July 29, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Z’bar yatikisika

Spread the love

 

HALI ya mambo visiwani Zanzibar si shwari. Yaliyotabiriwa baada ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kumtunuku urais Dk. Ali Mohammed Shein sasa yanadhihiri, anaandika Faki Sosi.

Tayari Jeshi la Polisi visiwani humo limeanza kufunga maduka, kukamata daladala kwa madai ya kufanya ubaguzi wa kisiasa.

Wanachama na wapenzi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) visiwani humo ndio wanaolalamika kubaguliwa na wafanyabiashara pia madereva na makonda wa daladala pale wanapohitaji huduma hizo.

Kutokana na malalamiko hayo, Hamad Rashid Mohammed, Mkuu wa Wilaya ya Wete visiwani humo amefunga maduka matatu pamoja na kuzuia shughuli za usafirishaji zinazofanywa na baadhi ya daladala kati ya Wete na Mtambwe.

Wafanyabiashara wanaotajwa kufungiwa maduka yao ni Titi Juma Othman, Sai Juma Seif pamoja na Hamad Haji.

Mkuu huyo wa wilaya (Mohammed) amedai kwamba, wamelazimika kufunga maduka hayo baada ya kujiridhishwa kuwa, wafanabiashara hao wanauza bidhaa kwa misingi ya itikadi za kisiasa.

Mohammed amesema, suala hilo atalifikisha wizarani kutokana na ukiukwaji huo wa leseni ili hatua za kisheria zichukuliwe.

Kutokana na ZEC kuvuruga matokeo ya uchaguzi halali wa tarehe 25 Oktoba mwaka jana, kada mbalimbali zililaumu hatua hiyo kwamba ingeweza kusababisha chuki na uhasama wa kisiasa kama ilivyokuwa mwaka 1995.

ZEC chini ya kada wake, Jecha Salima Jecha ilifuta matokeo ya tarehe 25 Oktoba mwaka jana yaliyokuwa yakielekea kumpa ushindi Maalim Seif Sharif Hamad, aliyekuwa mgombea wa Chama cha Wananchi (CUF) dhidi ya Dk. Shein wa CCM kwa madai ya kuwepo kwa kasoro.

Jecha alifuta matokeo hayo kinyume cha sheria ikiwa tayari ametangaza zaidi ya nusu ya majimbo ya uchaguzi huo visiwani humo jambo ambalo lilitabiriwa kurejesha uhasama wa kisiasa.

Wakati Serikali ya Dk. Shein ikichukua hatua ya kufunga maduka na kuzuia daladala kwa madai ya ubaguzi wa kisiasa, Maalim Seif amewataka Wazanzibar kuonesha msimamo wao wa kutoshirikiana na rais huyo.

Ametoa kauli hiyo jana alipozungumza na viongozi wa chama hicho Micheweni, Kaskazin Pemba ambapo amesema;

“Tukikazana serikali hii itaondoka lakini ikiwa mnangoja Maalim Seif au Marekani kuiondoa, kwa sheria ya kimataifa haiwezekani kwani Marekani haiwezi kuingilia mambo ya ndani ya Zanzibar.”

Jecha alimpa ushindi Dk. Shein baada ya uchaguzi haramu ulifanyika tarehe 20 Machi mwaka huu.

error: Content is protected !!