May 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Zambia kuwakosesha ajira 30,000 Tanzania

Bandari Dar es Salaam Tanzania

Spread the love

 

IWAPO Kanuni za Usafirishaji Mizigo Mizito na Kichele za nchini Zambia zitaanza kutumika, zaidi wa Watanzania 30,000 wana hatihati ya kukosa ajira. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Kanuni hizo za mwaka 2021 zimekuja ikiwa imepita miaka 15 tangu Sheria ya Uwezeshaji Kiuchumi Wananchi (2006) kupitishwa nchini Zambia.

Hatihati ya Watanzania hasa madereva 30,000 kukosa ajira imeanishwa na Katibu Mtendaji wa Chama cha Mawakala wa Forodha Tanzania (TAFFA), Elitunu Malamia wakati akizungumza na waandishi wa habari mkoani Dar es Salaam.

Malamia amesema, nchi ya Zambia pamoja na kusaini Itifaki za Jumuiya ya MaendeleoKusini mwa Afrika (SADC), imetengeneza kanuni ambazo zinakiuka dhana ya ushindani wa kibiashara katika upande wa usafirishaji.

Amesema iwapo Kanuni hiyo ya Usafirishaji Mizigo Mizito na Kichele ya 2021 itaruhusiwa kutumika Watanzania 30,000 watakosa ajira za moja kwa moja huku zaidi ya watu laki tano wakiathirika.

Mtendaji huyo wa TAFFA amesema, kanuni hizo za Zambia zinataka asilimia 50 ya magari ya kusafirisha mizigo kutoka bandari ya Dar es Salaam yaendeshwe na raia wa Zambia, asilimia 30 mizigo ibebwe na Treni kupitia Reli ya Tanzania na Zambia (Tazara) na asilimia 20 ibebwe na magari ya Watanzania.

“Sisi TAFFA, Chama cha Wamiliki wa Malori Tanzania (TATOA) na Chama cha Wasafirishaji (TAT), tunaomba Serikali izungumze na wenzetu wa Zambia waachane na kanuni hizo kwa kuwa zinakiuwa sheria za ushindani kibiashara lakini pia zinavunja Itifaki ya SADC ambayo Zambia ni wanachama,” amesema.

Malamia amesema, kwa sasa zaidi ya malori 25,000 yanasafirisha mizigo nje ya nchi na asilimia 70 ya mizigo inaenda Zambia na Demokrasia ya Congo sawa na malori takribani 17,000 hivyo iwapo hakutakuwa na mabadiliko ya kanuni hizo maumivu yatakuwa makubwa kwa nchi.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa TATOA, Elias Lukumay amesema, kanuni hizo hazihatarishi ajira pekee za madereva wa Tanzania ila hata mapato yatapungua akitolea mfano kuwa kwa siku moja zaidi ya malori 1,000 yanaenda nje ya nchi ambapo yanatumia mafuta zaidi lita milioni 2.

“Lori moja linaweka lita 2,000 za mafuta hivyo Serikali inaingiza kodi, ukipiga hesabu kwa lori 25,000 ni fedha nyingi zitapotea. Lakini pia kuna kulipia vibali vya hati ya kusafiria tutapoteza fedha, niombe Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki aingilie kati kwani athari itakuwa kubwa,” amesema.

Lukumay amesema, bandari ya Dar es Salaam ni langu kuu la biashara ambapo asilimia 40 ya mizigo inayoingia nchini inapita hapo hivyo kutopata ufumbuzi wa kadhia hiyo Watanzania wengi watateseka.

Makamu Mwenyekiti huyo alisema mikakati ya Bandari ya Dar es Salaam ni kupitisha tani milioni 30 kwa mwaka kutoka tani milioni 17 ila hofu yao ni kuwa iwapo kanuni hizo za Zambia zitafanya kazi lengo hilo halitatimia.

Amesema kwa miezi mitatu ambayo Rais Samia Suluhu Hassan ameingia madarakani kumekuwepo na mabadiliko makubwa ndani ya bandari ila uendelevu wake utaonekana kama kutakuwepo na bishara huria kwa nchi wananchima wa SADC.

“Miezi mitatu ya Rais Samia tumeshuhudia upanuzi wa barabara ya kuingia bandarini, maboresho kwenye kushusha na kupakia mizigo, maamuzi yanafanyika kwa pamoja kati ya Serikali na wadau. Haya yote yanaweza kuonekana ya muhimu iwapo hili la Kanuni za Zambia litapata ufumbuzi kwa kuwa Zambia ni nchi ya pili kwa kupitisha mizigo nchini,” amesema.

Lukumay amesema, wao kama wadau wakuu wa sekta ya usafirishaji wanafarijika na namna Serikali inashiriki kutatua changamoto na kuahidi kuongeza ushirikiano na Serikali kuhakikisha bandari ya Dar es Salaam inafanikiwa kupokea na kupitisha mzigo wa tani milioni 30.

Makamu huyo amesema, kwa sasa Kamati ya Kuboresha Huduma Bandarini (PIC) inafanya kazi kwa kiwango cha kuridhisha hali ambayo kwa miezi mitatu hii ya Rais Samia hali imebadilika.

“Kulikuwa na utaratibu mbaya sana pale bandarini, mfano dereva anaingiza gari anaambiwa atoe fedha, barabara mbaya na mengine mengi ila kwa sasa yametatuliwa,” amesema.

Amesema changamoto ambazo bado zipo zinaendelea kutatuliwa hali ambayo inatoa matumaini ya kuifanya bandari kuwa bora zaidi.

error: Content is protected !!