April 13, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Zitto aandika barua nyingine, sasa IMF aitaka kuikagua BoT

Zitto Kabwe, Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo

Spread the love

KIONGOZI wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe ameeleza kuwa ameliandikia barua Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), kulitaka kuja nchini kuifanyia ukaguzi Benki Kuu (BoT), kutokana na kuwa na mashaka ya ukaguzi uliofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa hesabu za serikali (CAG). Anaripoti Faki Sosi, Dar es Salaam … (endelea)

Zitto ameyasema hayo leo tarehe 11 Aprili 2020, wakati akihutubia kupitia vyombo vya habari vya mtandao ambapo ametanabaisha kuwa kutokana na kashfa ya wizi wa fedha za EPA Serikali, Benki Kuu, Bunge na CAG walikubaliana kuwa Benki Kuu inapaswa kukaguliwa na chombo huru kwa niaba ya CAG.

Soma hotuba kamili ya Zitto ya uchambuzi huo wa CAG

UCHAMBUZI WA RIPOTI ZA MDHIBITI NA MKAGUZI MKUU WA HESABU ZA SERIKALI WAKATI YA UTAWALA WA AWAMU YA TANO CHINI YA RAIS JOHN POMBE MAGUFULI

UTANGULIZI

Ndugu zangu, Watanzania wenzangu, leo tarehe 11 Aprili, 2020 siku moja kabla ya Sikukuu ya Pasaka, siku ambayo kwa ndugu zetu Wakristo kote ulimwenguni ni siku muhimu na yenye kuleta tafakari kwa ustawi wao kiimani, nimeona niitumie kuwasilisha uchambuzi wa Chama chetu, ACT Wazalendo, chama ambacho kimeendelea kujipambanua kama Chama mbandala na kinachozielekeza katika kujadili masuala makubwa ya kitaifa na kupendekeza suluhu yake.

Kwa kuzingatia utamaduni wetu huo, na baada ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuwasilisha Taarifa yake kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019; Sisi ACT Wazalendo, tumeisoma, kuipitia na kuichambua taarifa husika, kwa lengo la kuitumia ili itusaidie kutimiza wajibu wetu wa kuisimamia Serikali kama chama mbadala nchini na kama Chama cha Upinzani Bungeni.

Katika uchambuzi wetu wa mwaka huu, tumeona ni bora pia tufanye mapitio ya Taarifa za CAG kwa miaka yote mitano ya Serikali ya Awamu ya Tano (2015/16 – 2018/19) Hivyo, uchambuzi wetu utakuwa ni uchambuzi mtambuka tangu Serikali ya Rais Magufuli ilipoingia madarakani hadi sasa. Uchambuzi huu unaibua ukweli mmoja tu kwamba Miaka 5 ya Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Magufuli ni Miaka 5 ya kushindwa kazi, na ni Miaka 5 ya kufuja fedha za Watanzania, yaani “Five years of Incompetence”.

Kwa kuwa uchambuzi wetu umebaini masuala mengi, na kwa kuwa hatutaweza kuwa na muda wa kutosha kujadili masuala yote hayo, uchambuzi wetu umejielekeza katika masuala makubwa 10, kama ifuatavyo.

Kuporomoka kwa Makusanyo ya Kodi

Ndugu Wananchi,

Mtakumbuka tangu Serikali ya Rais Magufuli iingie madarakani imekuwa ikijinasibu kuwa kinara wa ukusanyaji kodi. Kupitia tarifa mbalimbali za TRA na Msemaji Wa Serikali, tumekuwa tukiaminishwa kwamba ukusanyaji wa mapato umeongezeka katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Tano.

Hata hivyo, Uchambuzi wa ACT Wazalendo kwenye Ripoti ya CAG umebaini kwamba, uwezo wa Serikali ya Magufuli wa kukusanya mapato kulinganisha na Pato la Taifa umeshuka kwa kiwango cha kutisha. Hii inapelekea Serikali kushindwa kutekeleza Bajeti iliyopitishwa na Bunge na kuifanya Bajeti kuwa haina maana.

Suala hili tumekuwa tunalizungumza kila mwaka tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie Madarakani. Kwenye Bajeti ya Serikali ya mwaka wa Fedha wa 2016/17 (mwaka wa kwanza kamili wa Serikali ya Awamu ya Tano), Serikali ilipanga kukusanya shilingi 29.5 trilioni, kwa mujibu wa ripoti ya CAG ya 2016/17, kati ya fedha hizo, Serikali ilikusanya shilingi 25.3 trilioni tu. Na hivyo, kutokufikia lengo la makusanyo kwa 14.33%.

Bajeti ya Pili, Mwaka 2017/18, jumla ya shilingi 31.7 trilioni zilitarajiwa kukusanywa na zilipitishwa kutumika na Bunge. Serikali iliweza kukusanya kutoka vyanzo vyake vyote shilingi 27.7 trilioni tu. Hivyo kutofikia lengo la makusanyo kwa 12.66%.

Bajeti ya Tatu, Mwaka 2018/19 Jumla ya Shilingi Trilioni 32.5 zilitarajiwa kukusanywa. Lakini kwa mujibu wa Taarifa ya CAG, Serikali ilikusanya shilingi Trilioni 25.8 tu. Hivyo kutofikia lengo la makusanyo kwa 21%. Makusanyo ya Mapato yote ya Serikali katika mwaka 2018/19 yalikuwa madogo kuliko Bajeti ya mwaka uliotangulia wa 2017/18 kwa Shilingi Trilioni 1.9, yaani chini ya 7% ya Bajeti ya Pili ya Serikali ya Awamu ya Tano. Kwa miaka 3 ya mwanzo ya Serikali ya Awamu ya Tano wastani wa lengo lisilofikiwa ni 16%.

Ukilinganisha na Serikali iliyopita, kwa miaka mitatu ya mwisho wa Serikali hiyo, wastani wa lengo lisilofikiwa na Serikali katika ukusanyaji wa mapato ya Bajeti lilikuwa ni 6.3% tu – ambapo kwa mwaka 2013/14 lengo halikufikiwa kwa 9%, kwa  mwaka 2014/15 nako lengo halikufikiwa kwa 4%, na kwa mwaka wa fedha wa 2015/16 lengo halikufikiwa kwa 6% tu.

Ndugu Wananchi,

Duniani kote ufanisi wa Taifa kukusanya kodi hupimwa kwa kutazama uwiano wa Makusanyo ya Kodi kwa thamani ya shughuli za uchumi katika nchi husika, yaani Tax/GDP Ratio kwa lugha ya kiuchumi. Wakati Serikali ya Awamu ya Tano inaingia madarakani mwaka 2015/16 Uwiano wa Makusanyo ya Kodi kwa Pato la Taifa ilikuwa ni 13.68% – Maana yake Katika shilingi 100 inayozalishwa katika Uchumi, shilingi 13.7 zilikuwa zinakusanywa na Serikali kama Mapato.
Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa miaka Mitano, 2015/16 mpaka 2020/2021 uliweka lengo la Uwiano wa Makusanyo ya Kodi kwa Pato la Taifa kuwa 20%. Kiwango cha Juu kabisa cha kiashiria hiki kilifikiwa mwaka 2013/14 wakati wa Awamu ya Nne ambapo ilikuwa 16.9%.

Kipimo hiki cha Ufanisi kinaonyesha kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inashindwa kukusanya kodi kulingana na ukuaji wa uchumi wa Taifa.Kwa Mujibu ya Ripoti za CAG,  Mwaka 2016/17 Uwiano wa Makusanyo ya Kodi kwa Pato la Taifa ulishuka mpaka 13.2%, mwaka 2017/18 ulikuwa 12.8% na Mwaka 2018/19 umekuwa 11.4%.Kwa kutumia kipimo hiki Tanzania inashika mkia katika EAC.

Hii ndiyo hali katika Miaka 5 ya Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Magufuli, Ni Miaka 5 ya kushindwa kazi na ni Miaka 5 ya kufuja fedha za Watanzania, yaani “Five years of Incompetence”.

Deni la Taifa linakua kwa kasi kuliko kasi ya Ukuaji wa Uchumi

Ndugu Wananchi,

Pamoja na kuporomoka kwa uwezo wa Serikali ya Magufuli katika ukusanyaji wa kodi, Serikali hiyo pia imeendelea kupalilia ukuaji wa deni la Taifa. Serikali ya Awamu ya Tano iliingia madarakani Deni la Taifa likiwa ni Shilingi Trilioni 33.5 Mwezi Juni, 2015. Deni hilo liliongezeka kwa 22% kufikia Shilingi Trilioni 41 ilipofika Mwezi Juni, 2016.

Katika ukaguzi wa CAG wa mwaka 2015/16, alionyesha kuwa mikopo ya Biashara yenye riba kubwa na muda mfupi wa kuiva kabla ya kulipa iliongezeka kwa kasi zaidi ndani ya muda mfupi. Kati ya Juni 2015 na Juni 2016 MIkopo ya Biashara iliongezeka kwa 31%. Vile vile CAG alionyesha kuwa Serikali ilikopa katika soko la ndani 42% ya kiwango ilichopaswa kukopa na hivyo kusababisha madhara makubwa kwenye uchumi ikiwemo mzunguko wa Fedha kuporomoka na kusabaibsha hali ngumu ya maisha ya wananchi.

Mwaka 2016/17 mwenendo wa Deni la Taifa uliendelea kuwa ule ule ambapo Deni liliongezeka kwa 12% kufikia Shilingi Trilioni 46. Serikali iliendelea kukopa zaidi ya kiwango kwenye soko la ndani ambapo dhamana za Serikali ziliongezeka kwa 26% zaidi ya kiwango kilichoruhusiwa na Bunge katika Bajeti.

Vilevile, mwaka 2016/17 CAG alieleza kuwa Serikali ilikopa zaidi ya kiwango kinachotakiwa kutoka Benki Kuu ya Tanzania kwa jumla ya Shilingi Trilioni 1.5 na kusababisha riba ya mkopo huu kuzidi kwa 269% kufikia shilingi 157 bilioni. Suala kama hili lilitokea katika ukaguzi wa mwaka 2015/16 ambapo Serikali ilichota fedha Shilingi Bilioni 441 kutoka Benki Kuu kinyume cha sheria na kuficha mkopo huo (hidden loan) wakaguzi wasione.

Mwaka 2017/18 mwenendo wa Deni la Taifa uliendelea kukua kwa tarakimu mbili ambapo Deni liliongezeka kwa 11% kufikia Shilingi Trilioni 51. Mwaka 2017/18 Serikali ilianza kushindwa kulipa Deni la ndani kutoka kwenye mauzo ya hati fungani kama ambavyo imekuwa kawaida ya miaka ya nyuma. Mwaka huu Serikali ilipaswa kulipa madeni yenye thamani ya Shilingi Trilioni 6.1 lakini kutoka kwenye soko la ndani iliweza kukusanya shilingi Trilioni 5.7 tu. Mwenendo wa Serikali kuvunja sheria ya Benki Kuu kwa kukopa zaidi ya kiwango na kujaribu kuficha deni iliendelea ambapo shilingi 212 bilioni zilichotwa kutoka Benki Kuu katika mwaka huu wa Fedha wa 2017/18.
Mwaka huu ambao tunafanyia uchambuzi, Deni la Taifa limefikia Shilingi Trilioni 53 ilipofika Juni 2019, deni lilikuwa kwa 4% tu kutokana na kukosekana kwa mikopo ndani na nje ya nchi kufuatia hali mbaya ya Uchumi ambayo ni zao la maamuzi ya Serikali. Tutaona hili pia kwenye suala la makusanyo ya kodi.

Ukuaji huu wa deni la Taifa, haujawahi kushuhudiwa tangu nchi hii imeasisiwa, na sisi ACT Wazalendo tumekuwa tukitilia mashaka mwenendo wa ukuaji wa deni hilo. Uchambuzi wetu unaonyesha kuwa Deni la Taifa limekuwa kwa wastani wa 12.25% kwa mwaka kati ya mwaka 2015/16 – 2018/19.  Wakati deni hilo likiumuka hivyo, chini ya Serikali ya Rais Magufuli, ukuaji wa Pato la Taifa la Tanzania (GDP) umekua kwa wastani wa 6% tu, yaani, deni la Taifa limekuwa mara mbili zaidi ya ukuaji wa Pato la Taifa.

Kutokana na kukua kwa kasi kwa Deni la Taifa kiwango cha Bajeti kwa ajili ya kuhudumia Deni (kulipa deni na riba) kimeongezeka kwa kutoka Shilingi Trilioni 6.3 Mwaka 2015/16 hadi Shilingi Trilioni 10 mwaka 2018/19. Kwa vyovyote vile, hali hii ndiyo inayosababisha “vyuma kukaza”.

Hii ndiyo hali katika Miaka 5 ya Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Magufuli, Ni Miaka 5 ya kushindwa kazi na ni Miaka 5 ya kufuja fedha za Watanzania, yaani “Five years of Incompetence.”

Deni la Shilingi Trilioni 2.7 za watoa huduma

Ndugu Wananchi,

Kutokana na ukusanyaji wa kodi mdogo, na uwezo mdogo wa kubuni vyanzo vipya vya mapato. Uchambuzi wetu umebaini kwamba, mwaka 2015/16 madai dhidi ya Serikali ( accumulated libalities OR Payables) yalikuwa ya jumla ya shilingi Trilioni 1.98 ambapo ziliongezeka mpaka shilingi Trilioni 2.8 mwaka uliofuata wa 2016/17, ongezeko la 40% katika mwaka mmoja.

Mwaka 2017/18 madai ya Watu (Makampuni binafsi, wakandarasi nk ) dhidi ya Serikali yaliongezeka mpaka kufikia shilingi Trilioni 3 sawa na ongezeko la 15% kutoka mwaka uliopita. Mwaka 2018/19 madai haya yameshuka kidogo mpaka shilingi Trilioni 2.7, lakini ni kiwango kikubwa sana cha pesa za watu ambazo Serikali inazishikilia mkononi baada ya kupokea huduma za Watu hao.

Ukijumlisha na Madai ya marekesho ya Kodi ambayo sekta binafsi wanaidai Serikali yenye thamani ya takribani shilingi Trilioni 2. Kwa muktadha huo, ni dhahiri kwamba, mchawi wa mdororo wa uchumi ni Serikali yenyewe, kwani inashikilia fedha za wakandarasi na watoa huduma na hivyo kudumaza shughuli za uzalishaji mali, na wakati mwingine kufukarisha wananchi. Taasisi inayoongoza kuwa na madai makubwa ni Wakala wa barabara nchini (TANROADS) ambapo katika mwaka wa Fedha 2018/19 ilikuwa inadaiwa Shilingi Bilioni 949 ikiwemo adhabu (penalties) za thamani ya Shilingi Bilioni 224.

Hii ndiyo hali katika Miaka 5 ya Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Magufuli, Ni Miaka 5 ya kushindwa kazi na ni Miaka 5 ya kufuja fedha za Watanzania, yaani “Five years of Incompetence”.

Serikali haina tena uwezo wa kulipa Madeni ya Ndani kwa Ukamilifu

Ndugu Wananchi,

Kama tulivyokwisha bainisha hapo awali, kuhusu uwezo mdogo sana wa ukusanyi wa kodi chini ya Serikali ya Rais Magufuli. Kwa mwaka wa fedha 2018/19, makusanyo yote ya kodi za Serikali yalikuwa jumla ya Shilingi Trilioni 15.1 tu wakati malipo yote ya madeni ya ndani na nje yalikuwa jumla ya Shilingi Trilioni 10, sawa na 67% ya makusanyo yote ya TRA. Hii ni maana yake ni kuwa katika kila shilingi 100 zilizokusanywa na TRA mwaka 2018/19, Shilingi 67 zililipa Deni la Taifa, hivyo nchi kubakia na Shilingi 33 tu kugharamia mambo mengine ikiwemo kulipa mishahara ya watumishi na miradi ya maendeleo.

Kutokana na hali hii, Serikali ilikopa ili kulipa madeni, lakini bado pesa ilizokopa pia hazikutosha, kutokana na soko la ndani kudorora. Serikali ilipanga kukopa Shilingi Trilioni 5.7 lakini ikapata shilingi Trilioni 3.9 tu sawa na 68% ya matarajio. Uchambuzi wetu unaonyesha kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inayoundwa na Chama cha Mapinduzi imeshindwa kusimamia vema Uchumi wa Taifa kiasi kwamba haina uwezo wa kusimamia Deni la Taifa kiasi cha kushindwa kulipa Deni la Ndani (Rollover) kwa ukamilifu wake.

Tumeona kuwa uwezo wa soko la mikopo ya ndani kulipa Deni la ndani ulikuwa 68% tu ya Deni zima, maana yake 32% ya malipo ya madeni ya ndani ilibidi yatoke ama nje au kutolipwa. Yote haya yamesababishwa na uwezo mdogo wa Viongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano.

Hii ndiyo hali katika Miaka 5 ya Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Magufuli, Ni Miaka 5 ya kushindwa kazi na ni Miaka 5 ya kufuja fedha za Watanzania, yaani “Five years of Incompetence”.

Ufichaji wa Madeni ya Serikali kwa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii

Ndugu Wananchi,

Mbaali na ukusanyaji hafifu wa kodi, ukuaji wa deni la Taifa na kushindwa kulipa madeni ya ndani. Uchambuzi wetu umebaini kwamba, Serikali imekuwa ikieleza Deni la Taifa kuwa dogo kuliko uhalisia. Mathalan, mwaka 2015/16, Deni la Taifa liliripotiwa bila kutajwa kwa Shilingi Trilioni 3.2 ambazo mifuko ya Hifadhi ya Jamii inaidai Serikali. Mwaka 2016/17 Jumla ya Shilingi Trilioni 4.6 hazikuripotiwa kwenye Deni la Taifa.

Kutotambua madeni haya kwenye Deni la Taifa kunaweka hatarini uhai wa mifuko ya hifadhi ya jamii ambayo wastaafu wanategemea kwa maisha yao ya kila uzeeni. Tanzania hupata wastaafu takribani 3500 kila mwaka, hivyo kutotambua madeni ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kwenye Deni la

Taifa kunasababisha wastaafu wengi kuhangaika bila kulipwa mafao yao kwa muda mrefu.
Mwaka 2018/19 pekee CAG alikagua mafaili ya wastaafu 3,820 ambao wangepaswa kulipwa Jumla ya Shilingi Bilioni 157.6 kama mafao yao. Wastaafu karibuni wote wa Mwaka huu wa Fedha hawajalipwa mafao na bado wanahangaika mitaani kufuatilia mafao yao.

Hii ndiyo hali katika Miaka 5 ya Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Magufuli, Ni Miaka 5 ya kushindwa kazi na ni Miaka 5 ya kufuja fedha za Watanzania, yaani “Five years of Incompetence”.

Ufisadi kupitia Mizigo inayokwenda nje (transit goods)

Ndugu Wananchi,

Mnafahamu kwamba, nchi yetu ni lango kuu la kupitisha bidhaa mbalimbali kwenda nchi jirani.  Pamoja na uzembe wa Serikali ya CCM, unaofanya tusinufaike sana na bandari zetu za Dar es salaam, Mtwara na Tanga, lakini bandari hizo zimekuwa chanzo cha mapato ya Serikali.

Kila Mwaka CAG hukagua mizigo inayokwenda nje ya nchi kupitia bandari zetu, kujiridhisha endapo imevuka mipaka ya nchi au la. Katika Mwaka wa Fedha 2018/19 CAG ameonyesha kuwa Bidhaa zenye thamani ya Kodi ya Shilingi Bilioni 312 ziliingizwa nchini kama transit lakini hazikutoka nje ya mipaka yetu.

Wakati Serikali ya Awamu ya Tano inaingia madarakani mwaka 2015/16 kodi iliyokwepwa kwa transit goods ilikuwa Shilingi Bilioni 42. Mwaka 2017/18 upotevu huu wa Kodi ulifikia Shilingi Bilioni 108. Ongezeko la ukwepaji kodi kupitia njia hii umekua kwa 742%!.

Huu ni uthibitisho kuwa ama uwezo wa Serikali kusimamia makusanyo ya Kodi kwa Bidhaa zinazokwenda nje ya nchi ni mdogo au Serikali imeachia Wafanyabiashara wachache kufaidika na ukwepaji huu wa kodi kwa sababu wanazozijua wenyewe.

Hii ndiyo hali katika Miaka 5 ya Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Magufuli, Ni Miaka 5 ya kushindwa kazi na ni Miaka 5 ya kufuja fedha za Watanzania, yaani “Five years of Incompetence”.
Kesi za thamani ya Shilingi Trilioni 1.68 dhidi ya Serikali zipo Mahakamani (Continget Liabilities)
Eneo lingine ambalo uchambuzi wetu umegundua ni madeni yanayoibuliwa na kesi mbalimbali ambazo Serikali inafunguliwa na watu mbalimbali kutokana na mikataba ambayo watu hao waliingia na Serikali.

Katika kipindi tunachotazamia kuanzia mwaka 2015/16 mpaka sasa, mashtaka dhidi ya Serikali yameongezeka sana na hivyo kuongeza kiwango cha madeni yanayoweza kuibuka (contingent liabilities ). Mwaka 2015/16 Serikali ilikuwa na kesi kwenye mahakama mbalimbali zenye madai ya Jumla ya shilingi Bilioni 850. Mwaka 2016/17 ziliongezeka kesi zenye thamani ya shilingi Bilioni 135. Mwaka 2017/18 Madai dhidi ya Serikali kutokana na kesi yaliongezeka kwa Shilingi Bilioni 52 na mwaka 2018/19 yameongezeka kwa jumla ya shilingi bilioni 639.

Kutokana na maongezeko ya Madai yanayozaliwa na kesi zilizopo mahakamani Serikali ina kesi zenye thamani ya shilingi Trilioni 1.68 kwa mujibu wa Taarifa za CAG za miaka ya Fedha 4 iliyochambuliwa. Ongezeko la madai dhidi ya Serikali linaongezeka kwa kasi sana na hii inatokana na Serikali kutojali mikataba ambayo imeingia na wawekezaji nchini. Ongezeko la madai dhidi ya Serikali kati ya mwaka 2017/18 na 2018/19 lilikuwa ni kwa asilimia 1228! Hii ni ishara kuwa Serikali yetu haiminiwi tena na watu wanaona bora waende Mahakamani tu. Pia inaonyesha uzembe wa hali ya juu wa Serikali katika kushughulikia mikataba mbalimbali.

Hii ndiyo hali katika Miaka 5 ya Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Magufuli, Ni Miaka 5 ya kushindwa kazi na ni Miaka 5 ya kufuja fedha za Watanzania, yaani “Five years of Incompetence”.

Manunuzi yasiyofuata Sheria yenye thamani ya Shs Trilioni 1.41

Ndugu wananchi,

Uchambuzi wetu unaonyesha kuwa, Jumla ya Hoja za Ukaguzi kwenye eneo la Manunuzi ya Umma ni Shilingi Trilioni 1.4 ( 2015/16: Shs Bilioni 148.5, 2016/17: Shs Bilioni 627, 2017/18: Shs Bilioi 570, 2018/19: Shs Bilioni 66 – Taarifa ya CAG 2018/19 haikujumuisha Taarifa kadhaa nyeti mwaka huu).

Hoja kubwa katika Ukaguzi wa CAG wa miaka yote ya nyuma kabla ya 2018/19 ni hoja ya Manunuzi kutoka nje ya watoa huduma wasiothibitishwa na Serikali (goods from UNAPPROVED Suppliers). Hoja hii imekuwa Hoja ya Kudumu katika Ripoti zote za CAG Sura ya Tisa. Mwaka 2017/18 manunuzi ya namna hii yalikuwa na thamani ya Shilingi Bilioni 432.

Hata hivyo, kwa sababu ambazo hatujazibaini, Ukaguzi wa mwaka 2018/19 umeliacha eneo hili kabisa. Bado tuko kwenye mshangao, hatujui CAG amelazimika kuficha nini?. Je? Ni maelekezo kutoka juu?, ni kuifichia aibu Serikali? Au ni kufunika kombe, katika mwaka huu wa uchaguzi?
Hii ndiyo hali katika Miaka 5 ya Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Magufuli, Ni Miaka 5 ya kushindwa kazi na ni Miaka 5 ya kufuja fedha za Watanzania, yaani “Five years of Incompetence”.

Serikali kutumia fedha bila kupitishia kwenye Mfuko Mkuu

Ndugu Wananchi,

Katika uchambuzi wa Taarifa ya CAG tuliofanya mwaka 2018 tulionyesha kuwa shilingi Trilioni 1.5 hazikujulikana zimekwenda wapi. Hoja yetu hiyo ilipelekea kufanyika kwa uhakiki maalumu na CAG, na ambapo bado Serikali ilishindwa kuonyesha zilipokwenda fedha hizo, zaidi ya kudai kuwa ilihamishia Ikulu matumizi ya shilingi 976 bilioni kati ya hizo 1.5 trilioni bila kumpa CAG uthibitisho wa uhamishaji huo wala kuonyesha fedha hizo zimefumikaje huko Ikulu.

Katika uchambuzi wetu wa Mwaka 2019 tulionyesha kuwa katika ukaguzi wa CAG wa Bajeti ya mwaka 2017/18 ameonyesha kuwa shilingi Bilioni 800 hazikutolewa kwa ukaguzi. Mwaka huu hali imekuwa tofauti ambapo kiwango cha Fedha kilichotolewa kutoka Mfuko Mkuu wa Serikali kwenda kwenye Matumizi ya Serikali kilizidi kiwango kilichokuwamo kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali. Kiwango kilichozidi kilikuwa ni Shilingi Trilioni 1.2 ambazo zilitolewa kama Mkopo (overdraft ) kutoka Benki Kuu ya Tanzania.

Tatizo kubwa la mwaka huu ni kuwa Katiba ya nchi imevunjwa kwa Serikali kupokea Fedha na kuzitumia bila kwanza kupita kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali. Katiba ya Tanzania inataka kuwa fedha yote inayokusanywa kutoka vyanzo vyote vya mapato lazima iingie Mfuko Mkuu wa Serikali kabla ya kuruhusiwa kutolewa ili kutumika.

Katika mwaka wa Fedha 2018/19 Serikali ilitumia Shilingi Trilioni 1.7 bila kwanza kupita kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali. Baadhi ya Fedha hizi zinatokana na Mikopo kutoka Nje, Shilingi Trilioni 1.2 ambapo CAG anasema zilikwenda kulipia miradi ya Maendeleo moja kwa moja.

Ni muhimu sana nifafanue kwa ufupi ni kwa nini eneo hili ni muhimu katika usimamizi wa Fedha za Umma. Kwa mujibu wa Katiba yetu, hakuna fedha ya umma inayotoka kutoka Mfuko Mkuu wa Serikali bila idhini ya CAG. Kwa hiyo matumizi ya Fedha za Umma yakitumika bila kupita Mfuko Mkuu wa Serikali maana yake ni kuwa CAG hajaidhinisha.

Hii ni hatari sana kwani ni rahisi sana fedha za Umma kutumika vibaya. Hizi shilingi Trilioni 1.7 zinazotokana na mikopo kutoka nje zimelipwa huko huko nje, kwa mfano, kununua ndege za ATCL, zinaweza kuwa zimetumika kuweka kwenye akaunti za watu binafsi huko nje. Fedha kutopita Mfuko Mkuu wa Serikali ni kichaka cha kukwepa udhibiti wa CAG ili kufanya ubadhirifu. Uvunjifu huu wa Katiba umeshamiri tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani.

Tangu mwaka 2015/16 CAG amekuwa akionyesha namna Katiba haizingatiwi lakini pia namna mifumo ya udhibiti katika Mfuko Mkuu wa Serikali haizingatiwi. Mwaka 2015/16 kulikuwa na tofauti ya Shilingi Trilioni 2.9 katika masalio ya fedha katika Hesabu Jumuifu lakini Serikali haikuweka wazi (no disclosure ) kiasi cha kusababisha Hesabu Jumuifu za Taifa kutokuwa sahihi na kupata Hati Mbaya ya Ukaguzi. Mwaka 2016/17 Shilingi 1.5 Trilioni hazikutolewa uthibitsho wa matumizi yake kwa ajili ya ukaguzi.

Mwaka 2017/18 Shilingi Bilioni 800 pia hazikuwa na uthibitisho wa matumizi yake. Mwaka 2018/19 Mfuko umetoa Fedha zaidi ya ilizopokea na shilingi Trilioni 1.7 hazikuingizwa kabisa Mfuko Mkuu. Yote haya yanatokea kwa sababu ya kukosekana kwa mifumo madhubuti ya uwajibikaji kwani uvunjifu wa Katiba ni kosa kubwa linalostahili adhabu kubwa.

Hii ndiyo hali katika Miaka 5 ya Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Magufuli, Ni Miaka 5 ya kushindwa kazi na ni Miaka 5 ya kufuja fedha za Watanzania, yaani “Five years of Incompetence”.

Ukaguzi wa Benki Kuu ya Tanzania mashaka

Wakati akikabidhi Ripoti ya Mwaka 2018/19 kwa Rais, CAG alisema kuwa moja ya mafanikio ya mwaka huu ni Ofisi ya Ukaguzi ya Taifa kufanya ukaguzi wa Benki Kuu. Napenda kuwakumbusha Watanzania kuwa kufuatia kashfa ya Wizi wa Fedha za EPA Serikali, Benki Kuu, Bunge na CAG walikubaliana kuwa Benki Kuu inapaswa kukaguliwa na chombo huru kwa niaba ya CAG.

Ilikubaliwa kuwa Moja ya Makampuni makubwa ya Ukaguzi ( The Big 4 ) duniani ndio yawe yanafanya ukaguzi huo. Mwaka 2018 Serikali iliaamua kununua Korosho kwa kutumia Fedha kutoka Benki Kuu.

Kutokana na Korosho zile kukosa soko mpaka wakati Mwaka wa Fedha unakwisha Juni 2019, Fedha zilizochukuliwa kutoka Benki Kuu hazikuwa zimerudi. Serikali haikutaka hoja hii kuonyeshwa katika Taarifa ya Ukaguzi. Vile vile, katika manunuzi ya Ndege kutoka Kampuni mbalimbali ambazo Tanzania imeagiza ndege kulikuwa na Fedha ambazo zimetolewa Benki Kuu na kulipwa kwa Akaunti nyengine kabla ya kulipwa kwa kampuni zinazotengeneza ndege.

Ili kuficha mambo haya iliamuriwa kuwa Kampuni Binafsi zisikague tena Benki Kuu ya Tanzania. Aliyekuwa CAG wakati huo hakukubaliana na maamuzi haya kwa maandishi. Tunatoa Wito kuwa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) lifanye ukaguzi Maalumu wa  Benki Kuu ya Tanzania ili kubaini kinachofichwa.

HITIMISHO

Ndugu Wananchi,

Bila shaka yoyote ile, Serikali ya CCM ya Awamu ya Tano chini ya Rais Magufuli haingependa ukweli huu ujulikane na Watanzania masikini ambao fedha zao wanazokatwa katika kodi ndizo zimekuwa zikifisidiwa na kufujwa. Lakini sisi kama Chama makini na Chama Mbadala kinachotegemewa na Watanzania kuongoza Mabadiliko wanayoyataka tuna wajibu wa kuwaonesha kwamba Miaka 5 ya Serikali hii si chochote bali ni ya ulaghai uliokusudiwa kuficha Miaka 5 ya kushindwa kazi na Miaka 5 ya kufuja fedha za Watanzania.

Njia pekee ya kubadilisha haya ni kuiondosha CCM madarakani. Watanzania hatuwezi kuendelea kukamuliwa kila siku ili fedha zetu zikafujwe namna hii na wajanja wachache wanaotulaghai kwamba eti ndiyo wakombozi wetu. Wanatwambia Hapa Kazi Tu, kumbe ni Kazi ya kupiga hela za Watanzania. Hali hii imechosha! Hali hii imetosha! Na sisi ACT Wazalendo tumedhamiria kuifikisha mwisho. Tutashirikiana na nyinyi Watanzania kuhakikisha tunaiondosha hali hii na tunaunda Serikali Mpya inayowajibika kwenu na  ambayo italinda kila senti ya fedha zenu zinazokusanywa kutokana na kodi zenu na itakayotuletea maisha ya raha na furaha kwa kila mmoja wetu.

Mwisho kabisa, pamoja na salamu zangu za Pasaka kwa wananchi wote, ninapenda kutumia fursa hii kuwasihi ndugu zangu Watanzania, tuendelee kuchukua tahadhari kubwa kuhusu janga la KORONA. Hata tunapojiandaa kusherehekea sikukuu ya Pasaka, tuendelee kujihadhari sana, na kusikiliza tahadhari tunazopewa na wataalamu wa afya.

Ahsanteni sana.

Kabwe Z. Ruyagwa Zitto
Kiongozi wa Chama
ACT Wazalendo
Aprili 11, 2020
Dar es salaam

error: Content is protected !!