June 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Zito Kabwe, kutoka uzalendo hadi usaka tonge

Spread the love

ZITTO Zuberi Kabwe, kiongozi mkuu wa chama cha ACT- Wazalendo, ni ndumilakuwili. Ni kigeugeu. Haaminiki. Anaandika Saed Kubenea … (endelea).

Anataka kupanda farasi wawili kwa wakati mmoja; lakini kwa barabara tofauti. Anasukumwa na maslahi binafsi.

Leo anaweza kusema hili, kesho akasema lile. Jana alisema hili; lakini keshokutwa atasema tofauti na kile alichokieleza juzi, jana na leo.

Pamoja na tabia yake hii kujulikana kwa wengi, bado Zitto anataka aaminike kwa umma.

Jumapili wiki hii, alinukuliwa na vyombo vya habari akisema, “mshindi halali wa uchaguzi wa 25 Oktoba, Tanzania Zanzibar atangazwe.”

Lakini kauli ya Zitto juu ya mgogoro wa kisiasa Visiwani, aliitoa takribani mwezi mmoja tangu pale wabunge wa upinzani walipomtuhumu Dk. Ali Mohammed Shein na John Pombe Magufuli, kuvunja Katiba.

Upinzani ulidai bungeni na unaendelea kusisitiza nje ya Bunge, kwamba Dk. Shein siyo rais halali Visiwani. Naye Magufuli “ameingia Ikulu kwa mlango wa nyuma.”

Kelele za wapinzani zilimsukuma Spika wa Bunge, Job Ndugai, kuamuru wabunge wanaotetea Katiba, watolewe nje ya Bunge. Amri ya spika ikatekelezwa.

Aidha, wiki mbili zilizopita, Zitto huyuhuyu alitoka hadharani kumtetea Prof. Sospeter Muhongo, aliyeteuliwa kuwa waziri wa nishati na madini katika serikali ya Magufuli.

Akiandika katika akaunti yake ya face book, Zitto alisema, “waliosema ufisadi ni mfumo ndio wanasema leo Prof. Muhongo hafai kuwa waziri, kwa sababu ya tuhuma za wizi wa fedha za umma katika akaunti ya Tegeta Escrow.”

Alihoji: “Sijui lini mahakama ilimhukumu Muhongo! Sijui lini Muhongo kawa mfumo. Tujifunze kuweka akiba.”

Prof. Muhongo alikuwa waziri wa nishati na madini wakati wa sakata la Tegeta Escrow.

Zitto anasema kamati ya Bunge ilipendekeza na Bunge likaazimia kuwa Prof. Muhongo avuliwe madaraka yake ya uwaziri. Prof. Muhongo alijiuzulu.

“Akafanyiwa uchunguzi na Kamishna wa Maadili na kutamka kuwa hakukutwa na kosa la kimaadili. Unajengaje hoja kuwa hana haki ya kuteuliwa kuwa waziri?

“Kesha adhibiwa kwa kosa la awali, kwa kujiuzulu. Sheria ipi inasema hana haki ya kuteuliwa tena?

“Niliongoza Kamati ya PAC. Nina uhakika waziri Muhongo kwenye sakata lile alishauriwa vibaya na kujikuta anatetea ubadhirifu…

“Mwenye ushahidi dhidi ya Muhongo si aende mahakamani? Tuache siasa za porojo porojo.” Tuanze kujadili:

Kwanza, undumilakuwili wa Zitto, haukuanza leo, jana wala juzi. Alianza tabia hii wakati akiwa mwanachama katika Chama cha Demokrasia na Maendeo (Chadema).

Hata kufukuzwa kwake ndani ya chama hicho, kulichangiwa na tabia yake hiyo.

Ndani ya Chadema, ambako Zitto alifanikiwa kufikia cheo cha naibu katibu na naibu kiongozi wa upinzani bungeni, alihubiri asiyoamini na kuamini asichohubiri.

Kwa mfano, Zitto aliwahi kusema, yeye atakuwa mtu wa mwisho kuhujumu Chadema. Lakini matendo yake yakawa tofauti na kile alichokuwa akikinena.

Ndani ya Chadema, Zitto alikuwa akishirikiana na wanaokivuruga chama. Wanaotuhumiwa kutaka kuangamiza maisha ya viongozi wakuu wa chama na wanaotajwa kuwa maadui wa chama.

Amekuwa akitajwa kuhusika na njama za kutaka kuondoa viongozi kinyume cha taratibu. Amekuwa akitajwa kuasisi matumizi ya rushwa kipindi cha uchaguzi.

Anadaiwa kukubali kupokea fedha kutoka kwa maadui wa chama kwa lengo la kukidhoofisha, huku akiuhadaa umma kuwa anakipenda chama hicho.

Alikituhumu chama anachodai kukijenga – nje ya vikao – kusheheni ukabila na udini. Akawa anatolea mfano wa mchakato wa kuwapata wabunge wa Viti Maalum mwaka 2005, ambapo alisema wengi walitoka mkoa wa Kilimanjaro.

Lakini ni yeye aliyekuwa Katibu wa Kamati ya kutafuta wabunge wa Viti Maalum. Kama kuna makosa yalifanyika, yeye ndiye alikuwa mhusika mkuu. Asingeweza kujivua tuhuma hizo.

Kama kuna upendeleo, basi ndiye aliyehusishwa zaidi kwa kuhakikisha anampitisha dada yake, Mhonga Saidi.

Katika kipindi chake chote cha kuwa naibu katibu mkuu na mbunge, Zitto hakukisaidia Chadema mkoani Kigoma bali alitumia Chadema kujijenga binafsi.

Pili, Zitto Zuberi Kabwe, anayedai kuguswa na kilichotokea katika uchaguzi wa 25 Oktoba, Unguja na Pemba, hakuwa miongoni mwa wabunge waliopinga uvunjifu wa katiba bungeni.

Hakuwa miongoni mwa waliosimama kupigia kelele wanaovunja katiba. Alibaki kimya. Alishirikiana na wanaovunja katiba. Akaungana na wanaomshangilia Dk. Shein. Akamwagiwa sifa na Magufuli.

Alipohojiwa na waandishi wa habari, Zitto alibeza waliotoka nje ya Bunge. Akawaita wabinafsi.Wanasiasa uchwala.

Akiwa nje ya Bunge na kubaini jinsi upepo wa kisiasa kuhusu Zanzibar unavyovuma kwa mashinikizo ya mabalozi na jumuiya za kimataifa, Zitto amegeuka nyuzi 180 kutoka alipokuwa awali. Anazungumza lugha moja na waliotolewa bungeni.

Tatu, hata utetezi dhidi ya Prof. Muhongo umefuata njia hiyohiyo. Ni kujikomba. Anategemea huruma ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), ili kimsaidie aweze kuwa mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mashirika ya Umma (PAC).

Zitto anayedai kuwa Prof. Muhongo hana kosa, kamati ambayo yeye aliiongoza ilimtuhumu Prof. Muhongo kuwa dalali katika wizi wa fedha ndani ya akaunti ya Tegeta Escrow.

Taarifa ya PAC inaeleza katika ukurasa wa 58, kwamba “Prof. Muhongo ndiye aliyekuwa Dalali Mkuu aliyewakutanisha Bw. Harbinder Sethi na Bw. James Rugemalira.”

Sethi ndiye alijiita mmiliki mpya wa kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL). Rugemalila alikuwa mmiliki wa kampuni ya VIP Engineering and Marketing Limited, iliyokuwa ikimiliki asilimia 30 ya hisa katika IPTL.

Katika mkataba kati ya serikali na IPTL, serikali kupitia Tanesco, ndiyo ilikuwa ikilipia gharama za matengenezo ya mitambo na gharama nyingine za ufundi ikiwamo ununuzi wa vipuri.

Tanesco ndiyo ilikuwa ikinunua mafuta kwa ajili ya kuendeshea mitambo ya IPTL na kisha kampuni hiyo kuiuzia Tanesco umeme inaogharamia kuuzalisha, tena kwa bei kubwa mno.

Ilikubaliwa kuwa mara baada ya mkataba kumalizika, mitambo hiyo ingekuwa mali ya serikali.

Hata hivyo, wakati mkataba unakaribia kufika mwisho ili mitambo ikabidhiwe kwa Tanesco, Prof. Muhongo akaruhusu kampuni ya IPTL kuuzwa kwa mwekezaji mwingine.

Akaagiza Tanesco wajifunge katika mkataba mwingine wa miaka mitano wa kununua umeme kwa muwekezaji mpya.

Hapa ndipo hasa kwenye ufisadi. Kwamba mitambo ambayo tayari ilikuwa iwe mali ya Tanesco, haiwezi tena kurudi mikononi mwa umma.

Ni kwa sababu, Prof. Muhongo ameruhusu kuuzwa kwa mkataba, kinyume na makubaliano ya awali ya mkataba huo. Huyu ndiye anayetetewa na Zitto.

Hatua ya serikali kukubali kujifunga katika mkataba na kampuni mpya, ni kielelezo tosha kuwa kuna wizi umefanyika.

Aidha, ndani ya Bunge, Prof. Muhongo alipatikana na hatia ya kuvunja kifungu cha 29 cha sheria ya fedha ya mwaka 2012.

Kifungu kinamtaka waziri husika, kuthibitisha uuzaji wa hisa, pale makampuni mawili au matatu yanapoamua kuuza hisa zao.

Prof. Muhongo hakufanya hivyo. Yawezekana alijua kuwa nyaraka zilizowasilishwa kwa Wakala wa serikali wa Usajili wa Biashara (BRELA), hazikuwa halali. Zilighushiwa.

Akizungumza kwa sauti ya jeuri, Prof. Muhongo alisema, suala la uhalali wa umiliki wa hisa katika kampuni hizo linahusu wanahisa wenyewe. Serikali haiwajibiki kuingilia mahusiano ya kibiashara ya wanahisa katika kampuni binafsi.

Kitendo cha Prof. Muhongo kushindwa kutimiza wajibu wake, jambo ambalo lilisababisha nyaraka feki kutumika kuhadaa ulimwengu, ndiyo chanzo cha wizi huu.

Zitto anajua yote haya. Anajua kuwa Prof. Muhongo hakuwajibika kisiasa kama anavyodai. Alifukuzwa uwaziri na Bunge kwa kuvunja sheria.

Alituhumiwa kukodisha watu kusambaza uongo bungeni ili kujitakasa. Akatumia fedha za umma kuchapisha na kusambaza nyaraka za uongo kwa wabunge ili kulinda kitumbua chake.

Haingii akilini kwa mtu anayejua ukweli huu, kutetea uhalifu, bila kuwa na ndimi mbili; na bila kutegemea kupata faida au manufaa mengine ya kisiasa na kiuchumi.

Hata kauli ya Zitto kuwa Kamati ya Maadili ya Ikulu, imemsafisha Prof. Muhongo, nayo haina mashiko. Inadhalilisha wananchi na ina vimelea vya hongo. Sababu ni hizi:

Kamati ya maadili ya Ikulu, yenyewe ni mtuhumiwa wa ufisadi wa wizi katika akaunti ya Escrow. Haiwezi kumsafisha mtuhumiwa na wananchi wakakubaliana na utakaso huo.

Baadhi ya wafanyakazi wa Ikulu, wametajwa katika orodha ya wanufaika; na kuna madai kwamba fedha zilichotwa kwa amri ya rais.

Aliyekuwa rais wa Jamhuri wakati huo, Jakaya Kikwete, alionekana kuanzia sura yake, maneno yake na kauli zake, kuwa mmoja wa wanufuikaji wa fedha za wizi.

Mpaka kesho, Kikwete anasumbuliwa na dhambi hii – moyoni, akilini na hadharani. Anashindwa kuficha ushiriki wake yeye na familia yake katika kashfa hii kubwa.

Aidha, mpaka Zitto anamsafisha Prof. Muhongo, umma haujaelezwa majina ya waliokwapua mabilioni ya shilingi kupitia benki ya Stanbic, tawi la Tanzania.

Kauli kwamba kuna fedha za umma zilizokuwa zimehifadhiwa BoT zimekwapuliwa Stanbic, ilitolewa kwa mara ya kwanza na Zitto.

Alisema, kuna watu wamegawana mabilioni ya shilingi ya Escrow kutoka ndani ya benki hiyo, kwa kutumia masanduku na mifuko ya plastiki.

Vilevile, kauli ya Zitto ya kumtetea Prof. Muhongo, sharti ipingwe na kulaaniwa na kila mmoja, kwa kuwa imesheheni dharau kwa umma na Bunge.

Hii ni kwa sababu, kauli ya kutaka wananchi wenye ushahidi kuwasilisha malalamiko yao mahakamani, ni kauli zinazolenga kutetea uhalifu.

Mara kadhaa, wananchi wamezoea kuzisikia kauli hizo kutoka midomoni mwa wezi na watuhumiwa wa ufisadi nchini.

Nani asiyejua kuwa ili uende mahakamani kushitaki ni lazima uwe mwathirika wa moja kwa moja wa tendo unalolilalamikia – Locus standi.

Ushahidi wa hili, ni kesi ya Dowans dhidi ya Tanesco. Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kiligonga mwamba mahakamani pale kilipotaka kuzuia malipo ya fedha za umma zilizokuwa zikidaiwa na kampuni hiyo.

Zitto hafanyi kwa bahati mbaya. Anakusudia. Ana lengo analotaka kutimiza. Anataka kuwa mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya PAC.

Anategemea kuungwa mkono na wabunge wa CCM. Kamati hii ndilo duka la wengi waliojizolea mabilioni ya shilingi kwa ulaghai mkubwa.

Katika hili la kutaka kuwa mwenyekiti wa kamati ya Bunge, Zitto yuko tayari hata kusujudia wachafu. Tusubiri kuona mengine.

error: Content is protected !!