KIONGOZI wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, amedai kama dosari zinazoendelea kujitokeza katika chaguzi ndogo visiwani Zanzibar, hazitatokomezwa, Uchaguzi Mkuu wa 2025 utakuwa mbaya zaidi ya Uchaguzi Mkuu wa 2020. Anaripoti Mwandishi Wetu, Zanzibar…(endelea).
Zitto ametoa kauli hiyo leo Jumatatu, visiwani Zanzibar, akibainisha dosari 15 zinazodaiwa kujitokeza katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Mtambwe, uliofanyika tarehe 28 Oktoba mwaka huu, ambapo aliyekuwa mgombea wa ACT-Wazalendo, Dk. Mohamed Ali Suleiman, alitangazwa kuwa mshindi.
“Mnafahamu mambo mbalimbali yalifanyika ambayo sisi tunaona kama ishara mbaya na hasi tunapoelekea uchaguzi mkuu wa 2025. Matarajio yote ambayo tumekuwa nayo kwa ajili ya mageuzi ya kiuchaguzi hapa Zanzibar ni kama mambo hayaendi kokote,” amesema Zitto.
Zitto amesema “sababu kila jambo ambalo limelalamikiwa katika uchaguzi wa 2020, limetokea katika uchaguzi mdogo wa Mtambwe na si Mtambwe peke yake, limetokea katika chaguzi ndogo zilizofanyika hapa Zanzibar.”
Akitaja dosari hizo, Zitto alidai daftari la wapiga kura lilikuwa na wapiga kura hewa, baadhi ya wapiga kura kupewa kura zaidi ya moja, baadhi ya watendaji wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), kuingia vituoni wakiwa na kura mifukoni na kutumbukiza kwa nguvu kwenye masanduku ya kura wakati wa kuhesabu kura.
Dosari nyingine zilizotajwa na Zitto ni baadhi ya wasimamizi wa kura kuziharibu kwa makusudi hususan za wapiga kura wanaobaika ni wa ACT-Wazalendo, ili kuwa na kura nyingi zilizoharibika kumpunguzia ushindi mgombea wa chama hicho.
Leave a comment