August 10, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Zanzibar kinakaribia kunuka

Spread the love

MAALIM Seif Shariff Hamad, anayeaminika kuwa ndiye mshindi halali wa uchaguzi mkuu wa 25 Oktoba, amegoma kufanya mazungumzo yoyote na Dk. Ali Mohamed Shein, aliyetangazwa kuwa mshindi wa urais, anaandika Jabir Idrissa.

Akizungumza na waandishi wa habari Vuga mjini Unguja, Maalim alisema, “siwezi kukutana na Dk. Shein na kujadiliana naye kwa lolote kuhusu mustakabali wa Zanzibar.”

Amesema,“…nikutane na Dk. Shein kwa lipi? Nakutana naye kama nani? Siwezi kufanya mazungumzo juu ya mustakabali wa Zanzibar na mtu ambaye yuko madarakani kwa kuvunja katiba.”

Maalim ameeleza hayo wakati akijibu swali la mmoja wa waandishi wa habari Visiwani. Ni muda mfupi baada ya Kaimu Mwenyekiti wa chama hicho, Twaha Taslima, kusoma maazimio ya Baraza Kuu la Taifa la chama hicho.

Seif alikuwa i na kuweka msisitizo kwamba hakutakuwa na mazungumzo yoyote na kiongozi huyo ambaye kwa msimamo wa CUF hakupata ridhaa ya wananchi ya kuongoza Zanzibar.

Mwanasiasa huyo machachari Visiwani amesema, msimamo wake pamoja na CUF, ni kutomtambua Dk. Shein kama rais na kutoshirikiana naye kwa lolote na serikali atakayaoiunda.

Akijibu madai ya kwa nini anaendelea kutumia rasimali za serikali wakati haitambui serikali iliyopo, Maalim amesema, “nitaendelea kutumia walinzi na gari za serikali kwa sababu ni stahiki zangu.

“Situmii huduma hizi kama zawadi. Hapana. Hizi ni haki zangu kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka (1984), Toleo la 2010.

Maalim Seif alikuwa makamo wa rais katika serikali iliyopita. Kabla ya kuanza mfumo wa vyama vingi, Maalim aliwahi kushika madaraka ya waziri kiongozi.

Amesema, kwa msingi huohuo, ni haki yake kutibiwa na kugharamiwa matibabu ndani na nje ya nchi.

“Ni stahiki zangu kikatiba. Mimi ni kiongozi tena mkubwa tu. Kwa yale yanayonistahiki kufanyiwa kisheria, isionekane kuwa siitambui serikali kwa hivyo nisihudumiwe. Ni haki yangu… isitoshe hizi fedha ni za wananchi nami nachangia kodi ama anavyochangia wengine. Hizi fedha hazitoki mfukoni mwa viongozi wa CCM,” ameeleza.

Kwa sehemu kubwa Maalim Seif alijibu maswali yaliyoelekezwa moja kwa moja kwake binafsi; na alitoa ufafanuzi kidogo kwa yale yaliyohusu zaidi uchaguzi wa Zanzibar na hatima ya mgogoro uliotengenezwa na Chama Cha Mapinduzi.

Akijibu maswali juu ya msimamo wa Baraza Kuu, Taslima ambaye aliteuliwa Oktoba mwaka jana kuongoza kamati ya uongozi ya chama baada ya Profesa Ibrahim Lipumba kujiuzulu, alisema kuwa CUF itaendelea kutumia njia za kidemokrasia kupigania haki yake ya ushindi wa uchaguzi mkuu wa 25 Oktoba.

Uchaguzi mkuu huru na haki wa rais, wawakilishi na madiwani, ulifutwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, Jecha Salim Jecha tarehe 28 Oktoba, kinyume na katiba na sheria za nchi.

Tasrima ambaye ni wakili wa Mahakama Kuu amesema, “tunaamini kwa njia hii, hatutafika mbali wanaokalia madaraka bila ya ridhaa ya wananchi wa Zanzibar watatambua kuwa wanapaswa kurudisha haki ya wananchi na kuipa CUF mamlaka ya kuongoza dola.”

Katika uchaguzi huo wa marudio ambao CUF inashikilia kuuita, “uchaguzi haramu na batili kisheria,” Jecha alimtangaza Dk. Shein kuwa mshindi kwa kudai kuwa amepata 399,981, sawa na asilimia 91 ya kura zilizopigwa.

Aidha, akatangaza kuwa CCM kimeshinda viti vyote 54 vya uwakilishi, Unguja na Pemba.

error: Content is protected !!