Friday , 19 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Zitto aeleza ACT-Wazalendo itakayofanya ikiingia Ikulu
Habari za Siasa

Zitto aeleza ACT-Wazalendo itakayofanya ikiingia Ikulu

Spread the love

KIONGOZI wa chama cha siasa cha upinzani nchini Tanzania cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe amechambua masuala mbalimbali ambayo chama hicho endapo kikiibuka mshindi katika Uchaguzi Mkuu utaaofanyika Jumatano tarehe 28 Oktoba 2020 itayafanya. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea)

Uchaguzi Mku wa Zanzibar, wenyewe utafanyika kwa siku mbili tarehe 27 na 28 Oktoba 2020.

Zitto ametoa uchambuzi huo leo Jumatano tarehe 5 Agosti 2020 mbele ya wajumbe wa mkutano mkuu wa chama hicho unaofanyikia ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam akisema, Serikali itakayoundwa na ACT-Wazalendo itakuwa na kauli mbiu ya ‘kazi na bata,’

Lengo la mkutano huo ni kuteua wagombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wa Zanzibar. Pia, kupitisha Ilani ya uchaguzi kwa pande zote mbili ya Tanzania nay a Zanzibar.

Zitto ameanza kwa kusema, ninafuraha kubwa sana kuwa leo tupo tumejumuika hapa kwenye Mkutano Mkuu Maalum wa Chama chetu hichi chenye miaka sita tokea kuanzishwa kwake.

“Ni chama kichanga kuliko vyama vyote vilivyopo Tanzania kwa umri wake. Taaswira ya mkutano huu ni tofauti kabisa na umri wa chama chenyewe. Mkutano huu umejumuisha Wajumbe kutoka kila kona ya nchi yetu.”

“Hongereni sana wana ACT kwa kazi kubwa mnayoifanya ya kujenga chama imara. Kwa taaswira hii sina mashaka baada ya Oktoba 2020, ACT kitakuwa ni chama kinachoongoza Serikali,” amesema Zitto

“Wiki chache zijazo tutaanza kuzunguka nchi yetu, kila kijiji, kila kata na kila jimbo kuzungumza na wananchi kuhusu maono yetu juu ya nchi yetu. Tutawapa wananchi machaguo ya aina ya Watanzania wanayotaka kuishi katika miaka mitano inayokuja.”

Zitto amesema,wananchi watakuwa na chaguo la wazi kati ya Tanzania wanayoishi sasa au Tanzania mbadala ambayo sisi ACT Wazalendo tunataka kushirikiana nao kuijenga.

“Sisi tunakwenda kuwashirikisha Watanzania, wabara na wa Zanzibar, aina ya Taifa tunalotamani kuwa nalo, Tanzania yenye watu wenye hali bora kijamii na furaha ya kweli, yenye kujali utu, yenye mfumo mzuri wa utoaji haki, yenye demokrasia ya kweli, yenye uhuru na yenye uchumi jumuishi, imara na unaostawi,” amesema

Kiongozi huyo amesema, katika miezi miwili ya kuzunguka huko “tutakuwa tunakamilisha zoezi muhimu la kikatiba la kila miaka mitano Watanzania kupata fursa adhimu ya kuchagua viongozi wao. Uchaguzi wa mwaka huu ni uchaguzi muhimu sana katika maisha ya Taifa letu.”

“Kiongozi mkuu wa Taifa tunayekwenda kumchagua na wawakilishi wetu katika Baraza la Kutunga Sheria na mabaraza ya madiwani ndiye atakayetuongoza kuingiza nchi katika muongo wa sita tangu Tanganyika ipate uhuru na tangu Jamhuri ya Muungano iundwe.”

Zitto amesema, vile vile tunakwenda kuchagua kiongozi ambaye ataiongoza Zanzibar kuingia muongo wa sita tangu Mapinduzi ya Zanzibar. Kwa uzoefu wa miaka mitano iliyopita Watanzania wanakwenda kufanya maamuzi muhimu sana.

Huku akishangiliwa na wajumbe wa mkutano huo, Zitto amesema, uchaguzi wa mwaka 2020 ni uchaguzi wa kuchagua; uhuru wa kweli kwa kila mtu dhidi ya ukandamizwaji, matumaini dhidi ya hofu, amani na usalama kwa kila mtanzania dhidi ya tafrani na misukosuko nas iasa safi dhidi ya siasa za chuki na za kizandiki.

“Utaifa na mahusiano yenye tija kimataifa dhidi ya mgawanyiko na kujitenga, maendeleo Jumuishi ya watu dhidi ya maendeleo ya vitu, utajiri wa watu dhidi ya utajiri wa serikali,” amesema

Zitto amesema, muhimu zaidi ni uchaguzi wa kuchagua kurudisha utu na heshima kwa kila mtanzania hasa wanawake na watoto dhidi ya kejeli, manyanyaso ya makundi fulani ya jamii yetu.

“Ni uchaguzi wa watu dhidi ya uchaguzi wa vitu,”

Zitto amewaeleza wajumbe kwamba mkutano mkuu huu wa chama chetu leo, utafanya maamuzi muhimu ya ajenda hizi za uchaguzi wa mwaka huu na watu watakaobeba ajenda hizi.

“Ni matumaini yangu kuwa mtawapa Watanzania wagombea ambao kwa kuwatazama tu watarejesha nyuso za furaha na matumaini ambayo yamepotezwa katika miaka mitano iliyopita,” amesema Zitto

“ACT Wazalendo imedhamiria na kujiandaa kikamilifu kujenga na kuongoza Tanzania ya Watanzania. Tanzania ambayo kila mtanzania, mtoto, kijana, mwanamke, mwanamume, mzee, wa kijijini na mjini ana haki sawa mbele ya sheria na ana fursa stahiki za kujenga na kuzifikia ndoto zake.”

Katika kusisitiza hilo, Zitto amesema, “muhimu zaidi ni uchaguzi wa kuchagua kurudisha utu na heshima kwa kila mtanzania hasa wanawake na watoto dhidi ya kejeli, manyanyaso ya makundi fulani ya jamii yetu. Ni uchaguzi wa Watu dhidi ya Uchaguzi wa Vitu.”

Zitto amesema, “tunataka Serikali ambayo sio tu itatokomeza ubaguzi ila pia itafanya jitihada za makusudi kuhakikisha kila Mtanzania, bila kujali jinsia, dini, maumbile, itikadi, umri, kabila, anashiriki kikamilifu katika kuongoza taifa hili katika nyanja mbalimbali na anaishi maisha yenye mafanikio, maisha ya raha na furaha.”

“ Kauli mbiu yetu ya #KaziNaBata ni dhana jumuishi, kwa sababu kila Mtanzania, ana haki ya kufurahia Utanzania wake na maisha yake. Tunataka Watanzania wafanye kazi kwa bidii na pia wafaidi matunda ya jasho lao. Wawe na Raha na Furaha. #KaziNaBata,” amesema Zitto huku akishangiliwa na wajumbe wa mkutano huo

Kiongozi huyo amesema, kwenye Taifa lenye zaidi ya asilimia 80 ya watu wake wakiwa na umri chini ya miaka 35, ni dhamira yetu, kuwekeza na kutengeza sera, sheria na taratibu zitakazohakikisha kuwa vijana wa taifa hili wanakuwa kipaumbele na chachu ya maendeleo, kwao wao na kwa taifa.

“Tunataka Serikali zitakazoongozwa na ACT Wazalendo, zikatae kuona vijana wa nchi zetu mbili wananyang’anywa fursa, wanakatishwa ndoto zao, wanakandamizwa na kufanywa watwana ndani ya taifa lao,” amesema

“Tunataka kuona Serikali itakayoundwa na ACT Wazalendo, kuwa serikali ya vijana kwa ajili ya vijana wa Tanzania wa kike na wa kiume. Lakini pia kuandaa maisha stahiki uzeeni kwa kuwa na Mfumo Madhubuti wa Hifadhi ya Jamii kwa wote ambayo itahakikisha kuwa kila Mtanzania na kila Mzanzibari anakuwa na Bima ya Afya na Pensheni akifika umri wa kutoweza kufanya kazi,” amesema

Zitto amesema, tunataka kuhakikisha huduma za jamii bora, zenye ufanisi zinatolewa kwa wakati stahiki hazitakuwa na upendeleo kwa viongozi au watu wachache, bali zitakuwa kwa kila Mtu.

“Tunataka tuwe na elimu bora yenye kukidhi vigezo vya soko la ajira na kuwaanda wahitimu kuvumbua na kujiajiri.”

“Hatutaki kuona vijana wamalizapo vyuo vikuu au vyuo vya ufundi kuwa na mzigo wa madeni ndio maana Serikali itachukua mikopo yote iliyotolewa kwa wahitimu wa Elimu ya Juu mpaka sasa ili kuondoa mzigo kwa vijana kuhudumia madeni hayo.

“Na kuanza upya mfumo wa kugharamia Elimu kwa kutoa ufadhili wa gharama za masomo ‘tuition fee’ bure kwa watu wote watakaodahiliwa kwenye vyuo vya Elimu ya Juu na Vyuo vya Ufundi Mchundo. Vijana wote watakaojiunga na Elimu ya Ufundi ya VETA watasoma bila malipo ili kuondoa kikwazo cha vijana kupata Stadi na ujuzi kuendesha maisha yao,” amesema

Zitto amesema, “vijana wanaonisikiliza leo wana chaguo la wazi kabisa – kuchagua chama na mgombea wa chama ambacho kitaendelea kuwaweka katika mnyororo wa madeni au kuchagua chama na mgombea wa chama ambaye atawaondoa katika utumwa wa madeni ndani ya siku 100 baada ya kuingia madarakani.”

“Tunataka Serikali ambayo itahakikisha huduma bora za afya kwa watu wote na sio Serikali inayotamba kwa kujenga majengo. Chaguo kwa wanawake waja wazito lipo wazi katika uchaguzi wa mwaka huu – kati ya chama na mgombea wa chama ambacho kitaendelea kulipisha huduma za afya na kugeuza afya kuwa bidhaa kama nyanya sokoni kuchagua chama na mgombea wa chama ambaye atahakikisha kila Mtanzania ana Bima ya Afya na ana hifadhi ya Jamii ambayo ina mafao yatakayomwezesha asiwe na mashaka kabisa apatapo majanga. Ni uchaguzi ulio wazi kabisa,” amesema

Kuhusu uchumi, Zitto amesema, uchumi wa wananchi walio wengi na si uchumi wa Serikali na kundi la wachache.

“Tunataka Serikali itakayowekeza kwenye sekta zinazoajiri watanzania wengi, hasa Kilimo, Ufugaji na uvuvi, ili kuleta kilimo cha kimapinduzi ambacho kitawaondoa Wakulima, Wavuvi na Wafugaji kutoka katika dimbwi la umasikini. Wakulima, Wavuvi na Wafugaji wa Tanzania wana uchaguzi ulio wazi kabisa.”

“Tunataka Serikali ambayo itaboresha na kuwezesha ustawi wa sekta isiyo rasmi hasa ya biashara ndogo ndogo ambazo nyingi zinafanywa na wanawake na vijana,” amesema

“Mifumo ya kodi na urasimishaji biashara vitalenga katika kuleta ufanisi na kukuza biashara na si kudumaza na kuleta ukiritimba. Tafiti, sayansi na tekinolojia vitakuwa chachu katika kutengeneza fursa na kukuza uchumi jumuishi,” amesema

Zitto amesema, ACT Wazalendo kimeongoza juhudi za kuona tunakuwa na mashirikiano na vyama makini katika uchaguzi huu.

“Mwenyekiti wetu amefanya kazi kubwa sana ya kuwasilisana na baadhi ya viongozi wa vyama kufanikisha hili.”

“Kwetu sisi ushirikiano na vyama vyengine vya siasa vilivyo makini ni jambo muhimu sana katika kukabiliana na CCM. Tunaamini kupitia ushirikiano na vyama vyengine, kazi ya kuiondoa CCM Madarakani inakuwa rahisi mno kuliko kila chama kupigana kivyake,” amesema

Pia, zitto amesema, leo mtapokea pia tarifa ya maandalizi ya Ilani ya uchaguzi itakayowezesha yote niliyoyataja hapo juu. Niwaambie kuwa Wajumbe wa Kamati Kuu na Halimashauri Kuu wamefanya kazi kubwa ya kutupatia ilani bora ili wagombea wetu waweze kuwa na ajenda mahususi ya kutuwezesha kushinda uchaguzi mwaka huu.

Amesema, Ilani hizi ni dhamira ya chama katika kuifikia na kuijenga Tanzania ya watanzania na Zanzibar ya Wazanzibari, zaidi ni mkataba kati cha chama na watanzania na chama na Wazanzibari. Sisi, ACT Wazalendo tunaamini na tunawataka watanzania waamini pamoja nasi kuwa, INAWEZEKANA

✓ Kufanya kazi na kula Bata
✓ Kuishi Maisha ya Raha na Furaha
✓ Kuondoa Serikali dhalimu madarakani
✓ Kuwa na Serikali inayoheshimu sheria, utu, uhuru na ustawi wa watu wake
✓ Kujenga Uchumi jumuishi na endelevu
✓ Kila mtanzania kufikia ndoto zake
✓ Kuwa na umoja wa kitaifa na heshima kimataifa

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

CCM yakemea ufisadi, yaipa kibarua TAKUKURU

Spread the love  CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimekemea vitendo vya ubadhirifu wa...

Habari za Siasa

Bajeti ya Ikulu 2024/25 kuongezeka, bunge laombwa kurudhia Sh. 1.1 trilioni

Spread the love  WIZARA ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa...

Habari za SiasaTangulizi

Tanzania, Uturuki zanuia kukuza biashara, uwekezaji

Spread the loveSERIKALI za Tanzania na Uturuki zimekubaliana kuendeleza dhamira ya kuimarisha...

Habari za Siasa

Tume huru ya uchaguzi yatangaza ajira watendaji daftari wapiga kura

Spread the love  TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), imetangaza nafasi...

error: Content is protected !!