June 30, 2022

Uhuru hauna Mipaka

ZANU PF yameguka mapande mawili

Rasi wa Zimbabwe Robert Mugabe

Spread the love

CHAMA tawala nchini Zimbabwe cha ZANU-PF kinakabiliwa na mpasuko mkali baada ya mwanachama wake, Didymus Mutasa aliyefukuzwa, kuahidi kuunda chama kipya ili kumpa changamoto Rais Robert Mugabe.

Kwa mujibu wa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), Didymus Mutasa amesema kuwa chama hicho kipya kitakachoanzishwa pia kitaitwa ZAZU-PF lakini herufi PF yao itasimama badala ya maneno”People First” na siyo “Patriotic Front” inayotumiwa na kile cha Rais Mugabe.

Hivi karibuni ZANU-PF ilimfukuza Mutasa na wanachama wengine waandamizi akiwemo aliyekuwa Makamu wa Rais Joice Mujuru, baada ya kuwatuhumu kupanga njama za kumtoa madarakani Rais Mugabe mwaka uliopita, ingawa wanachama hao wamekana madai hayo.

Mujuru ndiye anatajwa kukiongoza chama hicho kipya kitakachoundwa kukabiliana na Mugabe ambaye huenda akagombea tena kiti cha urais katika uchaguzi wa mwaka 2018. Rais huyo mkongwe barani Afrika mwenye miaka 91, ameiongoza Zimbabwe tangu ipate uhuru wake mwaka 1980.

Kwa sasa Rais Mugabe, anafanya ziara yake ya kwanza katika nchi jirani ya Afrika Kusini katika kipindi cha zaidi ya miaka ishirini.

Ziara hiyo iliyoanza Jumanne wiki hii, inakuja huku Zimbabwe ikikabiliwa na matatizo ya kiuchumi na mgawanyiko ndani ya chama chake tawala cha ZANU-PF.

Waziri wa habari wa Zimbabwe, Jonathan Moyo, ametupilia mbali taarifa kwamba ziara ya Rais Mugabe nchini Afrika Kusini inalenga kuomba msaada.

Rais Mugabe ndiye mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU) na Jumuia ya Maendeleo ya Kiuchumi kwa nchi za Kusini mwa Afrika (SADC).

error: Content is protected !!