Zitto ametoa kauli hiyo leo Ijumaa, tarehe 28 Oktoba 2022 katika mkutano wa viongozi wa dini na wanasiasa, wa kuchambua ripoti ya kikosi kazi hicho.

“Ripoti hii sio asilimia 100 ya kile ambacho wengi tungependa kiwe, wala hata sidhani kama ni asilimia 70 lakini ni step forward, sio step backward na naomba hili nilisisitize kwenye masuala haya unakwenda kwenye mkutano na mambo yako 10,”

“Ukitoka na yote haukuwa mkutano sababu kuna wanaotaka hiki na wanaotaka hiki. Mkielewana kuna ambayo mtayapata na kwa hakika kuna baadhi mambo tumefanikiwa sana na kuna baadhi hatukufanikiwa kwa hiyo mapambano yataendelea,” amesema Zitto.

Mwanasiasa huyo amesema eneo la uchaguzi lilikuwa gumu katika kikosi kazi hicho, kutokana na mvutano uliokuwepo baina ya wajumbe wake.

“Lilikuwa eneo gumu sana hata kupata compromise (maelewano) iliyopatikana, baadhi yetu tuliingia kwenye kikosi kazi tukitaka tutoke na tume huru ya uchaguzi, Tutoke na uchaguzi wa Serikali za Mitaa kusimamiwa na Tume ya uchaguzi, tutoke na kuwepo sheria moja ya uchaguzi inayosimamia chaguzi zote nchini,”

“Sababu sasa hivi kuna Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa ambayo iko chini ya TAMISEMI, kuna sheria ya uchaguzi wa wabunge na Rais, kwa hiyo kuna sheria tofauti tukasema tuwe na sheria moja,” amesema Zitto.

Zitto amesema “mule ndani si kila mtu alikuwa anataka mageuzi na pia huwa kuna nguvu fulani hivi ya dola yaani mumtoe rais kabisa, inawezekanaje? Basi angalau wenyeviti na makamu wenyeviti wa tume wateuliwe na Rais, wengine waingie kwenye ushindani. Sisi tukaona as long as wamekubali wajumbe waombe kazi ni hatua ya mbele mengine tutayabadilisha mbele.”

Kiongozi huyo wa ACT-Wazalendo, amesema eneo lingine ambalo halikufanikiwa ni Tume ya Taifa ya Uchaguzi kutowatumia wakurugenzi wa halmashauri maarufu kama Ma-DED, katika maofisa wa chaguzi.

Amesema katika eneo la uchaguzi walichofanikiwa ni wajumbe wa tume ya uchaguzi kuomba nafasi hizo kisha kufanyiwa usaili.

“Tulichofanikiwa kikubwa ni wajumbe wa tume ya uchaguzi Rais kutoamka asubuhi na kutangaza wajumbe wa tume, mapendekezo ambayo kikosi imetoa mtu yeyote, Mtanzania yeyote anataka kuwa mjumbe aombe, afanyiwe usaili majina yapelekwe kwa Rais, Rais atateua kama nchi nyingine wanavyofanya.

Katika kipengele cha ushindani wa kisiasa, Zitto amesema pendekezo lao la marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa na kanuni zake limefanikiwa, ambapo kikosi kazi kimeshauri ifanyiwe marekebisho ili kuondoa kifungu kinachowapa mamlaka kuratibu mikutano ya hadhara.

Kuhusu mchakato wa katiba mpya, Zitto amesema kikosi hicho kimependekeza Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya 2011, ifanyiwe marekebisho ili kuanisha mchakato wake unapaswa kuwa vipi.

Pia, Zitto amesema kikosi hicho kimependekeza ufanyike mkutano wa kitaifa kwa ajili ya kujadili masuala yanayobishaniwa ikiwemo muungano wa Tanganyika na Zanzibar na madaraka ya Rais , ili yapatiwe suluhu.

“Kikosi kimependekeza baada ya sheria ya mabadiliko ya katiba kupitishwa bungeni na tayari maafikiano yamepatikana, iundwe jopo la wataalamu wachache wasiozidi watano waiangalie Rasimu ya Jaji Warioba,” amesema Zitto.

Hata hivyo, Zitto amesema mapendekezo mengine ambayo hayakufanyiwa kazi, yataendelea kupambaniwa.“Lakini its next struggle , umepata hiki, kingine fanyia kazi kwenye struggle inayofuata.”

error: Content is protected !!