July 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Z’bar kudhibiti Dawa za Kulevya

Spread the love

OFISI ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, imeikabidhi Wizara ya Afya vifaa vya maabara vyenye uwezo wa kubaini dawa za kulevya. Anaandika Mwansihi Wetu … (endelea).

Akikabidhi vifaa hivyo kwa Naibu Katibu wa Wizara ya Afya, Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Dk. Omar Dadi Shajak amesema, kuna umuhimu wa kuvitunza na kuvitumia vifaa hivyo kwa njia zilizo sahihi ili viweze kuleta tija katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya nchini.

Ametoa wito kwa jamii hasa wadau wakuu wanaohusika na mapambano dhidi ya dawa za kulevya kufanya kazi kwa ushirikiano ili kuhakikisha kuwa mapambano hayo yanafanikiwa.

Amesema Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais kupitia Tume ya Kuratibu na Udhibiti wa Dawa za Kulevya Zanzibar itaendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo ili kusaidia upatikanaji wa vifaa vya kisasa katika kufanikisha mapambano hayo.

Amelishukuru Shirika la Umoja wa Mataifa la Kupambana na Dawa za Kulevya na Uhalifu Duniani (UN ODC) kwa kutoa vifaa hivyo vya dawa na kuwaomba washirika wengine wa maendeleo kusaidia juhudi hizo.

Mapema akipokea vifaa hivyo katika hafla iliyofanyika Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Migombani, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Halima Maulid Salum ameishukuru Ofisi hiyo kwa jitihada zake inazochukua katika kukabiliana na dawa za kulevya na kuahidi kuvitumia vifaa hivyo kwa uangalifu mkubwa.

Naye Mkemia Mkuu wa Serikali Zanzibar Dk. Slim Rashid Juma amesema, vifaa hivyo vitasaidia na kurahisisha uchunguzi wa dawa za kulevya na kuweza kutofautisha kwa haraka baina ya dawa hizo na kemikali.

Amesema matarajio ya maabara yao ni kuwa na vifaa vya kisasa kwa ajili ya kurahisisha na kuwezesha kufanya uchunguzi wa aina zote za dawa za kulevya, kwa lengo la kuondosha usumbufu wa kusafirisha sampuli kwenda Tanzania Bara.

error: Content is protected !!