June 30, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Zitto achokonoa upya sheria za madini

Zitto Kabwe, Kiongozi wa ACT Wazalendo na Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD)

Spread the love

 

MAJUZI, Waziri wa Madini nchini Tanzania, Dotto Biteko ameainisha uwekezaji wa miradi mipya mikubwa mitatu inayoanza kufanyiwa uwekezaji nchini. Anaandika Zitto Kabwe, Dar es Salaam … (endelea).

Ametaja miradi hiyo, kuwa ni mradi wa dhahabu Nyanzaga wilayani Sengerema mkoani Mwanza; mradi wa Jumbo graphite wilayani Nachingwea mkoani Lindi na mradi wa Kabanga Nickel, uliyopo wilayani Ngara mkoani Kagera.

Hii ni miradi mikubwa sana, yenye uwekezaji wa thamani ya dola za Marekani 942 milioni. Katika orodha hii, sikutaja mradi wa rare earth metals, madini ambayo ndio yanaendesha simu za mkononi, kompyuta na magari ya umeme. Mradi huu unafanyika mkoani Songwe.

Ukijulimsha miradi yote hii pamoja na miradi mingine, kiwango cha fedha za uwekezaji kinazidi dola za Marekani 1 bilioni.

Hii ni hatua inayostahili pongezi nyingi kwa serikali kwa ujumla, lakini pia kwa waziri wa madini na watumishi wote wa wizara hiyo.

Waziri wa Madini, Dotto Biteko

Aidha, miradi hii inakuwa miradi ya kwanza kufanyika nchini tangu mabadiliko makubwa ya sheria ya madini mwaka 2017; mabadiliko ambayo kwa kiwango kikubwa siyaungi mkono kwa kuwa yana madhara makubwa zaidi kwa nchi kuliko sheria ya madini ya mwaka 2010.
Mradi wa Kabanga Nickel una madini ya Cobalt mengi sana na ndio madini yenye thamani kubwa.

Cobalt ni sehemu ya madini ambayo pia inaendesha simu zetu na magari ya umeme na hii ndio sababu kubwa ya Marekani na China kugombania Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), ambayo ina asilimia 60 ya hifadhi ya Cobalt duniani.

Kwa lugha nyingine, haya ni madini mkakati. Mwenye kudhibiti Cobalt ndio mwenye dunia kwa miaka 50 ijayo. Tani moja ya Cobalt ilikuwa inauzwa dola 53,500 za Marekani mwezi Oktoba 2021.

Tanzania inatarajia kuuza nje tani 3,000 za Cobalt kwa mwaka zitakazoingiza zaidi ya dola za Marekani 160 milioni kwa mwaka.

Kwa upande wa Nickel tutanarajia kuuza nje takribani tani 40,000 kwa mwaka zitakazoingiza dola za Marekani 700 milioni.

Mradi huu peke yake unaweza kuingiza zaidi ya dola za Marekani bilioni moja kwa mwaka kwa miaka karibu 30 ijayo.

Hata hivyo, ni mradi wenye mazonge yake kutokana na kugubikwa usiri mkubwa wa namna mwekezaji alivyopatikana.

Profesa Palamagamba Kabudi

Mnamo tarehe 19 Januari 2021, serikali iliingia mkataba na kampuni ya LZ Nickel ya Uingereza, ambayo siku moja baadaye ikabadili jina na kuitwa Kabanga Nickel limited.

Wakati huo kampuni ilikuwa na mfanyakazi mmoja na asset (aseti) za paundi milioni 8 tu, lakini serikali ikawapa mradi uliotafitiwa kwa dola za Marekani 250 milioni. Kwa maana hiyo, tumewafanyia utafiti bure.

Thamani ya fedha zilizowekwa kwenye utafiti zilikuwa nyingi sana kiasi kuugawa mradi ule bure, ni jamnbo linaloshangaza wengi. Siamini kuwa timu ya majadiliano ya serikali iliyoongozwa na Prof. Palamagamba Kabudi ilikuwa haijui ukweli huu.

Kama hawakuwa wanajua, basi mikataba mingi ambayo timu hii imeingiza nchi kwayo, itakuwa ni ya hovyo sana. Muda utasema.

Maswali ya msingi ya kujiuliza: Ni kwanini hatukufanya zabuni ya wazi ya mradi huu badala ya njia ya maombi ya kawaida ya leseni?

Serikali kwa mujibu wa sheria ilichukua leseni zote za miradi iliyokuwa haiendelezwi (retainer licences), jambo ambalo pia lilikuwa hovyo kwani ni sawa na utaifishaji.

Rais Samia Suluhu Hassan

Kwanini sasa serikali hiyo hiyo ikaamua kutoa bure mradi ambao umefanyiwa kazi na ambao umetumia mabilioni shilingi za walipa kodi wa taifa hili? Hawa LZ Nickel Limited ambao hawapo kwenye soko lolote la hisa duniani walipatikanaje?

Nyaraka zinaonesha kampuni hiyo ilisajiliwa Februari mwaka 2019, ikaanza mazungumzo na serikali Agosti 2020 na kupewa mgodi Januari 2021.

Je, timu ya majadiliano ya serikali chini ya Prof. Kabudi iliijua lini ampuni hii? Kampuni ilijuaje kuwa serikali inataka kutoa mashapo haya kwa kampuni nyengine?

Mpaka kufikia wakati kampuni ya LZ/Kabanga inaingia mkataba na serikali, ilikuwa na wamiliki 18, na kwamba kampuni ya Lifezone Limited, ilikuwa na hisa nyingi Zaidi. Yenyewe ilikuwa na hisa 100,000 kati ya hisa zote 343,894 ambazo sawa na asilimia 29.

Katika wanahisa wote hapakuwa na hata mmoja mwenye uzoefu wa uchimbaji wa Nikeli popote ulimwenguni. Nilitumia njia zangu mbalimbali kuwajulisha watu wa serikali kuhusu makosa makubwa wanayofanya katika jambo hili, lakini hakuna aliyesikia.

Prof. Kabudi na timu yake iliyojadiliana na mwekezaji wa mkataba huu wa LZ/Kabanga Nickel wamefanya dhambi kubwa ambayo huko usoni itakapofahamika wataingia kwenye historia mbaya sana.

Nina taarifa kuwa kampuni hii ni mali ya Barrick Gold kwa mgongo wa nyuma. Yawezekana Prof. Kabudi na timu yake, waliamua kuwapa zawadi Barrick Gold baada ya majadiliano yao kuhusu mgogoro wa Acacia.

Hili tutaweza kulifafanua zaidi siku za usoni, lakini ibakie kuwa mradi wa Kabanga Nickel, ni mradi wa Barrick uliofichwa kupitia kampuni ya LZ Nickel ya Uingereza.

Ni muhimu sana serikali iweke wazi wamiliki wote (beneficial owners) wa LZ/Kabanga Nickel. Kuna tatizo kubwa zaidi kwenye mikataba ya uendeshaji ambayo Tanzania inaingia na makampuni haya kwa kinachoitwa Framework Agreements.

Tangu makubaliano ya Barrick Gold na Serikali ya Tanzania ya kuundwa kwa kampuni ya Twiga Minerals yafikiwe, wananchi wamepokea mambo haya kibubusa bila kufanya tathmini ya kina.

Kwamba, sheria mpya ya madini inakataza mikataba ya madini ambayo tuliita MDAs. Lakini ukitazama kwa jicho la uchambuzi, hizi Frameworks Agrements ni sawa na kurudi kwenye MDAs. Serikali inatuambia kuwa inamiliki asilimia 16 ya hisa kwenye migodi, lakini ukisoma hizi Framework Agreements, unakutana na kitu tofauti.

Kwamba, umiliki uko kwenye hiyo kampuni ya uendeshaji na sio migodi. Sheria ya madini ya mwaka 2010 na kanuni zake, inataka mgodi mmoja mmoja uorodheshe hisa zake kwenye Soko la Hisa la Dar es Salaam mpaka asilimia 35 ya mgodi mzima.

Lakini hizi Framework Agreements zilizoandaliwa na Prof. Kabudi na wenzake, zinatoa mianya ya wawekezaji kutoorodhesha hisa katika soko la hisa la Dar es Salaam.

Muhimu kuliko yote ni kuwa leseni ni ya mwekezaji sio ya kampuni Hodhi kwa hiyo hicho kinachoitwa asilimia 16 kinakuwa kiini macho tu.

Kwa mfano, kampuni ya Tembo ambayo ndio ubia kati ya serikali na LZ/Kabanga Nickel haina leseni ya madini ya Nickel. Mwenye leseni ni LZ/Kabanga Nickel. Mwenye leseni ndio mwenye mali.

Walichotufanya kina Prof. Kabudi na timu yao ya majadiliano (GNT), ni kutuuzia nyumba ambayo mmiliki wa kiwanja ni mwengine. Jambo linalonishangaza, ni kuwa Serikali mpya ya Rais Samia Suluhu Hassan, bado imeendelea kuwatumia kina Prof. Kabudi katika mazungumzo ya miradi mingine.

Siku Rais akishtuka kuhusu ubovu ya hizi Frameworks Agreements, nchi yote itakuwa imeshawekwa rehani. Kinachoitwa GNT kivunjwe na kazi yote ifanywe na Tume ya Madini.

Vile vile, zinazoitwa Frameworks Agreements zifutwe na kila mwekezaji aingize mtaji wake kwa mujibu wa Sheria. Hata usiri wa mikataba ya madini bado ni tatizo kubwa, ambalo linaondoa imani ya wananchi kuwa miradi hii ina maana yeyote kwao.

Uchambuzi niliofanya kwenye uwekezaji wa mradi wa Kabanga Nickel, unaonyesha kuwa bado tunatoa rasilimali za taifa kama zawadi kwa wanaoitwa wawekezaji.

Uchambuzi huo huo unaweza kufanywa kwa makubaliano ya Serikali na Barrick Gold kupitia Twiga Minerals. Ni muhumu tukaweka mikataba hii ya wazi ili Serikali ipate mrejesho kutoka kwa wananchi wake, jambo ambalo litasaidia kuwapo maboresho zaidi.

Jambo lingine la kufanyiwa tathmini ni maandalizi yetu katika fungamanisho kati ya sekta ya madini na sekta nyengine za uchumi.

Mathalani, mpaka sasa, mgodi wa Geita Gold bado unazalisha umeme wake wenyewe. Shirika la umeme la taifa (TANESCO), halijaweza kufikisha umeme mgodini na hivyo kutopata mapato ya dola za Marekani 3 milioni ila mwezi, ambazo sawa na Sh. 80 bilioni kwa mwaka.

Migodi hii mitatu mipya na mwengine wa Rare Earth Metals huko Songwe inahitaji umeme na ndio hatua ya kwanza ya fungamanisho.. Nyanzaga hakuna umeme mkubwa, Kabanga hakuna umeme mkubwa, Lindi hakuna umeme mkubwa na wala Songwe, hivyo tunarudi kwenye makosa yaleyale.

Ni wajibu wa serikali kuhakikisha kuwa TANESCO wanafikisha umeme kwenye migodi hii na mingine inayokuja ili kufaidika na uwekezaji wake.

Pamoja na kumpongeza Waziri Biteko kwa kazi kubwa ya kuwezesha miradi hii niliyotaja,ambayo itasababisha kuongeza mauzo ya Tanzania nje kwa dola za kimarekani 6.3 bilioni, ndani ya miaka mitatu ijayo na kwa miaka takribani 30 ijayo, anapaswa kuanza maandalizi ya fungamanisho.

Ukumbi wa Bunge

Ni muhimu waziri wa madini afanye kikao na waziri wa nishati ili kuhakikisha kuwa migodi yote iliyopo na mipya itatumia umeme wa Tanesco ambao sasa asilimia 60 unatokana na Gesi Asilia ya hapa hapa nchini na asilimia 25 unatokana na maji, hivyo fedha yote itabakia Tanzania.

Afanye hivyo kwa sekta zote. Ni nasaha zangu pia wizara ya madini ishughulike moja kwa moja na mikataba ya madini kupitia Tume ya Madini badala ya kinachoitwa Timu ya Majadiliano ya Serikali ambacho ni kichaka chenye madhara makubwa kwa uchumi wa taifa na madhara hayo tutayaona siku sio nyingi.

Tanzania haipaswi kufurahia faida za takwimu tu bali wananchi wake wanapaswa kufaidika na matunda katika mnyororo mzima wa thamani ili rasilimali zetu zifaidishe watu wetu.

Ni aibu kubwa kwamba mpaka leo Geita Gold (GGM), wanazalisha umeme wenyewe kwa mafuta ya dizeli na hivyo kusababisha fedha nyingi nje. Mikataba ya madini sasa iwekwe wazi kwa mujibu wa sheria za nchi yetu. Hakuna sababu yeyote ile inayozuia mikataba hiyo kuwekwa wazi.

Mwandishi wa makala haya, Zitto Zuberi Kabwe, kitaaluma ni mchumi. Amewahi kuwa mbunge wa Kigoma Kaskazini na Kigoma Mjini, kwa nyakati tofauti. Kwa sasa, ni kiongozi wa chama cha siasa cha ACT- Wazalendo, kinachounda Serikali ya Umoja wa Kitaifa na Chama Cha Mapinduzi (CCM), Visiwani Zanzibar.

error: Content is protected !!