May 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Zembwela aitosa East Afrika Radio, atua Wasafi

Spread the love

ALIYEKUWA mtangazaji wa East Africa Radio na East Africa Television kwa zaidi ya miaka sita, Hillary Daudi ‘Zembwela’ amekihama rasmi kituo hicho na kujiunga na kituo cha Wasafi Media kinachomiliki Wasafi FM na Wasafi TV. Anaripoti Kelvin Mwaipungu … (endelea).

Zembwela ambaye alikua akitangaza kipindi cha Supamix cha East Africa Radio pamoja na kipindi cha Uswazi cha EATV, ameanza kuonekana na kusikika leo kupitia Wasafi FM na Wasafi TV katika kipindi cha uchambuzi wa magazeti na Maulid Kitenge ambaye alitua wiki iliyopita akitokea EFM.

Wasafi Media inayomilikiwa na Msanii Nassibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ ipo katika mkakati wa  kujiimarisha na kuanza vipindi kwa saa 24 kuanzia wiki ijayo, huku tayari baadhi ya vipindi ikiwemo Sports Arena, Sports Court na Block 89 vikiwa vimeanza kuruka na kujipatia mashabiki.

Taarifa kutoka Wasafi Media zinaeleza kuwa, majina makubwa zaidi katika tasnia ya habari yanatarajiwa kutangazwa kujiunga na kituo hicho kuanzia leo Jumatano mpaka Jumapili hii, wakati vipindi vyote vikitarajiwa kuanza kuruka kuanzia Jumatatu ijayo.

Baadhi ya wamiliki wa vyombo vya habari, wameingiwa na hofu kubwa ya kupoteza watangazaji wao mahiri katika usajili mkubwa unaoendelea kufanywa na kituo cha Wasafi Media huku wananchi wengi wakiwa na kiu ya kuona ubora wa vipindi vya kituo hicho.

error: Content is protected !!