May 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Zitto ‘achambua’ kauli ya Mama Samia, Majaliwa

Zitto Kabwe, Kiongozi wa ACT-Wazalendo

Spread the love

 

ZITTO Kabwe, Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, amesema kauli ya Mama Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Tanzania na Waziri Mkuu, Kasim Majaliwa kwamba ‘Rais John Magufuli yupo na anaendelea na majukumu yake,’ haijajibu maswali. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).

Zitto ametoa kauli hiyo leo Jumanne tarehe 16 Machi 2021, kupitia waraka wake kwenda kwa wananchi, akieleza ufafanuzi zaidi unahitajika kwa kuwa, suala la afya ya rais si suala binafsi.

“Hata kauli ya Makamu wa Rais jana akiwa njiani kwenda mkoani Tanga haikukidhi haja, imeongeza mshawasha badala ya kuzima tetesi zilizoenea, imeacha maswali mengi zaidi badala ya kujibu maswali yanayoulizwa kuhusu afya ya rais, imeibua sintofahamu zaidi badala ya kuleta utulivu kwa wananchi,” ameeleza Zitto.

Katika siku za hivi karibuni, baada ya Rais Magufuli kutoonekana hadharani kwa zaidi ya wiki mbili, kumeibua mjadala katika vyombo vya habari vya ndani na nje ya nchi kuhusu afya yake na kule alipo.

Mara ya mwisho, Rais Magufuli alionekana hadharani tarehe 27 Februari 2021, katika hafla fupi ya kumwapisha Dk. Bashiru Ally, kuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Ikulu ya Dar es Salaam.

Ijumaa wiki iliyopiota, Waziri Mkuu, Majaliwa akiwa msikitini wilayani Njombe, alitamka kuwa amezungumza na Rais Magufuli na kutaka Watanzania wapuuze kauli za kuzua taharuki kuhusu afya ya rais kwani anaendelea na majukumu yake kama kawaida.

Pia, jana Jumatatu, tarehe 15 Machi 2021, Mama Samia akiwa katika siku yake ya kwanza ya ziara mkoani Tanga, alisema Rais Mafufuli anawasalimu wakazi wa mji huo kwa kumchagua kuwa rais kwa awamu nyingine.

Zitto amesema, ni vizuri kwa serikali kumaliza mjadala mkali unaoendelea kwenye vyombo vya habari vya nje na mitandao ya kijamii kwa serikali kueleza hali halizi.

Na kwamba, kukithiri kwa mijadala hiyo, kunaendelea kuibua sintofahamu kwa wananchi hasa baada ya serikali kutotoa ufafanuzi zaidi.

Rais John Magufuli

“Kukithiri kwa mijadala hiyo kumesababisha hali ya wasiwasi na taharuki miongoni mwa wananchi. Hali hiyo inatia shaka zaidi na kutokuonekana hadharani kwa rais mwenyewe kwa takriban siku 16 sasa.”

“Aidha, ukimya wa hali ya juu miongoni mwa viongozi serikalini kumeongeza uzito wa suala hili,” amesema Zitto.

Kwenye waraka huo, Zitto ameshauri mambo kadhaa ikiwa ni pamoja na serikali kuwaacha huru watu wote waliokamatwa na Jeshi la Polisi kwa kuhoji juu ya afya ya rais.

Ameiomba mamlaka kueleza wananchi hali halisi ya afya ya rais, itumie pia maelezo hayo kutujibu kwa kina wananchi iwapo Rais bado anao uwezo wa kutekeleza majukumu yake au la.

“Katibu Mkuu Kiongozi atamke rasmi kuwa Makamu wa Rais amekuwa akitekeleza madaraka ya rais kwa mujibu wa Katiba na kwamba ni Kaimu Rais kwa mujibu wa itifiki zote,” ameeleza.

Pia, ameshauri Chama cha Mawakili (TLS) na AZAKI nyengine za uwajibikaji kupaza sauti zao kulinda Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

error: Content is protected !!