May 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Zahanati zachelewa kufunguliwa kisa uhaba wa watumishi

Naibu Waziri Ofisi ya Rais-Tamisemi, Dk. Festo Dugange

Spread the love

 

MBUNGE wa Kilwa Kaskazini (CCM), Francis Ndulane, amesema uhaba wa watumishi wa umma, unasababisha baadhi ya zahanati jimboni humo, kuchelewa kufunguliwa. Anaripoti Nasra Bakari, DMC … (endelea).

Ndulane ameyasema hayo leo Jumatatu, tarehe 31 Mei 2021, katika kipindi cha maswali na majibu, jijini Dodoma.

Mbunge huyo wa Kilwa Kaskazini, ameihoji Serikali, lini itapeleka watumishi wa afya jimboni humo, ili kuondoa tatizo la uhaba wa watumishi wa afya.

“Je, serikali ina mpango gani wa haraka wa kupeleka watumishi wa idara ya afya, katika Jimbo la Kilwa Kaskazini, ambalo lina uhaba mkubwa wa watumishi. Kiasi cha kufanya baadhi ya zahanati kutoa huduma duni na nyingine kuchelewa kufunguliwa,” amesema Ndulane.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri Ofisi ya Rais- Tamisemi, Dk. Festo Dugange, amesema hivi karibuni Serikali itaajiri watumishi wa kada za afya mbalimbali, na kwamba baadhi yao watapangia jimboni humo.

“Mwezi Mei 2021, Ofisi ya Rais-Tamisemi, imetangaza nafasi 2,726 za ajira za kada mbalimbali za afya. Watumishi hao watapangwa kwenye vituo vya kutolea huduma za afya kote nchini,” amesema Dk. Dugange.

Dk. Dugange amesema “kwa kutoa kipaumbele kwenye vituo vya kutolea huduma za afya, vyenye upungufu mkubwa wa watumishi, ikiwemo baadhi ya vituo katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa.”

Aidha, Dk. Dugange amesema mpango wa Serikali ni kuendelea kuajiri watumishi hao, ili kutatua uhaba wa watumishi katika hospitali, vituo vya afya na zahanati za umma nchini.

error: Content is protected !!