August 10, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Zanzibar yaiponza Tanganyika

Spread the love

UCHAGUZI wa marudio uliofanyika tarehe 20 Machi 2016, na Sheria ya Makosa ya Mtandaoni iliyopitishwa na Bunge kwa haraka haraka mwaka jana, vimeanza kuleta madhara kwa Tanzania Bara, baada ya Marekani kufuta msaada wa zaidi ya Tsh 1 trilioni kwa Tanzania, anaandika Josephat Isango.

Marekani, kupitia Shirika la Changamoto za Milenia (MCC), imeiondoa Tanzania katika nchi zinazostahili kupewa Tsh 1.4 trilioni za ngwe ya pili ambazo zingeelekezwa katika miradi ya umeme, maji, afya na barabara.

Bodi ya MCC iliyoketi juzi ilisema kuwa Tanzania imekosa sifa kwa kuvunja misingi waliyokubaliana ikiwa ni pamoja na kusimamia misingi ya kidemokrasia na kutotunga sheria zinazokandamiza uhuru wa wananchi kujieleza.

Kuna uwezekano wa Tanzania kukosa misaada mingine kutoka nchi ya Jumuiya ya Ulaya, iwapo haitafanya jitihada za wazi kusahihisha makosa hayo.

Kwa uamuzi huo, serikali ya Tanzania itapaswa kutafuta fedha kwenye vyanzo vingine ili kukamilisha miradi iliyokuwa inafadhiliwa na MCC, mfano barabara ya Sumbawanga hadi Tunduma, na barabara zingine mkoani Tabora, Katavi na Rukwa.

Uchaguzi wa marudio wa Zanzibar wa 20 Machi umelalamikiwa kuwa si halali kwani Jecha Salim Jecha, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC,) hakuwa na mamlaka ya kisheria wala kikatiba kufuta uchaguzi wa Oktoba 25 mwaka jana.

Mgogoro uliopo sasa unaosababisha nchi kukosa misaada umesababishwa na Jecha, ukapewa baraka za CCM, sababu CCM hawakukubali matokeo yasiyowapa ushindi, ili Dk Ali Mohamed Shein abaki madarakani Zanzibar.

Benson Kigaila, Mkurugenzi wa Oganaizesheni, Mafunzo na Usimamizi wa Kanda wa Chadema, anasema kitendo cha Rais John Magufuli kupuuza suala la Zanzibar kinaathiri zaidi Tanzania Bara kwani misaada ya MCC mingi haikuwa inaelekezwa Zanzibar.

“Serikali ya Magufuli haina pesa za kutosha hata kulipa mishahara ya wafanyakazi. Kwa hiyo kama alipuuza Zanzibar akidhani kuwa Bara hawataathirika, tusubiri tuone shida zitakazowakabili hata wafanyakazi wa Bara, ndio utaona kuwa tumefanya vibaya sana kukataa kufuata matakwa ya demokrasia kwa sababu ya ulafi wa madaraka uliotufikisha hapa.”

Wakati wa mkutano wa 16 na 17 wa Bunge, David Kafulila aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), alidokeza kwamba Marekani ingesitisha msaada kwa ajili ya miradi ya MCC, lakini alipingwa vikali na Profesa Sospeter Muhongo, aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini.

Tayari vyama vya siasa na wachumi kadhaa wameonya serikali na kuitaka ipeleke bungeni marekebisho ya sheria inayolalamikiwa.

Lakini serikali inasema ilitarajia hatua kama hiyo kutoka kwa MCC, hivyo ilijiandaa mapema kukabiliana na uamuzi huo.

Akizungumza na MwanaHALISI Online, Dk Philip Mpango, Waziri wa Fedha na Mipango, amesema baada ya kuona tishio la wahisani mara kwa mara serikali iliondoa mabilioni hayo ya wahisani katika bajeti ya mwaka 2016/17.

“Sisi hatujapata kwa maandishi barua kutoka MCC. Badala yake tunaona kwenye mitandao kama nyie. Hatujui wamesitisha kwa muda gani na watakaporejesha watatoa masharti gani. Cha msingi sasa sisi tusisitize kukusanya mapato ya ndani ili tuweze kujitegemea,” amesema Mpango.

Bashiru Ally, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, anasema kiwango cha pesa ambacho Tanzania itakosa ni kikubwa kwa nchi masikini, hivyo miradi mingi ya umeme, maji, afya, barabara itaathirika.

error: Content is protected !!