August 13, 2022

Uhuru hauna Mipaka

‘Yowe’ la Lipumba lamuibua Leticia

Spread the love

SIKU moja tangu Profesa Ibrahim Lipumba, aliyekuwa mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) taifa, alalamikie kitendo cha Baraza Kuu la Uongozi kumsimamisha uanachama, Leticia Mosore aliyekuwa makamu mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, naye Amelia na chama chake akisema, ‘naonewa’, anaandika Pendo Omary.

11 Agosti mwaka huu, NCCR Mageuzi ilitangaza kumsimamisha uanachama na uongozi mwanamama huyo. Leticia anakumbukwa kama miongoni mwa viongozi wa NCCR walioitisha mkutano na wandishi wa habari mwaka jana na kupinga ushirikiano wa vyama vya UKAWA.

Barua ya kumsimamisha Leticia inasomeka, “Chama cha NCCR- Mageuzi kilikutana katika kukao chake cha Halmashauri Kuu ya Taifa cha kawaida tarehe 16 Julai, 2016, ambapo pamoja na mambo mengine kilikusimamisha uongozi na uanachama.”

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Mosore amesema barua hiyo nyenye kumbukumbu Na. NCCRM/KM/15/15, ina mapungufu kwasababu haielezi sababu za kumsimamisha.

“James Mbatia (Mwenyekiti wa NCCR), amekiuka Katiba ya chama ya mwaka 1992, yenye marekebisho ya mwaka 2014, Ibara ya 10 inayotoa haki ya kujitetea mbele ya kikao, binafsi sikuitwa kwenye kikao hicho ili kujieleza na kujitetea kwa tuhuma wanazonituhumu,” amesema.

Leticia amedai kuwa, mwaliko alioupata ulikuwa ni barua ya kuhudhuria kikao hicho kama makamu mwwenyekiti na kusema hatua aliyochukuliwa dhidi yake, iliwahi kuchukuliwa pia dhidi ya Mbatia mnamo mwaka 2012.

“Katika kipindi hicho, wajumbe 21 sawa na asilimia 70 ya wajumbe wa Halmashauri Kuu, walisaini waraka wa kumkataa wakimtuhumu kwa kukidhoofisha chama lakini Mbatia alipewa siku 14 ili ajitetee. Inakuaje mimi sijapewa fursa hiyo,” amesema Leticia.

Hata hivyo, MwanaHALISI online limeona barua hiyo ya kumsimamisha Leticia Mosore, ambapo imehitimisha kwa kusema, “Aidha, unayo haki ya kikatiba kukata rufaa ndani ya vikao vya chama.”

 

error: Content is protected !!